E
Tangazo la mfalme Artashasta
12a Haya ndiyo maneno ya barua: 12b Mfalme mkuu Artashasta kwa watawala wa nchi katika majimbo mia moja ishirini na saba toka Bara Hindi hata Kushi, na kwa wale wanaoupenda ufalme wetu, salamu. 12c Kuna wengine ambao wanapozidi kutukuzwa kwa ukarimu wa wafadhili huzidi kutakabari, hata, licha ya kujaribu kuwadhuru raia zetu tu, huanza kufanya mashauri juu ya wafadhili wao wenyewe, kwa sabau hawawezi kuzistahimili fadhili hizo nyingi. 12d Si kama huondoa shukrani miongoni mwa watu tu, ila pia huinuliwa kwa maneno makuu ya wapumbavu na kutumaini kuepukana na hukumu ya Mungu ajuaye yote anayeupatiliza uovu. 12e Hata mara nyingi wenye mamlaka wamedanganywa na maneno laini ya rafiki waliokabidhiwa kazi za utawala, na hivyo wameishiriki damu ya wasio na hatia na kutiwa katika maafa yasiyo na dawa, 12f kwa sababu watu hawa wameishawishi mioyo myema ya bwana zao isiyofikiri mabaya kwa hila ya maelekeo ya mabovu. 12g Basi, hayo niliyoyasema mtaweza kuona, si sana kwa kuzichungua taarifa za zamani, bali hasa kwa kuchunguza mambo ya siku hizi yaliyotendeka juzi juzi tu kwa uovu wao wasiostahili mamlaka waliyopewa. 12h Yatupasa kuangalia sana siku hizi zijazo tuufanye ufalme wetu uwe na utulivu na amani kwa watu wote. 12i si kwa kuyasikiliza maneno ya watu, ila kwa kuamua kwa haki na uangalifu mambo yanayoletwa mbele yetu. 12j Maana Hamani Mwana wa Hamedatho, Mmakedonia ni mgeni kabisa hana damu yoyote ya Kiajemi, na yeye hana kabisa dalili ya shukrani kwa wema wetu, huyo alikaribishwa akae kwetu, 12k akashirikishwa ule upendeleo tunaowaonesha watu wa mataifa yote, hata akaitwa baba yetu. Naye alipewa heshima na wote kwa kuwa alikuwa mtu wa pili baada ya mfalme mwenyewe. 12l Lakini yeye, kwa kuwa hakuweza kukistahimili cheo chake kikuu, alifanya shauri atunyang'anye ufalme wetu na uzima wetu, 12m na kwa ujanja na udanganyifu mwingi alijaribu kumwua, si Mordekai tu, aliye mwokozi wetu na mfadhili wetu wa daima, ila na Esta pia, mshiriki wa ufalme wetu, asiye na hatia, pamoja na taifa lao lote. 12n Maana kwa hila hizo alidhani kutuacha upweke pasipo msaidizi, hata awape Wamakedonia ufalme wa Waameji. 12o Nasi tumeona ya kuwa Wayahudi, ambao huyu mtu wa shari nyingi amewatoa wauawe, sio watenda maovu hata kidogo, bali hujitawala kwa sheria ya haki kabisa; 12p nao ni wana wake aliye Juu, Mwenyezi, Mungu aliye hai, atengenezaye mambo ya ufalme kwa ajili yetu na kwa ajili ya baba zetu kwa utaratibu bora kabisa. 12q Basi, afadhali msiyatimize yale yaliyoandikwa katika barua mlizoletewa na Hamani mwana wa Hamedatho, kwa sababu aliyeyatenda hayo ametundikwa penye mlango wa Susa pamoja na wote wa nyumba yake; Mungu anayetawala yote amemlipa upesi stahili zake. 12r Itangazeni nakala ya barua hii kila mahali; waacheni Wayahudi wazifuate sheria zao wenyewe, kawapeni silaha ili siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, Adari, siku ile ile, wapate kujilinda nao watakaowashambulia katika shida yao. 12s Maana Mungu anayetawala yote ameifanya siku hiyo kuwa siku ya furaha wala si ya kufa kwa taifa teule, 12t nanyi, basi, katika sikukuu zenu za ukumbusho, mtaiadhimisha kwa furaha kama siku maalumu, ili sasa na sikuzote iwe siku ya wokovu kwetu na kwa Waajemi wenye nia njema, na ukumbusho wa maangamizo kwao wanaotuvizia. 12u Kwa hiyo mji wowote au nchi yoyote isiyoyafuata maagizo hayo itaharibiwa kabisa kwa upanga na kwa moto pasipo huruma, isipitiwe na mtu yeyote, bali ichukize daima hata kwa wanyama na ndege. 13Nakala ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao. 14Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Susa mjini.
15Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawati na nyeupe, mwenye taji kubwa la dhahabu, na joho la kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Susa wakapaza sauti, wakashangilia. 16Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. 17Na katika kila mkoa, na kila mji, popote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, maana waliwaogopa Wayahudi.