1 Wamakabayo UTANGULIZI WA VITABU VYA WAMAKABAYO
SRUVDC

1 Wamakabayo UTANGULIZI WA VITABU VYA WAMAKABAYO

UTANGULIZI WA VITABU VYA WAMAKABAYO
Vitabu viwili vya Wamakabayo havikupokelewa na Wayahudi na Waprotestanti katika orodha yao ya vitabu rasmi. Lakini Kanisa Katoliki toka zamani, lilivitazama kuwa vitakatifu kama vitabu vingine vya Biblia. Vitabu hivi vinasimulia vita vya Wayahudi na wafalme Waseleusidi, vita vya kupata uhuru wa dini na siasa. Vitabu vimepata jina la shujaa mkuu wa vita hivyo, ndiye Yuda, aliyepewa jina jingine: Makabayo (1 Mak 2:4).
KITABU CHA KWANZA CHA
WAMAKABAYO
UTANGULIZI
Kitabu cha kwanza cha Wamakabayo, katika sura za mwanzoni mwanzoni kinataja makundi mawili ya maadui wanaopiga vita; Kwa upande mmoja wanasimama watu wateteao ustaarabu wa Kigiriki, yaani wafuasi wa mfalme Antioko Epifani aliyenajisisha hekalu. Baadhi ya Wayahudi wengine wanamwunga mkono. Kwa upande wa pili yuko Matathia pamoja na kundi la Wayahudi walio waaminifu wa Torati na hekalu. Kitabu kimegawanyika katika sehemu kuu tatu:
1. Mashujaa wa Yuda Makabayo (3:1—9:22) ambaye anakufa vitani mwaka 160 K.K.
2. Mashujaa wa Yonathani halifa wa nduguye Yuda (9:23—12:53). Wakati wa Yonathani watu mbalimbali wa ukoo wa Waseleusidi wanapigana vita wajipatie ufalme. Yonathani anafaulu kuyafaidi magomvi hayo. Anapewa cheo cha ukuhani mkuu.
3. Simoni aliwaletea Wayahudi uhuru kamili katika dini na katika siasa (13:1—16:24). Akauawa mwaka 135 K.K.
Kitabu kimeandikwa na Myahudi fulani aliyeishi katika Nchi Takatifu kunako 100 K.K. Kimeandikwa katika lugha ya Kiebrania, lakini nakala tuliyo nayo ni tafsiri ya Kigiriki.
Ingawa mtungaji anasimulia habari zake kirefu na kutaja mambo madogo madogo, nia yake hasa ni ya kidini wala si kueleza historia. Masumbufu yanayolikabili taifa kadiri ya maelezo ya mtungaji wa kitabu ni adhabu ya Mungu kwa dhambi zake. Wanafaulu kupigana kishujaa kwa msaada wa Mungu tu. Mtungaji mwenyewe anapigania imani yake. Anafahamu wazi kwamba vita hivi ni vita kati ya upagani na mila za mababu. Yeye ni mkana ustaarabu wa Kigiriki. Anawapenda kwa moyo wote mashujaa wanaopigania Torati na hekalu, na kulipatia taifa uhuru wa kidini na wa kisiasa. Anasimulia vita vilivyookoa “Utaifa wa Kiyahudi”, taifa lililochaguliwa na Mungu kutuletea wokovu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Learn More About Swahili Revised Union Version