Amosi 6
BHNTLK

Amosi 6

6
Adhabu kwa sababu ya kujiamini
1Ole wenu nyinyi mnaostarehe huko Siyoni,
nanyi mnaojiona salama mlimani Samaria!
Nyinyi mwaonekana kuwa viongozi wa taifa maarufu
ambao Waisraeli wote huwategemea.
2Haya! Nendeni Kalne mkaangalie#6:2 Nendeni Kalne mkaangalie: Aya hii inaweza kueleweka kama onyo la Amosi kwa viongozi wa Israeli, au kama maneno ya kujivuna ambayo Amosi anawawekea mdomoni mwao. “Kalne” na “Hamathi” ilikuwa miji maarufu ya Siria (Isa 10:9). kila mahali,
tokeni huko mwende hadi mji ule mkubwa wa Hamathi,
kisha teremkeni hadi Gathi kwa Wafilisti.
Je, falme zao si bora kuliko zenu
na eneo lao si bora kuliko lenu?”
3Nyinyi mnajaribu kuifukuza siku mbaya.
Lakini mnauleta karibu utawala dhalimu.
4Ole wenu mnaolala juu ya vitanda vya pembe za ndovu
na kujinyosha juu ya masofa,
mkila nyama za wanakondoo na ndama!
5Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi
na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi.#6:5 Mfalme Daudi alitunga nyimbo (1Fal 16:17-23; 2Sam 1:17-27).
6Mnakunywa divai kwa mabakuli,
na kujipaka marashi mazuri mno.
Lakini hamhuzuniki hata kidogo
juu ya kuangamia kwa wazawa wa Yosefu.#6:6 Wazawa wa Yosefu: Yaani watu wa Israeli, ufalme wa kaskazini (taz 5:6 maelezo).
7Kwa hiyo mtakuwa wa kwanza kwenda uhamishoni,#6:7 Uhamishoni: Taz Amo 5:27.
na karamu za wenye kustarehe zitatoweka.
8Bwana Mwenyezi-Mungu ameapa kwa nafsi yake;
Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi asema:
“Nachukizwa mno na kiburi cha wazawa wa Yakobo;
tena nayachukia majumba yao ya fahari.
Mji wao na vyote vilivyomo nitawapa adui zao.”
9Kama wakibaki watu kumi katika nyumba moja, wote watakufa. 10Na atakapokuja mjomba wa aliyekufa kuitoa maiti nje aichome, akamwuliza yeyote atakayekuwako ndani pembeni mwa nyumba, “Je kuna mtu mwingine pamoja nawe?” Naye atamjibu, “La! Hamna!” Naye atamwambia, “Nyamaza kimya! Tusilitaje hata jina la Mwenyezi-Mungu.”#6:10 Maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri. Lakini inaonekana kwamba wazo la kutokumtaja Mwenyezi-Mungu katika mazingira hayo ni kutaka kuepa madhara zaidi.
11Tazama! Mwenyezi-Mungu anatoa amri,
nalo jumba kubwa labomoka vipandevipande,
na nyumba ndogo kusagikasagika.
12Je, farasi waweza kupiga mbio miambani?
Je, watu huilima bahari kwa ng'ombe?
Lakini nyinyi mmeigeuza haki kuwa sumu,
na tunda la uadilifu kuwa uchungu.#6:12 Zingatia muundo wa aya: Mistari miwili ya kwanza ni maswali ambayo hayahitaji majibu ila yanataja jambo ambalo ni dhahiri lisilowezekana; kisha katika mistari miwili ya mwisho nabii anataka kusema kwamba hayo ambayo hayawezekani ndio wanayofanya Waisraeli: kuvunja haki na mambo ya uadilifu.
13Nyinyi mnashangilia juu ya Lodebari,#6:13 Lodebari: Matumizi ya jina hili katika Kiebrania ni kama neno lenye maana “kitu batili” au “upuuzi.”
na kusema mmeuteka Karnaimu#6:13 Karnaimu: Maana ya jina la mji huu mdogo ni “pembe” nazo ni alama ya nguvu. kwa nguvu zenu wenyewe.
14Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Enyi Waisraeli,
kweli nitaleta taifa moja lije kuwashambulia,
nalo litawatesa nyinyi kuanzia Lebo-hamathi kaskazini,
hadi kijito cha Araba, upande wa kusini.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza