2 Timotheo Utangulizi
NEN

2 Timotheo Utangulizi

Utangulizi
Huu ulikuwa waraka wa mwisho kabisa wa Paulo. Baada ya kuandika waraka wa kwanza kwa Timotheo msaidizi wake, Paulo alikamatwa na kurudishwa gerezani huko Rumi. Katika waraka huu, Paulo alihisi fursa zake za kuhubiri Injili zilikuwa zikifikia kikomo. Alimkumbusha Timotheo kwamba hata kama maisha yake hapa duniani yangekoma, Mungu alikuwa amemwandalia maisha ya milele. Paulo pia alimkumbusha juu ya uaminifu wa Mungu ambaye alikuwa amemwongoza katika maisha yake yote. Aligusia nyakati za hatari ambazo zingekuja, na siku za taabu ambapo watu wangeiacha kweli na kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
Alijitahidi kumtia moyo Timotheo na kumwimarisha kwa ajili ya kazi kubwa aliyokabidhiwa. Paulo alitamani kumwona Timotheo tena, akimwomba amletee vile vitabu alivyokuwa ameviacha Troa.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Kusudi
Kumpa maelekezo ya mwisho, na kumtia moyo Timotheo, mchungaji wa kanisa la Efeso.
Mahali
Rumi.
Tarehe
Kati ya 66-67 B.K.
Wahusika Wakuu
Paulo, Timotheo, Luka, Marko.
Wazo Kuu
Barua hii inazungumzia uweza wa Mungu juu ya vitu vyote. Ingawa kuna mateso ambayo yataendelea kuongezeka, Mungu bado anatawala.
Mambo Muhimu
Kumwelekeza Timotheo ajitahidi kujionyesha kuwa amekubalika na Mungu, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, akilitumia kwa usahihi neno la kweli.
Mgawanyo
Shukrani za Paulo kwa ajili ya Timotheo (1:1-5)
Maagizo ya Paulo kwa Timotheo (1:6–2:2)
Sifa za mtumishi mwaminifu (2:3-26)
Mateso yajayo (3:1-17)
Maneno ya mwisho (4:1-22).

Kiswahili Contemporary Version (Neno: Biblia Takatifu)

Copyright ©1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.® Used by permission.

All Rights Reserved Worldwide Printed.

Learn More About Neno: Bibilia Takatifu 2014