Mithali 16
NEN

Mithali 16

16
1 # Mt 10:19; Mit 19:21 Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu,
bali jibu la ulimi hutoka kwa Bwana.
2 # 1Sam 16:7; 2Nya 6:30; Lk 16:15; Dan 5:27 Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,
bali makusudi hupimwa na Bwana.
3 # 2Nya 20:20; Za 20:4 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,
nayo mipango yako itafanikiwa.
4 # Isa 43:7; Kut 9:16; 2Nya 34:24; Rum 9:22 Bwana hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe;
hata waovu kwa siku ya maangamizi.
5 # Za 40:4; Mit 6:16; 11:20-21 Bwana huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo.
Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa.
6 # Kut 20:20; Mit 14:16; Dan 4:26 Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa;
kwa kumcha Bwana mtu hujiepusha na ubaya.
7 # Kol 1:10; Mwa 39:21; Za 105:15; Yer 39:12; 40:1; 42:12; Dan 1:9 Njia za mtu zinapompendeza Bwana,
huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani.
8 # Za 37:16; Mit 15:16; 17:1; Mhu 4:6 Afadhali kitu kidogo pamoja na haki
kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
9 # Yer 10:23 Moyo wa mtu huifikiri njia yake,
bali Bwana huelekeza hatua zake.
10 # Mit 17:7 Midomo ya mfalme huzungumza kwa hekima ya kiungu,
wala kinywa chake hakipotoshi haki.
11 # Law 19:36; Mit 11:1; Eze 45:10 Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Bwana;
mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye.
12 # Mit 26:28; 25:5; 29:14; 31:5 Wafalme huchukia sana kutenda maovu,
kwa maana kiti cha ufalme hufanywa imara kwa njia ya haki.
13 # Mit 22:11 Wafalme hufurahia midomo ya uaminifu;
humthamini mtu asemaye kweli.
14 # Mwa 40:2; Ay 29:24 Ghadhabu ya mfalme ni mjumbe wa mauti,
bali mtu mwenye hekima ataituliza.
15 # 2Nya 36:16; Mit 29:1; Yer 19:11 # Mwa 40:2; Ay 29:24; Mit 19:12; 25:2-7 Uso wa mfalme ungʼaapo, inamaanisha uhai;
upendeleo wake ni kama wingu la mvua wakati wa vuli.
16 # Za 49:20; Ay 28:15; Mit 3:13-14 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu,
kuchagua ufahamu kuliko fedha!
17 # Mit 4:24-27; Isa 35:8; Mdo 24:16 Njia kuu ya wanyofu huepuka ubaya;
yeye aichungaye njia yake, huchunga maisha yake.
18 # Es 5:12; Mit 29:23 Kiburi hutangulia maangamizi,
roho ya majivuno hutangulia maanguko.
19Ni afadhali kuwa mnyenyekevu katika roho
miongoni mwa walioonewa
kuliko kugawana nyara pamoja na wenye kiburi.
20 # Isa 30:18; Za 32:10; Yer 17:7 Yeyote anayekubali mafundisho hustawi,
tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Bwana.
21 # Mit 16:23 Wenye hekima moyoni huitwa wenye ufahamu,
na maneno ya kupendeza huchochea mafundisho.
22 # Mit 10:11 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwa wale walio nao,
bali upumbavu huleta adhabu kwa wapumbavu.
23 # Ay 15:5; Mit 16:21 Moyo wa mtu mwenye hekima huongoza kinywa chake,
na midomo yake huchochea mafundisho.
24 # Mit 24:13-14 Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali,
ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.
25 # Mit 12:15; 14:12; Es 3:6 Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu,
bali mwisho wake huelekeza mautini.
26 # Mit 9:12; Mhu 6:7 Shauku ya mfanyakazi humhimiza kufanya kazi;
njaa yake humsukuma aendelee.
27 # Yak 3:6 Mtu mbaya kabisa hupanga mabaya,
maneno yake ni kama moto uunguzao.
28 # Mit 14:17; 17:9 Mtu mpotovu huchochea ugomvi,
nayo maongezi ya upuzi hutenganisha marafiki wa karibu.
29Mtu mkali humvuta jirani yake
na kumwongoza katika mapito yale mabaya.
30 # Mit 6:13 Yeye akonyezaye kwa jicho lake anapanga upotovu;
naye akazaye midomo yake amenuia mabaya.
31 # Mit 20:29 Mvi ni taji ya utukufu;
hupatikana kwa maisha ya uadilifu.
32 # Mit 19:11 Ni afadhali mtu mstahimilivu kuliko shujaa,
mtu anayeitawala hasira yake kuliko yule autekaye mji.
33 # Yos 7:14; Yn 1:7 Kura hupigwa kwa siri,
lakini kila uamuzi wake hutoka kwa Bwana.

Kiswahili Contemporary Version (Neno: Biblia Takatifu)

Copyright ©1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.® Used by permission.

All Rights Reserved Worldwide Printed.

Learn More About Neno: Bibilia Takatifu 2014