Amosi 1
BHNTLK

Amosi 1

1
Nabii Amosi
1Maneno ya Amosi, mmojawapo wa wachungaji wa mji wa Tekoa.#1:1 Tekoa: Mji huu ulikuwa mji katika eneo la milima la Yuda kusini mwa Yerusalemu (2Sam 14:1-4; 2Nya 11:5-6). Mungu alimfunulia Amosi mambo haya yote kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya lile tetemeko la ardhi,#1:1 Tetemeko la ardhi: Kuna kumbukumbu, kutokana na uvumbuzi wa mambo ya kale (Akiolojia) katika mji wa Hazori, kwamba kulitokea tetemeko la ardhi mwaka 760 K.K. na huenda ndilo linalohusika hapa. wakati Uzia alipokuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, alipokuwa mfalme wa Israeli.#1:1 Wakati Uzia …Yeroboamu … mfalme wa Israeli: Mfalme Uzia (2Fal 15:1-7; 2Nya 26:1-24; Isa 6:1) alitawala mwaka 781-740 K.K. katika utawala wa kusini wa Yuda, naye Yeroboamu II (2Fal 14:23-29) alitawala mwaka 783-743 katika utawala wa kaskazini Israeli. 2Amosi alisema hivi:
Mwenyezi-Mungu ananguruma kutoka mlima Siyoni,
anavumisha sauti yake kutoka Yerusalemu,
hata malisho ya wachungaji yanakauka,
nyasi mlimani Karmeli zinanyauka.#1:2 Aya hii hapa ni namna ya utangulizi ambao unatilia mkazo uwezo na nguvu kuu ya neno la Mungu. Mwenyezi-Mungu anapoongea, neno lake linatekelezwa kikamilifu na nguvu yake inaafiki na kudhihirika sio tu katika historia ya binadamu bali pia katika maumbile. Rejea Isa 55:10-11; Yer 1:12; Eze 12:25.
Hukumu ya Mungu kwa mataifa jirani ya Israeli
Damasko#1:3 Damasko: Mji mkuu wa Siria na ufalme wa Arami ambao ulikuwa adui wa jadi wa Israeli. Mwaka 732 K.K. Waashuru walivamia ufalme huo, wakawachukua uhamishoni wengi wa wakazi wake. Rejea 2Fal 16:9; Isa 7:8; 8:4; 17:1-3; Yer 49:23-27; Zek 9:1.
3Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Damasko wametenda dhambi tena na tena;#1:3 Tena na tena: Maneno yanayotafsiri kile ambacho katika Kiebrania neno kwa neno ni: “makosa matatu … makosa manne” mtindo wa kusema ambao una shabaha ya kusema uovu huo umefikia kilele chake na unatumika mwanzoni mwa kila sehemu ambayo ni kauli ya Mwenyezi-Mungu. Rejea Amo 1:6,9,11,13; 2:1,4,6.
kwa hiyo, sitaacha kuwaadhibu;
waliwatendea watu wa Gileadi ukatili mbaya.#1:3 Ukatili mbaya: Neno kwa neno “wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma”, bila shaka maneno yanayotumika kama mfano wa ukatili mbaya.
4Basi, nitaishushia moto#1:4 Moto: Matumizi ya moto mara nyingine huwa na maana yake halisi na mara nyingine maana ya mfano au ishara, kwa Amosi matumizi hayo yanaashiria hasira ya Mungu. Rejea Amo 1:4,7,10,12; 2:2,5; 5:6; 7:4. ikulu ya mfalme Hazaeli,
nao utaziteketeza kabisa ngome za mfalme Ben-hadadi.#1:4 Ben-hadadi: 2Fal 13:3.
5Nitayavunjavunja malango ya mji wa Damasko,
na kuwang'oa wakazi wa bonde la Aweni,#1:5 Bonde la Aweni: Maana yake “bonde la uovu”.
pamoja na mtawala wa Beth-edeni.#1:5 Beth-edeni: Maana yake “Nyumba ya anasa”. Amosi anabadili majina ya miji hiyo labda kuonesha kwamba hakubaliani na hali yao.
Watu wa Aramu watapelekwa uhamishoni Kiri.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Filistia
6Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Gaza wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Walichukua mateka watu kabila zima,
wakawauza wawe watumwa kwa Waedomu.#1:6 Wakawauza …watumwa kwa Waedomu: 2Nya 21:16-17; Yoe 3:4-8.
7Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Gaza,
nao utaziteketeza kabisa ngome zake.
8Nitawang'oa wakazi wa mji wa Ashdodi,
pamoja na mtawala wa Ashkeloni.
Nitanyosha mkono dhidi ya Ekroni,#1:7-8 Gaza …Ashdodi … Ashkeloni … Ekroni: Hii ilikuwa miji mitatu kati ya miji mitano ya Filistia; Isa 14:29-31; Yer 47; Eze 25:15-17; Sef 2:4-7; Zek 9:5-7.
nao Wafilisti wote waliosalia wataangamia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Tiro
9Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Tiro wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Walichukua mateka kabila zima hadi Edomu,
wakaukiuka mkataba wa urafiki waliokuwa wamefanya.
10Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Tiro,
na kuziteketeza kabisa ngome zake.”
Edomu
11Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Edomu wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Waliwawinda ndugu zao#1:11 Ndugu zao: Waisraeli walikuwa wazawa wa Yakobo, nduguye Esau, wazee wao Waedomu. Waisraeli kwa mapanga,
wakaitupilia mbali huruma yao yote ya kindugu.
Hasira yao haikuwa na kikomo,
waliiacha iwake daima.
12Basi, nitaushushia moto mji wa Temani,
na kuziteketeza kabisa ngome za Bosra.”#1:12 Temani …Bosra: Hii ilikuwa miji ambamo waliishi viongozi wa Edomu. Taz Yer 49:7 na 49:13 maelezo.
Amoni#1:13 Amoni: Kadiri ya Mwa 19:37-38, Waamoni na pia Wamoabu (2:1-3) walikuwa wazawa wa Loti ambaye alikuwa mpwa wake Abrahamu (taz Yer 49:1-6; Eze 21:28-32; 25:1-7; Sef 2:8-11).
13Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Amoni wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Katika vita vyao vya kupora nchi zaidi,
waliwatumbua wanawake waja wazito#1:13 Waliwatumbua wanawake waja wazito: Vitendo hivyo vya ukatili vinatajwa pia katika 1:3. nchini Gileadi.
14Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Raba,#1:14 Raba: Huu ulikuwa mji mkuu wa ufalme wa Waamoni, na ambao unaitwa pia Rabat-Amoni. Taz Yer 49:2.
na kuziteketeza kabisa ngome zake.
Siku hiyo ya vita patakuwa na makelele mengi,
nayo mapambano yatakuwa makali kama tufani.
15Mfalme wao na maofisa wake,
wote watakwenda kukaa uhamishoni.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza