DANIELI 10
BHNTLK

DANIELI 10

10
Maono ya Danieli kando ya mto Tigri
1Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Koreshi#10:1 Mwaka wa tatu wa …Koreshi: Au, mwaka 536 K.K. Taz 6:28 maelezo. wa Persia, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, alipewa ufunuo. Ufunuo huo ulikuwa wa kweli, lakini ulikuwa mgumu sana, haukueleweka. Hata hivyo alielewa ufunuo huo maana pia alifahamu maono.
2“Wakati huo, mimi Danieli, nilikuwa nikiomboleza kwa muda wa majuma matatu. 3Sikula chakula cha fahari, sikugusa nyama wala divai, na sikujipaka mafuta kwa muda wa majuma hayo yote matatu.
4“Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza,#10:4 Mwezi wa kwanza: Huu ulijulkana kama “Nisani” au pia “Abibu” na ulikuwa mwezi wa kwanza katika kalenda ya Waebrania yapata Machi-Aprili katika kalenda yetu. nilikuwa nimesimama kando ya mto Tigri. 5Nikainua macho, nikamwona mtu amevaa mavazi ya kitani na kiunoni amejifunga mkanda wa dhahabu kutoka Ufazi. 6Mwili wake uling'aa kama zabarajadi safi. Uso wake ulifanana na umeme, na macho yake yaliwaka kama miali ya moto. Miguu na mikono yake iling'aa kama shaba#10:5-6 Mtu amevaa …kitani …miguu …iling'aa kama shaba: Maelezo hayo yanaonesha kwamba mtu huyo ni malaika, labda malaika Gabrieli ambaye anatajwa mara kwa mara katika masimulizi ya Danieli (8:16). Vazi la kitani lilikuwa ishara ya usafi na lilitumika kama sare ya makasisi au makuhani. iliyosuguliwa sana. Sauti yake ilivuma kama sauti ya umati mkubwa wa watu.
7“Mimi Danieli peke yangu niliona maono hayo. Wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini walishikwa na hofu sana, wakakimbia, wakajificha. 8Hivyo, niliachwa peke yangu nikiangalia hayo maono ya kushangaza. Nguvu zikaniishia, na rangi yangu ikaharibika, nikabaki bila nguvu. 9Nilipoisikia sauti yake, nilianguka chini kifudifudi, nikashikwa na usingizi mzito. 10Hapo, mkono ukanigusa, ukanisimamisha, na kuimarisha miguu na mikono yangu. 11Akaniambia, ‘Danieli, wewe unayependwa sana, simama wima usikilize kwa makini maneno nitakayosema, maana nimetumwa kwako.’ Alipokuwa akiniambia maneno haya, mimi nilisimama nikitetemeka. 12Ndipo yeye akaniambia, ‘Danieli, usiogope. Mungu alilisikia ombi lako tangu siku ile ya kwanza ulipoamua kujinyenyekesha mbele yake ili upate ufahamu. Mimi nimekuja kwa ajili ya ombi lako hilo. 13Mkuu wa ufalme wa Persia alinipinga kwa muda wa siku ishirini na moja. Lakini Mikaeli, mmoja wa wakuu,#10:13 Mikaeli, mmoja wa wakuu: Huyu Mikaeli alikuwa malaika mlinzi wa Waisraeli (Dan 10:21; 12:1; Ufu 12:7). akaja kunisaidia, kwa hiyo nikamwacha huko pamoja na mkuu wa ufalme wa Persia, 14nami nimekuja kukusaidia uyafahamu mambo yatakayowapata watu wako wakati ujao, kwani maono uliyoona yanahusu wakati ujao.’
15“Alipokuwa ananiambia maneno hayo, niliangalia chini bila kuweza kuongea. 16Kisha, mmoja mwenye umbo la binadamu, aliigusa midomo yangu, nami nilifungua midomo yangu na kumwambia huyo aliyesimama karibu nami, ‘Ee bwana, maono haya yameniletea maumivu makali hata nimeishiwa nguvu. 17Mimi ni kama mtumwa mbele ya bwana wake. Nawezaje kuzungumza nawe? Sina nguvu na pumzi imeniishia!’
18“Yule mmoja aliyeonekana kama mwanaadamu akanigusa kwa mara nyingine, akanitia nguvu. 19Akaniambia, ‘Usiogope wewe unayependwa sana, uko salama. Uwe imara na hodari.’ Aliposema nami, nilipata nguvu, nikamwambia, ‘Bwana, umekwisha niimarisha; sema kile ulichotaka kusema.’ 20Naye akaniambia, ‘Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa ni lazima nirudi kupigana na malaika mlinzi wa Persia. Halafu, nitakapokuwa nimemshinda, malaika mlinzi wa mfalme wa Ugiriki atatokea. 21Lakini nitakujulisha yale yaliyoandikwa katika kitabu cha ukweli.#10:20-21 Kitabu cha ukweli: Hiki kinaweza kuwa kitabu ambacho kina orodha ya watu walio wake au kina matendo ambayo kila mtu alitenda. Sina mwingine wa kunisaidia kuwashinda hawa isipokuwa Mikaeli, malaika mlinzi wenu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza