Baruku 3
BHNTLK

Baruku 3

3
1“Ee Bwana, Mungu Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli, tunakulilia wewe kwa moyo uliotaabika na hoi. 2Usikilize ee Bwana, na utuhurumie, maana sisi tumetenda dhambi mbele yako. 3Wewe wadumu milele, lakini sisi, tumeangamia milele! 4Ee Bwana, Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli! Usikilize sasa sala ya Waisraeli walio kama wafu,#3:4 Walio kama wafu: Kulingana na 2:17-18, maneno haya yahusu wale ambao wako karibu kufa (rejea aya ya 3). sala ya hao waliokukosea, waliokataa kutii sauti yako wewe Bwana Mungu wao, hata balaa zikatuandama. 5Usikumbuke maovu ya wazee wetu, bali ukumbuke uwezo wako na jina lako. 6Wewe ni Bwana Mungu wetu, nawe ndiwe tutakayekusifu peke yako. 7Wewe umeweka mioyoni hali ya uchaji wako ili tupate kukuomba kwa jina lako. Sisi tutakusifu huku uhamishoni tuliko, maana tumeweka mbali nasi uovu wote wa wazee wetu waliokukosea. 8Tazama, sisi sasa tumo uhamishoni ambamo wewe umetutawanya, tudharauliwe, tulaaniwe na kuadhibiwa kwa sababu ya maovu yote ya wazee wetu ambao walikuacha wewe Bwana Mungu wetu.”
Hekima#3:9—4:4 Hekima: Sehemu hii ni mafundisho katika muundo wa kishairi kuhusu hekima. Mwandishi anawalenga Waisraeli waliopelekwa uhamishoni na kudhihirisha kwamba balaa wazizopata wamestahili kwa kumwacha Mungu na kukosa hekima. Utenzi huu, ingawa unatumia lugha ya maandishi yaliyotangulia kama vile Meth 8:22-31; Yobu 28:12-28, unaieleza hekima kama chemchemi ya uhai na kutamka dhahiri kwamba hekima ni ya Mungu peke yake na kwamba ameiwasilisha kwa Waisraeli katika muundo wa sheria. mwongozo wa Israeli
9Sikiliza amri za uhai, ewe Israeli!
tega sikio, ukajifunze hekima!
10Imekuwaje, ee Israeli,
imekuwaje uko nchini mwa maadui zako;
kwamba umezeeka katika nchi ya kigeni
na kutiwa unajisi kwa maiti?
11Imekuwaje umehesabiwa pamoja na walio kuzimu?
12Wewe umeiacha chemchemi ya Hekima.
13Kama ungalifuata njia ya Mungu
ungalikuwa unaishi kwa amani milele.
14Jifunze palipo na Hekima,
mahali penye nguvu,
mahali penye maarifa, upate kugundua penye maisha marefu na uhai,#3:14 Jifunze …upate kugundua penye maisha marefu na uhai: Meth 3:16.
penye mwanga wa kuangazia macho na penye amani.
15Nani amewahi kugundua alipo Hekima,
Nani aliyefaulu kuingia katika ghala zake?
16Wako wapi watawala wa mataifa,
wale watawalao wanyama duniani kwa mabavu?
17Wako wapi wale wachezao na ndege wa angani,
wenye kurundika fedha na dhahabu
ambazo watu huzitegemea,
hata hawatosheki kuzitafuta?
18Wapi waliopanga na kuhangaika kupata fedha tu
na ambao kazi zao hazikuacha alama yoyote?
19Wote hao watoweka na kuishia chini kuzimu,
na wengine wamezuka mahali pao.
20Kizazi kipya kimeikalia nchi,
nacho pia kikauona mwanga wa mchana,
lakini hakikujifunza njia ya maarifa
wala hakikuzijua njia zake, wala hakikufaulu kumpata Hekima.
21Wazawa wake walipotoka njiani mwa Hekima.
22Hekima hajapata kusikika Kanaani,
wala kuonekana katika Temani.
23Wazawa wa Hagari watafutao maarifa duniani,
wafanyabiashara wa Merani#3:23 Wafanyabiashara wa Merani: Tafsiri yamkini ya makala ngumu; Wengine wanafikiri hapa yahusu Midiani. na Temani,#3:23 Temani: Majina yote mawili yahusu watu wa kale wa Mashariki ya Kati waliosifika kwa hekima yao. Lakini mwandishi hapa anasema kwamba hekima ya kweli haipatikani kwao.
wasimulizi wa visa na wenye kutafuta maarifa,
hawajajifunza njia ya Hekima,
hawajui chochote juu ya njia zake.
24Ee Israeli, jinsi gani ilivyo kubwa nyumba ya Mungu!#3:24 Nyumba ya Mungu: Hapa yamkini yahusu makao ya Mungu mbinguni.
Na jinsi gani ilivyo kubwa nchi anayomiliki!
25Ni kubwa na haina mipaka,
haina kimo na haipimiki.
26Majitu#3:26 Majitu: Rejea Mwa 6:1-4 ambapo yaonekana kwamba wazo hili limetolewa huko ambako majitu yalitokea kutokana na muungano kati ya malaika na wanawake wa watu (rejea pia Kumb 2:10; Hek 14:6 na taz Mwa 6:2 maelezo). maarufu ya kale yalizaliwa humo;
watu wakubwa kwa kimo na stadi vitani.
27Mungu hakuwateua hao
wala kuwajulisha njia ya maarifa.
28Hivyo waliangamia kwa kutokuwa na hekima;
waliangamia kwa upumbavu wao wenyewe.
29Nani aliyepanda mbinguni akamchukua Hekima,
akamleta chini kutoka mawinguni?
30Nani aliyewahi kusafiri baharini na kumpata?
Nani awezaye kumnunua kwa dhahabu?
31Hakuna mtu ajuaye njia ya kwenda kwake,
wala anayejali njia iendayo kwake.
32Lakini yeye ajuaye kila kitu anamjua Hekima,
alimpata kutokana na maarifa yake.
Yeye aliyeitayarisha dunia tangu milele
aliijaza viumbe vyenye miguu minne.
33Yeye huutuma mwanga nao huenda;
aliuita nao ukamtii kwa hofu.
34Nyota huangaza mahali pao kwa furaha,
yeye huziita nazo husema, “Tupo hapa”.
Huangaza kwa furaha kwa ajili yake yeye aliyeziumba.
35Huyu ni Mungu wetu,
hakuna awezaye kulinganishwa naye.
36Mungu aliigundua njia yote ya maarifa
akampatia Yakobo mtumishi wake,
naam, akampatia Israeli aliyempenda.
37Baadaye Hekima alitokea duniani
akaishi pamoja na binadamu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza