2
1Basi, nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.#2:1 Ionekanavyo mahala pengine, hasa katika 2Kor 12:14, Paulo aliwatembelea Wakristo wa Korintho mara mbili. Yamkini ni wakati wa ziara hiyo ya pili Paulo alipohuzunishwa na mtu fulani naye Paulo akaitaka hiyo jumuiya kumchukulia hatua kali mtu huyo. 2Maana nikiwahuzunisha nyinyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! 3Ndiyo maana niliwaandikia: sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na nyinyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba mimi nikifurahi, nyinyi nyote pia mnafurahi.#2:3-4 Ling na 2Kor 7:8-12. Yahusu barua nyingine ambayo Paulo aliandika baada ya ile ya kwanza na kabla ya hii Barua ya pili kwa Wakorintho. 4Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwaonesheni kwamba nawapenda mno.
Msamaha
5Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi, ila amewahuzunisha nyinyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi. 6Adhabu#2:6 Adhabu: Paulo anasema juu ya adhabu ambayo yeye na Wakorintho waliijua; labda ilikuwa adhabu ya kutengwa na jumuiya ya waumini. Lakini Paulo anawataka Wakorintho wamsamehe mtu huyo na kumpa moyo (aya 7). aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha. 7Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa. 8Kwa hiyo nawasihi: mwonesheni kwamba mnampenda. 9Madhumuni yangu ya kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo. 10Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe, kama kweli ninacho cha kusamehe, nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.
Wasiwasi wa Paulo mjini Troa
12Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana. 13Lakini nilifadhaika#2:13 Nilifadhaika: Paulo alikuwa amemtuma Tito Korintho (labda pamoja na ile barua anayotaja katika 2:3-4) na yamkini alikuwa anatazamia kupata habari za Wakorintho na alikuwa na wasiwasi sana juu ya kukawia kwake Tito. sana kwa kutomkuta ndugu#2:13 Ndugu: Kama kawaida ni namna au neno la kumtaja Mkristo kwa vile Wakristo wote ni kama wa jamaa moja ya Mungu au ya Kristo. yetu Tito.#2:13 Tito: Alikuwa mwenzi wake Paulo katika kuhubiri Habari Njema. Huyu ndiye yule yule aliyeandikiwa barua ijulikanayo sasa kama “Barua kwa Tito”. Kama jina lake linavyoashiria, yeye hakuwa Myahudi. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia.
Ushindi kwa msaada wa Kristo#2:14-17 Katika sehemu hii Paulo anatumia mifano au picha ya mtu fulani kuelezea ukweli wa hali ya Kikristo: msafara wa ushindi - picha ya jeshi linalorudi kwa ushindi kutoka vitani; msafara ulipitia mijini kwa shangwe pamoja na nyara zao, nao watumwa walitangulia mbele ya msafara huo wakiwa na moshi wa ubani ambao kwa wale waliokuwa wamehukumiwa kuuawa hiyo ilikuwa harufu ya kifo kinachowangojea, bali kwa wengine hiyo ilikuwa harufu nzuri ya uhai. Kwa maneno hayo Paulo pia anagusia mafanikio yanayoendelea kupatikana katika shughuli za kusambaza Habari Njema au Injili. Ling Kol 2:15 na pia wazo la Mkristo kuwa kama mfungwa wa Kristo (Rom 6:22; 1Kor 7:22; Efe 6:6).
14Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo.#2:14 Shukrani kwa Mungu …ushindi wa Kristo: Tafsiri nyingine yamkini: “Shukrani kwa Mungu ambaye hutuwezesha kushinda kwa kuungana na Kristo”. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. 15Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote, wanaookolewa na wanaopotea. 16Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo? 17Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.