2
Moabu#2:1 Moabu: Eneo lao lilikuwa upande wa mashariki mwa Bahari ya Chumvi na kaskazini ya Waedomu. Taz Yer 48:1 maelezo. Rejea pia Isa 15:1-16:14; 25:10-12; Yer 48; Eze 25:8-11; Sef 2:8-11.
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Moabu wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Wamemkosea heshima marehemu mfalme wa Edomu
kwa kuichoma moto mifupa yake
ili kujitengenezea chokaa!#2:1 Waisraeli wa kale walifikiri kuchoma maiti kama adhabu kali kupindukia kwa vile walidhani kwamba kuteketeza mabaki hayo ilizuia wahusika kwenda huko walikokwenda watu baada ya kifo. Rejea Mwa 38:24; Lawi 20:14; 21:9.
2Basi, nitaishushia moto nchi ya Moabu,
na kuziteketeza kabisa ngome za mji wa Keriothi.#2:2 Keriothi: Moja ya miji mikuu ya Moabu upande wa mashariki ya Bahari ya Chumvi. Rejea Yer 48:24.
Wanajeshi watakapopaza sauti zao na kupiga tarumbeta,
watu wa Moabu watakufa katika makelele hayo ya vita.
3Isitoshe, nitamuua mtawala wa Moabu,
pamoja na viongozi wote wa nchi hiyo.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yuda
4Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Yuda#2:4 Watu wa Yuda: Watu wa Yuda wanalaumiwa kwa vile hao walikuwa wamepewa maagizo na sheria ya Mwenyezi-Mungu lakini hawakuzifuata ila waliabudu miungu mingine. Katika lawama hizo kuna sauti za Kumbukumbu la Sheria na maandishi kama hayo (Yoshua; Waamuzi; 1 na 2 Samueli; 1 na 2 Wafalme) zinasikika. wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Wamepuuza sheria zangu,
wala hawakufuata amri zangu.
Wamepotoshwa na miungu#2:4 miungu: Kiebrania ni “uongo”, neno ambalo hutumika mara nyingi kutaja vinyago vya miungu. ileile waliyoihudumia wazee wao.
5Basi, nitaishushia moto nchi ya Yuda,
na kuziteketeza kabisa ngome za Yerusalemu.”
Hukumu ya Mungu juu ya Israeli
6 # 2:6 Sehemu hii yote (Amo 1:3—2:16) ina kiungo chake kikuu katika ujumbe huu dhidi ya Israeli. Hapa madhambi yao wenyewe kwa wenyewe na sio dhambi dhidi ya mataifa mengine kama walivyoshtakiwa mataifa ya jirani ila inahusu utovu wa uhusiano mwema kati ya watu wa Mungu, jambo ambalo linadhihirika aghalabu katika kuwakandamiza maskini, vitendo vya mahakimu kupuuza haki, na pia matendo ya kidini yaliyokatazwa (rejea aya ya 8). Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Waisraeli wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Wamewauza watu waaminifu
kwa kuwa hawakuweza kulipa madeni yao;
na kuwauza watu fukara
wasioweza kulipa deni la kandambili.#2:6 Kulipa deni la kandambili: Matajiri waliwauza maskini utumwani waliposhindwa kulipa hata madeni madogo sana. Kutaja kanda mbili hapa yaweza kukumbusha desturi ya kutupia sehemu ya ardhi kandambili kama ishara ya kuimiliki (Rut 4:7).
7Huwanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge,
na maskini huwabagua wasipate haki zao.
Mtu na baba yake hulala na mjakazi yuleyule,#2:7 Mtu na baba yake hulala na mjakazi yuleyule: Huenda hapa yahusu uasherati wa kidini (taz Kumb 23:17 na pia taz Hos 4:14 maelezo), au yahusu visa vya akina baba na wanawe wa kiume kukaa na suria yule yule.
hivyo hulitia unajisi jina langu takatifu.#2:7 Jina langu takatifu: Taz Zab 8:1.
8Popote penye madhabahu,
watu hulalia nguo walizotwaa kwa maskini
kama dhamana#2:8 Kuhusu kushika nguo zilizochukuliwa kama dhamana, rejea Kut 22:26-27; Kumb 24:10-13. ya madeni yao;
na katika nyumba ya Mungu wao
hunywa divai waliyotwaa kwa wadeni wao.
9“Hata hivyo, enyi watu wangu,
kwa ajili yenu, niliwaangamiza kabisa Waamori
ambao walikuwa wakubwa kama mierezi,
wenye nguvu kama miti ya mialoni.
Naam, niliwaangamiza, matawi na mizizi.
10Niliwatoeni kutoka nchi ya Misri,
nikawaongoza kupitia jangwani miaka arubaini,
mpaka mkaichukua nchi ya Waamori kuwa yenu.
11Niliwateua baadhi ya wana wenu wawe manabii,
na baadhi ya vijana wenu wawe wanadhiri.#2:11 Wanadhiri: Hao walionesha tegemeo lao kwa Mwenyezi-Mungu kwa kuahidi rasmi kutokula au kunywa vitu fulani fulani, na kuahidi kutokata nywele zao na kutogusa maiti. Rejea Hes 6:1-8.
Je, enyi Waisraeli,
haya nisemayo si ya kweli?
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
12Lakini nyinyi mliwafanya wanadhiri wanywe divai,
na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.
13“Sasa basi, nitawagandamiza mpaka chini,
kama gari lililojaa nafaka.
14Hata wapiga mbio hodari hawataweza kutoroka;
wenye nguvu wataishiwa nguvu zao,
na askari watashindwa kuyaokoa maisha yao.
15Wapiga upinde vitani hawatastahimili;
wapiga mbio hodari hawataweza kujiokoa,
wala wapandafarasi hawatayanusurisha maisha yao.
16Siku hiyo, hata askari hodari
watatimua mbio bila chochote.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”