2 Wathesalonike 1
BHNTLK

2 Wathesalonike 1

1
1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.
2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.#1:2 Kama kawaida ya barua nyakati hizo, hii Barua kwa Wathesalonike inaanza kwa kumtambulisha mwandishi, na pia kwa namna inayofanana na 1Thes Silwano (Sila) na Timotheo wanatajwa. Taz 1Thes 1:1 maelezo.
Hukumu wakati wa kuja kwake Kristo#1:3-12 Katika sehemu hii Paulo anamshukuru Mungu kwa sababu ya kuongezeka na kuimarika kwa imani na upendo wa Wathesalonike licha ya mateso mengi yaliyowakabili (aya 3-4). Maneno haya ya shukrani ni machache kuliko ilivyo katika 1Thes (ling na 1Thes 1:1). Kutaja mateso hapa kunampa Paulo fursa ya kutaja katika sehemu hii juu ya kuja kwake Yesu Kristo mara ya pili, kuwatuza na kuwaadhibu waovu (aya ya 6-10).
3Ndugu, tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana. 4Ndio maana sisi tunajivunia nyinyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso#1:4 Udhalimu …na mateso: Rejea 1Thes 1:6; 2:14; 3:3 (ambapo panatajwa wazi lazima ya mateso). mnayopata.
5Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake, nyinyi mtastahili ufalme wake ambao kwa ajili yake mnateseka. 6Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa nyinyi 7na kuwapeni nafuu nyinyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake#1:7 Pamoja na malaika wake: Mat 25:31; Marko 8:38; taz 1Thes 3:11-13 maelezo. wenye nguvu 8na miali ya moto,#1:8 Miali ya moto: Katika A.K. picha au mfano wa moto ulitumiwa mara kwa mara kuandamana na kutokea au kuweko kwake Mungu (Kut 19:18; 24:17; Kumb 4:11-13; Eze 1:4; 8:2); katika mazingira mengine, picha ya moto inahusikana na hukumu, na hiyo ndiyo inayohusika hapa (aya 8-9). Rejea Isa 66:15; Mat 25:41; 1Kor 3:13-15. kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu. 9Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu, 10wakati atakapokuja siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Nyinyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.
11Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezesheni kustahili maisha aliyowaitia muyaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani. 12Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza