Hekima ya Sulemani UTANGULIZI
SRUVDC

Hekima ya Sulemani UTANGULIZI

UTANGULIZI
Katika sehemu ya kwanza ya kitabu cha Hekima ya Sulemani yasimuliwa madaraka ya Hekima katika kipeo cha mtu. Kinalinganisha baina ya wema na wabaya muda wanapoishi duniani na baada ya kufa (1—5). Sehemu ya pili inaeleza juu ya chanzo na tabia ya hekima na jinsi ya kuipata (6—9). Sehemu ya mwisho (10—19) inatukuza kazi ya hekima na ya Mungu katika historia ya taifa teule. Sehemu hii yakaza hasa tukio moja lililo kubwa kuliko yote katika historia hiyo, yaani uhuru wa kutoka Misri. UTANGULIZI mdogo wa sehemu hii ya tatu wasimulia mwanzo wa mtu toka Adamu mpaka Musa (10:1-14). Sura 13-15 zinakaripia vikali kuabudiwa kwa miungu wa uongo.
Mtungaji na tarehe ya kutungwa Kitabu
Kitabu hiki kimeingia katika orodha ya vitabu rasmi vya tafsiri ya Kigiriki ya Biblia, lakini siyo katika Biblia ya Kiebrania. Wakristo wa zamani za kale wamekichukua kama kitabu rasmi kutokana na tafsiri ya Kigiriki, yaani Septuaginta. Waprotestanti hawakukipokea katika orodha yao ya vitabu rasmi.
Sulemani alidhaniwa kuwa mtungaji wa kitabu hicho. Lakini mambo si hivyo. Mtungaji halisi alikiweka kitabu hicho chini ya ulinzi wa Sulemani, akamfanya ndiye mtungaji mwenyewe. Zamani hizo hii ilikuwa desturi ya watu wengi kufanya hivyo. Sulemani alitazamwa kama mwenye hekima kupita watu wa Israeli wote (tazama Mhubiri; Wimbo ulio Bora).
Kwa hakika mtungaji halisi ni Myahudi. Huyo amejawa na imani kwa “Mungu wa Mababu” (9:1). Anaona fahari kwa kuwa yu mmoja wa “watu watakatifu, wazao wasio na hatia” (10:15). Lakini yeye ni Myahudi aliyeingiwa na malezi na hali ya Kigiriki. Aliishi Iskanderia, mji Mkuu wa Misri. Iskanderia ulikuwa pia makao makuu ya malezi ya Kigiriki wakati wa nasaba ya wafalme Watolemayo. Pia Iskanderia ulikuwa mji mkuu wa Wayahudi walioishi ng'ambo ya nchi ya Palestina. Kwa sababu hii mtungaji huyo anaeleza sana matukio ya kutoka Misri, tofauti baina ya Wamisri na Waisraeli; kisha wanakaripia sana Wamisri kwa sababu waliabudu wanyama. Anatumia maneno ya Biblia ya Kigiriki (Septuaginta). Kwa hiyo inaonekana kwamba kitabu hicho kimeandikwa kwenye mwaka 50 K.K.
Kusudi la kitabu
Kitabu hicho kimeandikwa kwa ajili ya kuwaimarisha imani Wayahudi wenzake. Imani ya Wayahudi wa Iskanderia ilikuwa katika hatari ya kupotea kwa sababu ya fahari yao juu ya ustaarabu mkuu wa Iskanderia. Waliona fahari juu ya shule za elimu ya filosofia iliyo elimu kuu ya Wagiriki; walijivunia maendeleo ya maarifa. Walikwazwa na dini mbalimbali za kipagani za nyakati zile, walivutwa na wapiga falaki na waabudu Hermesi, mungu wa Kigiriki, na mengineyo. Katika kitabu yaonekana kuwa ameandika kwa ajili ya wapagani pia. Anataka kuwaongoza kwa Mungu ambaye huwapenda watu wote lakini hiyo si nia yake maalumu. Nia yake hasa ni kuwasaidia na kuwakinga wenzake, sio kuwaongoa wapagani.
Mafundisho ya kitabu
Mtungaji ni “Mtu mwenye hekima wa Israeli”. Kama walivyofanya wana-hekima wa zamani, naye pia huwahimiza watu watafute hekima inayotoka kwa Mungu. Hekima hiyo yapatikana kwa sala; tena hekima ni chemchemi ya fadhila, kisha hutuletea heri yote pia. Madhali alijifunza maarifa ya Iskanderia, mtungaji aunganisha hekima ya wazee na maarifa ya Iskanderia ya nyakati zake. Wazee wenye hekima walisumbuliwa sana na mawazo yao juu ya malipo ya kila mtu hapa duniani (tazama utangulizi uk. 601). Kitabu cha Hekima ya Sulemani huondoa mashaka juu ya swali hilo. Kutokana na malezi ya Kigiriki mtungaji amefahamu kwamba roho yaweza kujitenga na kuishi bila mwili (9:15), na kisha itaishi daima bila kufa. Anathibitisha ya kuwa “Mungu alimuumba mwanadamu apate kutoharibika” (2:23). Malipo ya hekima ni kutufanya kutoharibika na kutukaribisha kwa Mungu (6:18-19). Maisha ya hapa duniani ni matayarisho tu kwa maisha ya baadaye. Katika maisha ya baadaye watu wema wataishi pamoja na Mungu, wabaya watapata adhabu (3:9-10).
Kama vitabu vingine vya hekima kitabu hicho kinaeleza asili na tabia ya “Hekima” yenyewe. Katika kitabu hicho Hekima yenyewe inajionesha wazi zaidi kama nafsi kuliko katika vitabu vingine. Nafsi hiyo kwa upande mmoja ni tofauti na Mungu, kwa upande mwingine ina asili ya kimungu (tazama maelezo ya 7:22). Katika kusimulia habari za Israeli mtungaji anajishughulisha sana kueleza sababu gani Mungu hakuwaangamiza mara Wamisri na Wakanaani. Ilikuwa hasa saburi ya Mungu iliyowahurumia (11:15—21:27). Hivyo tunapata maelezo mengi katika kitabu hicho. Ni chakula bora cha roho kwa kila Mkristo. Kanisa huchota mara kwa mara masomo yake ya Liturujia katika kitabu hicho.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Learn More About Swahili Revised Union Version