4
1Hekima ni kitabu cha amri za Mungu,
yeye ni sheria idumuyo milele.#4:1 Yeye ni sheria idumuyo milele: Tangu mwanzo wa historia ya Israeli, hekima ilichukua nafasi ya pekee katika utendaji wa kazi (taz hasa 1Fal 3:10,12,28); baadaye pia ilichukuliwa kuwa sawa na sheria (rejea pia Kumb 4:6; Zab 119:98). Agano Jipya linaiona hekima kuwa sawa na ujumbe wa Injili (rejea 1Kor 2:6-7; Efe 3:10) au kuwa sawa na Yesu Kristo mwenyewe (1Kor 1:24,30; taz pia Yoh 1:1 maelezo).
Wanaomshikilia Hekima wataishi,
lakini watakaomwacha watakufa.#4:1 Wanaomshikilia Hekima wataishi …watakaomwacha watakufa: Rejea Kumb 4:1; 30:15-20; Meth 8:35-36.
2Geuka, ewe Yakobo, umchukue Hekima;
tembea kuelekea mng'ao wa mwanga wake.
3Usimpe mtu mwingine fahari yako;
usiwape mataifa ya kigeni mapato yako.
4Heri yetu sisi, ee Israeli,
kwa maana tumejulishwa yampendezayo Mungu.#4:4 Heri yetu …tumejulishwa yampendezayo Mungu: Tafsiri nyingine yamkini “Heri yetu … tumejulishwa matakwa ya Mungu (Rom 2:18)”.
Ombolezo na matumaini ya Yerusalemu#4:5—5:9 Sehemu hii imeangaziwa na sehemu nyingine za Biblia kama vile Kumb 32; Isa 40—55; 60—62. Mwandishi anawakumbusha Waisraeli kwamba hali yao mbaya inatokana na kumsahau Mungu (4:6-29); hata hivyo anawakumbusha pia ahadi za Mungu za kuwaokoa (4:30—5:9).
5Jipeni moyo enyi watu wangu;
watu mnaolidumisha jina la Israeli.
6Nyinyi hamkuuzwa kwa watu wa mataifa muangamie,
bali mlitiwa mikononi mwa maadui zenu
kwa sababu mlimkasirisha Mungu.
7Mlimchokoza yeye aliyewaumba nyinyi,
kwa kutoa tambiko kwa pepo badala ya Mungu,
8Mlimsahau Mungu wa milele#4:8 Mungu wa milele: Jina “Mungu wa milele” ambalo lilitumiwa katika Mwa 21:33 na Isa 40:28 linatumiwa mara nyingi zaidi katika Biblia ya Kigiriki, na mara kwa mara katika kifupi kama “yeye aliye milele”, yaani: Mungu wa milele (taz Bar 4:10,14,20,22,24,35; 5:2; rejea pia 2Mak 1:25; Dan 13:42 (Kigiriki) na Rom 16:26). aliyewalea
mkauhuzunisha mji wa Yerusalemu uliowatunzeni.
9Mji huo uliiona ghadhabu iliyokujia kutoka kwa Mungu,
ukasema: “Sikilizeni enyi jirani za Siyoni.
Mungu ameniletea huzuni kubwa,#4:9 Mwandishi anasema hapa (aya ya 9-29) juu ya mji wa Yerusalemu kana kwamba ni nafsi au mtu ambaye ni mama mjane anayeomboleza kwa majirani kuhusu kupokonywa watoto wake.
10kwa maana nimeuona uhamisho wa watoto wangu,
ambao Mungu wa milele amewaletea.
11Mimi niliwalea kwa furaha,
lakini nikawaacha waende kwa machozi na huzuni.
12Mtu na asifurahie mkasa wangu mimi mjane,
mimi niliyefiwa na watoto wengi.
Niliachwa mkiwa kwa sababu ya dhambi za wanangu,
kwa sababu waligeuka wakaiacha sheria ya Mungu.
13Hawakuzijali kanuni zake,
hawakufuata njia za amri za Mungu,
wala kupita katika njia ya uadilifu uliowaonesha.
14“Enyi jirani zake Siyoni, njoni.
Kumbukeni uhamisho wa wanangu, wa kiume na wa kike,
uhamisho aliowaletea Mungu wa milele.
15Maana alileta dhidi yao taifa la mbali,
taifa la watu katili na wa lugha ngeni,
wasio na heshima kwa wazee
wala huruma kwa watoto.
16Waliwachukua mbali wavulana wapenzi wa mjane,
wakaniacha pweke nimefiwa na binti zangu.
17Lakini mimi nawezaje kuwasaidieni?
18Ni yule tu aliyewaleteeni balaa hilo
ndiye awezaye kuwaokoeni mikononi mwa maadui zenu.
19Nendeni, watoto wangu, nendeni tu!
Mimi nimeachwa mpweke.
20Nimevua vazi la amani,
nimevaa vazi la gunia la kuomba.
Nitamlilia Mungu wa milele siku zangu zote.
21Jipeni moyo enyi watoto wangu! Mlilieni Mungu
naye atawaokoeni makuchani mwa maadui.
22Maana namtumainia Mungu wa milele awaokoeni.
na furaha imenijia kutoka kwake huyo Mtakatifu,
kwa sababu ya huruma itakayowajia karibuni,
kutoka kwa Mwokozi wenu, Mungu wa milele.
23Kwa huzuni na machozi niliwaacheni mwende,
lakini Mungu atawarejesha kwangu kwa shangwe na furaha ya milele.#4:23 Lakini Mungu atawarejesha …na furaha ya milele: Kama vile katika Isa 40—66 kurejeshwa kwa watu kunaelezwa kwa maneno yasiyo na kikomo.
24Kama jirani za Siyoni walishuhudia kutekwa kwenu,
sasa wataona mkipata wokovu kutoka kwa Mungu,
wokovu utakaowajieni kwa utukufu mkubwa,
kwa fahari ya Mungu wa milele.
25Wanangu, vumilieni ghadhabu hiyo iliyowajieni kutoka kwa Mungu.
Maadui zenu wamewatesa,
lakini mtashuhudia karibuni kuangamizwa kwao,
nanyi mtakanyaga shingo zao kwa miguu yenu.
26Wanangu wapendwa, mmetembea katika njia za taabu;
mlichukuliwa kama kundi la kondoo lililochukuliwa na maadui wakali.
27Jipeni moyo, wanangu, na kumlilia Mungu,
kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni.
28Kama vile mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu,
vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu mara kumi zaidi.
29Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa hizi
atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele.”
30“Jipe moyo, ee Yerusalemu.
Mungu aliyekupa jina lako#4:30 Jipe moyo …Mungu aliyekupa jina lako: Bar 5:4. Tafsiri nyingine “aliyekuita kwa jina lako”. atakufariji.
31Ole wao wale waliokutesa,
na waliofurahia kuanguka kwako!
32Miji ile waliyoitumikia watoto wako kama watumwa itakuwa hali mbaya;
Mji ule uliowapokea watoto wako utapata balaa!
33Kama mji huo ulivyoshangilia kuanguka kwako,
na kufurahia kuangamia kwako,
vivyo hivyo nao utapatwa na uchungu kwa kuangamia kwake.
34Nitaondolea mbali majivuno yake juu ya wingi wa watu wake,
na kiburi chake kitageuka kuwa masikitiko.
35Mimi Mungu wa milele nitamshushia moto utakaowaka kwa siku nyingi;
utakuwa makazi ya pepo kwa muda mrefu.
36“Angalia upande wa mashariki, ee Yerusalemu,
uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu!
37Tazama, watoto wako uliowaacha waende wanakuja nyumbani.
wanakuja pamoja kutoka mashariki na magharibi,#4:37 Watoto …wanakuja pamoja kutoka mashariki na magharibi: Rejea Isa 43:5; 60:4; Bar 5:5. Maneno “kutoka mashariki na magharibi” hapa yamkini yana maana ya kutoka kila mahali, ingawa neno “mashariki” laweza kumaanisha Babuloni ambako walihamishiwa Waisraeli kwa wingi.
Kwa amri ya Mungu Mtakatifu,
wanakuja wakishangilia utukufu wake.”