UTANGULIZI
Kitabu cha Baruku hakipo katika Biblia ya Kiebrania. Kanisa lilikichukua toka kwa tafsiri ya Biblia ya Kigiriki (Septuaginta) na kukichukulia kama kitabu rasmi tangu zamani za kale. Wayahudi na Waprotestanti hawakichukulii kama kitabu rasmi kwa sababu hakipo katika Biblia ya Kiebrania.
Kitabu hicho ni mkusanyo wa maandishi yenye tabia ya utungaji mbalimbali. S. 1:15—3:8 ni sala ya kuungamia dhambi na sala ya kutumainia huruma ya Mungu. S. 3:9—4:4 ni utenzi wa hekima. S. 4:5—5:9 ni andiko la kinabii. Vulgata inaunganisha kitabu hiki na kitabu “Waraka wa Yeremia”, yaani sura ya 6 ya Baruku. Dibaji ya kitabu inamtaja Baruku, mwandishi wa nabii Yeremia kama mtungaji wa kitabu (1:1-14). Lakini tabia ya utungaji katika sehemu mbalimbali inaonesha zaidi kwamba sehemu fulani fulani zimeandikwa na mtu mwingine, au na watu mbalimbali. Baadaye mkusanyaji fulani akaziunga ziwe kitabu kimoja na kukiweka chini ya jina la Baruku, mtu maarufu. Watungaji wengi walifanya hivyo zamani za kale (tazama utangulizi wa Vitabu vya Hekima uk. 470).
Kitabu hicho kinatufafanulia mazingira ya maisha ya Wayahudi wasiyoyaishi katika Palestina. Kinatuonesha kama Wayahudi hao waliokuwa mbali na hekalu la Yerusalemu walitimiza wajibu wao wa dini, yaani sala zao, ibada ya hadhara, kuishika Torati, uhusiano na Yerusalemu, matumaini ya kumpata Masihi. Maombolezo na kitabu cha Baruku vinabainisha kwamba Wayahudi wa baadaye walimheshimu sana nabii Yeremia.