2 Wathesalonike 3
BHNTLK

2 Wathesalonike 3

3
Tuombeeni kwa Mungu#3:1-5 Katika 3:1-2, Paulo anawataka walengwa wake wamwombee na katika aya 3-4 (kama vile pia katika 2:16-17) Paulo anasema anayo matumaini makubwa kwamba Mungu atawaweka Wathesalonike salama na anaomba katika aya ya 5 kwamba itakuwa hivyo.
1Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu. 2Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanauamini ujumbe huu.
3Lakini Bwana ni mwaminifu.#3:3 Bwana ni mwaminifu: 1Kor 1:9; 1Thes 5:24. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.#3:3 Yule Mwovu: Hapa yahusu Shetani. Rejea 2Thes 2:9 ambapo Shetani anatajwa. 4Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni.
5Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.
Jukumu la kufanya kazi#3:6-15 Sehemu hii yahusu onyo kwa wale ambao walingojea kwamba Kristo angerudi upesi, wakaacha kufanya kazi na kwa kufanya hivyo wakawa mzigo kwa wengine.
6Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa. 7Nyinyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu; 8hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu. 9Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano. 10Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, “Mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula.”#3:10 Mtu yeyote asiyependa kufanya kazi, asile chakula: Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanafikiri huu ni msemo wa kawaida wa maisha. Lakini wengine wanaona ni rejeo kwa Mwa 3:19.
11Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine. 12Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe.
13Lakini nyinyi ndugu, msichoke kutenda mema. 14Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye, kusudi aone aibu. 15Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu.
Maneno ya mwisho
16Bwana mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.
17Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi:#3:17 Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Taz 1Kor 16:21 maelezo. Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika.
18Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.#3:18 Baadhi ya hati za kale zina “Amina” mwishoni mwa aya hii.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza