UTANGULIZI
Kitabu hiki kimeingia katika orodha ya vitabu rasmi vya tafsiri ya Kigiriki ya Biblia, lakini siyo katika Biblia ya Kiebrania. Wakristo wa zamani za kale wamekichukua kama kitabu rasmi kutokana na tafsiri ya Kigiriki (yaani Septuaginta). Waprotestanti wanakichukulia kama mojawapo wa vitabu vya Apokrifa.
Mtungaji
Katika utangulizi wa mfasiri mjukuu wa mtungaji wetu hueleza kwamba yeye ndiye aliyefasiri kitabu hiki muda alipoishi Misri, yaani mwaka wa 38 wa mfalme Evergete. Bila shaka huyo ni mfalme Tolemayo wa Saba Evergete. Kwa hiyo fasiri hiyo imefanywa mwaka 132 K.K. Basi Yoshua mwana wa Sira mwenyewe, yaani babu yake, aliishi na kuandika hicho kitabu karibu mwaka 190 K.K.
Mwaka 198 K.K. Palestina ikaanza kutawaliwa na Waseleusidi. Waisraeli wakawa makundi mawili. Kundi moja lilipendelea sana Ugiriki hata likapata uongozi. Punde kidogo Antioko Epifani (175-163 K.K.) akataka kwa nguvu kuingiza ustaarabu wa Kigiriki katika Palestina. Yoshua mwana wa Sira akatumia nguvu zote za mapokeo ya wazee kwa kuupinga uzushi mpya huo. Yeye ni mwandishi, naye huunganisha mapendo ya Hekima na mapendo ya Torati. Amejawa na upendeleo kwa hekalu na madhehebu yake; aliujali sana ukuhani. Alivijua pia vitabu vitakatifu vya Manabii na vya Hekima. Alitaka kujivisha Hekima kwa ajili ya watu waitafuatao (33:18; 50:27).
Mafundisho ya kitabu
Kitabu cha Yoshua mwana wa Sira chafanana sana na vitabu vya Hekima vilivyotangulia. Lakini kinaleta pia mafundisho mapya: kuhusu kipeo cha mwanadamu na suala kuhusu majazi ya mtu kadiri ya maisha yake, mtungaji ameingiwa na mashaka yale yale waliyoingiwa Ayubu na Mhubiri.
Ana imani katika majazi; anaona kwamba saa ya kufa ni muhimu sana lakini hajui bado jinsi gani Mungu atamjazia kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
Yoshua mwana wa Sira afundisha jambo jipya juu ya Hekima, maana huzifanya sawa Hekima na Torati iliyotangazwa na Musa (24:23-24). Vivi hivi utenzi wa Baruku husawazisha Hekima na Torati (Bar 3:9—4:4). Wenye Hekima waliomtangulia Yoshua mwana wa Sira hawakufanya hivyo. Maandishi ya Hekima na maandishi ya Torati yalikuwa mambo mbalimbali. Kwake yeye kushika Torati na hasa kufuata barabara sheria zote za ibada ya hadhara (25:1-10). Yeye ni mtu anayependa na kushikilia sana kawaida na sherehe za ibada. Aidha mwana wa Sira anajitofautisha na wazee wenye hekima wa zamani za kale katika kufikiri na kueleza historia takatifu ya taifa teule (44:1-49; 16 na maelezo 44:1).
Yoshua mwana wa Sira ni shahidi wa mwisho wa Hekima ya Wayahudi katika Palestina ambaye kitabu chake kimeingia katika orodha ya vitabu rasmi. Yeye ni mfano bora wa watu walioitwa zamani zile “Wahasidimu” maanake, watu wacha Mungu (1 Mak 2:24). “Wahasidimu”. Watashindania imani yao wakipambana na udhalimu wa Antioko Epifani. Jamii mbalimbali ndogo ndogo za “Wahasidimu” wameendelea kuwapo katika Israeli hata zama za Yesu Kristo. Katika jamii hiyo mbegu ya mafundisho ya Yesu Kristo itachipuka. Katika maandiko ya Agano Jipya, waraka wa Yakobo mtakatifu hukopa mara ningi semi za kitabu cha mwana wa Sira. Katika vitabu vyote vya Agano la Kale, isipokuwa Zaburi, Liturujia hutumia zaidi kitabu cha Yoshua mwana wa Sira.
Utangulizi wa msafiri
Torati, manabii, na Waandishi wengine waliowafuata wametupasha mafundisho makuu sana hata hatuwezi kumsifu Israeli asitahilivyo kwa ajili ya elimu na hekima yake. Tena, ni lazima ya mtu siyo tu kupata maarifa kwa kusoma, bali pia, akiisha funzwa, lazima awafunze wengine kwa maneno na maandishi yake. Basi hii ndiyo sababu kwamba Babu yangu Yoshua alisomelea kwa saburi Torati, Manabii, na vitabu vinginevyo vya Mababu. Ikawa hata yeye alipopata kuwa mtaalamu sana akaonelea aandike masomo ya mafundisho na hekima. Na kusudi lake ni kwamba watu ambao wanatamani mafunzo wajiweke pia chini ya maongozi haya, kisha wajifunze vema zaidi kuishi kadiri ya Torati.
Kwa hiyo nanyi mnaombwa kuyasoma kwa uangalifu na wema, mkivumilia kwa upole makosa ambayo huenda yametokea katika ufasaha fulani, ingawa tulifanya juhudi kupata ufasiri bora. Kusema kweli, habari asilia kama zilivyoandikwa kwanza katika Kiebrania hazilingani na jinsi zilivyofasiriwa katika lugha nyingine. Aidha, mtu akiichunguza Torati yenyewe, Manabii, na vitabu vinginevyo, ataona kuwa ufasiri wake ni tofauti sana na maneno yake asilia.
Ilikuwa mwaka 38 wa hayati Mfalme Evergete hata nilipofika Misri na kuishi huko. Ikawa wakati huo nikagundua kitabu cha maarifa bora. Basi nami vile vile nikajipa wajibu mkubwa kutumia bidii na nguvu zangu kufasiri kitabu hiki cha sasa. Nikafanya uangalifu sana na maarifa mengi wakati huu, ili kwamba kazi hii kubwa iwe kwa mafaa, na kwamba kipigwe chapa kitabu kwa matumizi ya wale walio ugenini pia ambao wanataka kufunzwa na kuratibu mienendo yao na kuishi kadiri ya Torati.