13
Tahadhari kuhusu Ushirikiano
1Mwenye kugusa lami atatiwa uchafu; naye mwenye kufuatana na mwenye kiburi atapata kufanana naye. 2Usijitwike mzigo upitao nguvu zako; wala usishirikiane na mtu aliye tajiri kuliko wewe. Jinsi gani chungu kushirikiana na birika? Hiyo itagonga na hicho kitavunjwa. 3Tajiri hudhulumu, akaogofya; maskini hudhulumiwa, akasihi. 4Iwapo una faida kwake, tajiri atachuma kwako; ukihitaji atakuacha. 5Kama una kitu, atakaa nawe; hata utakapofilisika, hajuti. 6Je! Ana haja nawe? Basi atakudanganya, na kukushawishi, na kukutia tumaini; atakupa maneno mazuri na kusema, Unahitaji nini? 7Naye atakutahayarisha kwa karamu zake; hata amekukumbia yote mara mbili tatu. Mwishowe atakufanyizia mzaha; atakuahirisha, na kukuacha, na kutikisa kichwa chake. 8Ujihadhari usije ukadanganyika na kufedheheshwa katika uchangamfu wako. 9Mkuu akikualika na uwe makini, hivyo atazidi kukualika. 10Usijitangulize kwake, usije ukakatazwa; wala usijitenge naye, usije ukasahauliwa. 11Usifanye kusema naye kama na mwenzako; wala usisadiki maneno yake mengi; yaani, kwa maongezi mengi atakujaribu, na kwa kukunjua uso atakupeleleza. 12Mtu asiyeficha moyoni mwake yaliyosemwa hana rehema; maana hatajizuia na kuhizi wala na kufunga; 13basi ujihadhari uwe macho, maadamu unakwenda katikati ya hatari ya kuanguka. 15Kila kiumbe hupenda kilichofanana nacho, na kila mwanadamu humpenda aliyefanana naye. 16Wanyama wote huandamana aina kwa aina; vile vile mwanadamu ataambatana na mmojawapo wa aina yake. 17Jinsi gani mbwamwitu ashirikiane na mwana-kondoo? Vivyo hivyo mwenye dhambi na mwenye haki. 18Kuna amamni gani kati ya fisi na mbwa? Tena amani gani kati ya tajiri na maskini? 19Punda mwitu ni mawindo ya simba nyikani; ndivyo maskini walivyo malisho ya tajiri. 20Unyonge ni chukizo kwa mwenye kiburi; na umaskini ni chukizo kwa tajiri. 21Tena tajiri akitikisika huegemezwa na rafiki zake; mnyonge akiisha kuanguka husukumizwa mbali na rafiki zake. 22Tajiri akianguka, wapo wasidizi wengi; hata akinena yasiyoneneka, watu humkiri kuwa ana haki; mnyonge huanguka, na watu humshutumu; hata akitoa maneno ya hekima hakuna ampishaye. 23Tajiri anena, na wote wanyamaza na yale ayanenayo huyasifu hata mawinguni; maskini anena, nao husema, Nani huyu? Na iwapo amejikwaa, kumbe! Watazidi kumwangusha. 24Lakini utajiri pasipo dhambi ni mwema; na umaskini ni mbaya ukitoka katika ubaya.
25Moyo wa mtu hufanya kubadili uso,
Kwamba ni kwa wema au kwa ubaya.
26Uso mkunjufu hufunua moyo ulio fani;
Na kubuni mifano ni kuchosha akili.