8
Maono ya nne: Kikapu cha matunda
1Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Niliona kikapu kilichojaa matunda ya kiangazi. 2Naye Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nami nikamjibu, “Naona kikapu cha matunda ya kiangazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia:
“Mwisho umewafikia watu wangu wa Israeli.
Sitavumilia tena maovu yao.#8:2 Maneno “matunda ya kiangazi” na neno “mwisho” katika Kiebrania yanakaribiana sana kimatamshi.
3Siku hiyo, nyimbo za ikulu zitakuwa maombolezo.
Kutakuwa na maiti nyingi,
nazo zitatupwa nje kimyakimya.”#8:3 Nje kimyakimya: Au: “… nje. Kimya!”
Mungu ataiadhibu Israeli
4Sikilizeni enyi mnaowakandamiza wanyonge
na kuwaletea maangamizi fukara wa nchi.
5Mnajisemea mioyoni mwenu:
“Sikukuu ya mwezi mwandamo#8:5 Sikukuu ya mwezi mwandamo: Siku ya kwanza ya mwezi mpya ilikuwa sikukuu ya kidini ambamo biashara yote na kazi ziliachwa. Taz Zab 81:3 maelezo. Rejea pia Hes 28:11-15; 1Sam 20:5; 2Fal 4:23. itakwisha lini
ili tuanze tena kuuza nafaka yetu?
Siku ya Sabato itakwisha lini
ili tupate kuuza ngano yetu?
Tutatumia vipimo hafifu vya wastani na uzito,
tutadanganya watu kwa mizani isizo sawa,#8:5 Mizani isizo sawa: Lawi 19:35-36; Kumb 25:13-16; Meth 11:1; Mika 6:10-11.
6hata kuuza ngano hafifu kwa bei kubwa.
Tutaweza kununua watu fukara kwa fedha,
na wahitaji kwa jozi ya kandambili.”#8:6 Kwa jozi ya kandambili: Taz Amo 2:6 maelezo.
7Mwenyezi-Mungu, fahari ya Yakobo,#8:7 Fahari ya Yakobo: Maneno haya yanatumika karibu kama jina la sifa la Mungu; yanahusu Mwenyezi-Mungu mwenyewe. Taz Amo 7:2. ameapa:
“Hakika, sitayasahau matendo yao maovu.
8Kwa hiyo, dunia itatetemeka#8:8 Dunia itatetemeka: Nabii Amosi anataja tetemeko la ardhi mara kwa mara (1:1; 2:13 3:14-15; 9:1).
na kila mtu nchini ataomboleza.
Nchi yote itayumbayumba;
itapanda na kushuka,
kama yanavyojaa na kupwa maji ya mto Nili!”
9Bwana Mwenyezi-Mungu asema,
“Siku hiyo#8:9 Siku hiyo: Yaani siku ile ya Mwenyezi-Mungu ambayo atahukumu. nitalifanya jua litue adhuhuri,#8:9 Nitalifanya jua litue adhuhuri: Tukio kama la kupatwa jua. Kumbukumbu za Ashuru zinataja kupatwa kwa jua ambako kulionekana katika Mashariki ya Kati mnamo mwezi Juni mwaka 763 K.K. Matukio kama hayo yalichukuliwa kuwa ni dalili ya hukumu ya Mungu (Yoe 2:10).
na kuijaza nchi giza mchana.
10Sherehe zenu nitazigeuza kuwa kilio,
na nyimbo zenu za furaha kuwa maombolezo.
Nitawafanya nyote mvae magunia kwa huzuni
na kunyoa vipara vichwa vyenu,
kama kuomboleza kifo cha mtoto wa pekee;
na siku ya mwisho itakuwa ya uchungu mkubwa.”
11Bwana Mwenyezi-Mungu asema,
“Siku zaja ambapo nitaleta njaa nchini.
Lakini sio njaa na kiu ya chakula na maji,
bali njaa ya kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu.
12Watu watatangatanga kutoka bahari hata bahari,
kutoka upande wa kaskazini mpaka mashariki.
Watakimbia huko na huko wakitafuta neno la Mwenyezi-Mungu,
lakini hawatalipata.
13“Siku hiyo, hata vijana wenye afya,
wa kiume kwa wa kike,
watazimia kwa kiu.
14Wale wanaoapa kwa mungu wa uongo wa Samaria,#8:14 Wanaoapa kwa mungu wa uongo wa Samaria: “mungu wa uongo” hapa Kiebrania ni “Ashima” jina ambalo wafafanuzi wanafikiri yahusu namna ya mungu kwa mfano wa ng'ombe dume. Watu walizoea kuapa kwa miungu katika mahali pa ibada mjini Dani (taz 7:9 maelezo) na katika mahali pa ibada mjini Beer-sheba (taz 5:5).
na kusema: ‘Kwa nafsi ya mungu wako ee Dani’;
na, ‘Kwa nafsi ya mungu wa Beer-sheba’,
wote wataanguka na hawatainuka tena kamwe.”