5
Maombolezo ya Amosi
1Sikilizeni maombolezo#5:1 Ombolezo: Amosi anatumia hapa mtindo wa kishairi uliotumika katika kuomboleza kifo (rejea 2Sam 1:17-27; Yer 9:17-19). yangu juu yenu,
enyi Waisraeli:
2Umeanguka na hutainuka tena
ewe binti Israeli!#5:2 Binti Israeli: Israeli anatajwa hapa kama kijana bikira ambaye anakufa bila kupata kuonja muungano wa ndoa. Rejea Isa 47 ambapo kuna ombolezo juu ya kuanguka kwa Babuloni.
Umeachwa pweke nchini mwako,
hamna hata mtu wa kukuinua.
3Maana Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu 1,000 watatoka mjini kwenda kupigana
lakini watarejea 100 tu;
wataondoka watu 100 wa kijiji kimoja
lakini watanusurika watu kumi tu.”
4Mwenyezi-Mungu awaambia hivi Waisraeli:
“Nitafuteni mimi nanyi mtaishi!
5Lakini msinitafute huko Betheli
wala msiende Gilgali
wala msivuke kwenda Beer-sheba.
Maana wakazi wa Gilgali,
hakika watachukuliwa uhamishoni,#5:5 Wakazi wa Gilgali …watachukuliwa uhamishoni: Yaani Ashuru (taz Amo 3:11 maelezo).
na Betheli#5:5-7 Gilgali …Beer-sheba … Betheli: Miji hiyo inayotajwa hapa ilikuwa mahali pa ibada pa zamani sana, ambamo ibada kwa Mwenyezi-Mungu ilichanganyikana na ibada kwa miungu mingine. Taz Amo 3:14 maelezo; 4:4 maelezo. utaangamizwa!”
6Mtafuteni Mwenyezi-Mungu, nanyi mtaishi!
La sivyo, atawalipukia wazawa wa Yosefu#5:6 Wazawa wa Yosefu: Yosefu alikuwa mmoja wa watoto kumi na wawili wa Yakobo. Makabila mawili ya Waisraeli yalipewa majina ya watoto wa Yosefu: Efraimu na Manase (Mwa 48). Wakati wa Amosi Efraimu lilikuwa kabila lenye nguvu zaidi katika ufalme wa kaskazini na hivyo wazawa wa Yosefu hapa ni sawa na watu wa “Israeli”. kama moto;
moto utawateketeza wakazi wa Betheli
na hakuna mtu atakayeweza kuuzima.
7Tahadhari enyi mnaogeuza haki kuwa uchungu,
na kuuona uadilifu kuwa kama takataka!
8Huyo aliyezifanya Kilimia na sayari Orioni,#5:8 Aliyezifanya Kilimia na sayari Orioni: Kama Muumba wa nyota ambazo zilifikiriwa kuongoza nyakati na majira, Mwenyezi-Mungu anakuwa ndiye mwenye kuzithibiti na kuzimiliki. Vile vile nyota ni viumbe na haziwezi kuabudiwa kama walivyofanya watu wengine wa kale. Taz pia Yobu 9:8-9; 38:31.
ambaye huligeuza giza nene kuwa mchana,
na mchana kuwa usiku;
yeye ambaye ayaitaye pamoja maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya nchi kavu,
Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake.
9Yeye ndiye anayewaangamiza wenye nguvu,
na kuziharibu ngome zao.
10Nyinyi huwachukia watetezi wa haki
na wenye kusema ukweli mahakamani.
11Nyinyi mnawakandamiza fukara
na kuwatoza kodi ya ngano kupita kiasi.
Mnajijengea nyumba za mawe ya kuchonga,
lakini nyinyi hamtaishi humo;
mnalima bustani nzuri za mizabibu,
lakini hamtakunywa divai yake.
12Maana mimi najua wingi wa makosa yenu
na ukubwa wa dhambi zenu;
nyinyi mnawatesa watu wema,
mnapokea rushwa
na kuzuia fukara wasipate haki#5:10-12 Ninyi huwachukia watetezi wa haki …na kuzuia fukara wasipate haki: Amosi anaonesha tena jinsi Waisraeli wenye nguvu walivyozuia wanyonge kupata haki zao. Taz pia 2:6-7; 3:2; na 3:14-15. mahakamani.
13Basi, kutakuwa na wakati mbaya
ambao hata mwenye busara atanyamaza.
14Tafuteni kutenda mema na si mabaya,
ili nyinyi mpate kuishi
naye Mwenyezi-Mungu wa majeshi
awe pamoja nanyi kama mnavyosema.
15Chukieni uovu, pendeni wema,
na kudumisha haki mahakamani.
Yamkini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawafadhili watu wa Yosefu waliobaki.#5:15 Watu wa Yosefu waliobaki: Kuhusu “watu wa Yosefu” taz 5:6 maelezo. Na neno “waliobaki” kuashiria uhamisho wa wengi kutoka ufalme wa kaskazini hadi Ashuru mnao mwaka 722 K.K.
16Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi,
naam, Mwenyezi-Mungu asema:
“Patakuwa na kilio kila mahali mitaani;
watu wataomboleza: ‘Ole! Ole!’
Wakulima wataitwa waje kuomboleza,
na mabingwa wa kuomboleza#5:16 Mabingwa wa kuomboleza: Rejea Yer 9:17-22; taz pia Mat 9:23 maelezo. waje kufanya matanga.
17Patakuwa na kilio katika mashamba yote ya mizabibu;#5:17 Mashamba …mizabibu: Kwa kawaida wakati watu walipomaliza kuvuna mizabibu kulikuwa na sherehe kubwa lakini hukumu ya Mungu itafanya mashamba ya mizabibu kuwa mahali pa uchungu.
maana nitapita kati yenu kuwaadhibu.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.”
Siku ya Mwenyezi-Mungu
18Ole wenu nyinyi mnaoingojea kwa hamu
siku ya Mwenyezi-Mungu!#5:18-20 Siku ya Mwenyezi-Mungu: Amosi ni wa kwanza kusema juu ya siku ya pekee baadaye ambapo Mwenyezi-Mungu atakuja kuhukumu. Wengi zaidi walifikiri siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu ingekuwa siku ya ushindi na ukombozi kwa Israeli lakini ukweli ni kwamba ingekuwa siku ya maangamizi kwa sababu ya dhambi (taz Amo 3:2 maelezo). Kuhusu wazo hili kubwa taz Isa 2:12-22; 13:6-10; Yer 46:10; Eze 7:19; Yoe 1:15-20; 2:1-11; Zek 14:1; Mal 4:5.
Kwa nini mnaitaka sana siku hiyo?
Siku hiyo, itakuwa siku ya giza na sio ya mwanga!
19Mambo yatakuwa kama mtu aliyekimbia simba,
halafu akakumbana na dubu!
Au kama mtu anayerudi nyumbani kwake,
akatia mkono ukutani, akaumwa na nyoka.
20Siku ya Mwenyezi-Mungu itakuwa giza, na sio mwanga;
itakuwa huzuni bila uangavu wowote.
21Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nazichukia na kuzidharau sikukuu zenu;
siifurahii mikutano yenu ya kidini.
22Mjaponitolea sadaka zenu za kuteketezwa na za nafaka,
mimi sitakubali kuzipokea;
na sadaka zenu za amani za wanyama wanono
mimi sitaziangalia kabisa.
23Ondoeni mbele yangu kelele za nyimbo zenu!
Sitaki kusikiliza muziki wa vinubi vyenu!
24Lakini acheni haki itiririke kama maji,
uadilifu uwe kama mto usiokauka.#5:21-24 Nazichukia …sikukuu zenu … uadilifu uwe kama mto usiokauka: Ibada kwa Mungu zilikuwa hazina maana kama watu hawakuishi kwa uadilifu, yaani kuishi vema na kuwatendea wengine kwa haki.
25“Enyi Waisraeli, wakati ule mlipokuwa kule jangwani kwa miaka arubaini, je, mliniletea tambiko na sadaka hata mara moja? 26Je, wakati huo mlibeba kama sasa vinyago vya mungu wenu Sakuthi mfalme wenu na vinyago vya Kaiwani#5:26 Sakuthi …Kaiwani: Majina haya yanatajwa pia katika maandishi ya Babuloni nayo yahusu miungu ambayo ilihusishwa na Sayari iitwayo Saturno. mungu wenu wa nyota, vitu ambavyo mlijitengenezea wenyewe? 27Kwa hiyo nitawapeleka uhamishoni, mbali kuliko Damasko!”#5:27 Mbali kuliko Damasko: Labda dokezo kwa tukio la mwaka 722 K.K. ambapo watu wa Israeli kwa wingi walipelekwa uhamishoni (2Fal 17:3-6,18). Rejea Amo 5:5; 6:7; 7:11,17. Hayo amesema Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mungu wa Majeshi.