3
Kushindwa kwa mfalme Ogu
(Hes 21:31-35)
1“Kisha, tuligeuka, tukapanda kuelekea Bashani. Mfalme Ogu#3:1 Mfalme Ogu: Alikuwa mfalme wa Bashani. Eneo la “Bashani” lilikuwa kaskazini-mashariki ya ziwa la Galilaya. Eneo hilo lilikuwa maarufu kwa rutuba yake na mashamba yake (taz Zab 22:12). alitoka na watu wake wote kupigana nasi karibu na mji wa Edrei. 2Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Usimwogope, maana nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake na nchi yake. Utamtendea kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori aliyekaa kule Heshboni’.
3“Basi, Mwenyezi-Mungu alimtia mikononi mwetu mfalme Ogu wa Bashani na watu wake, tukawaangamiza hata asibakie mtu yeyote. 4Tuliiteka miji yake yote; hakuna hata mji mmoja ambao hatukuuteka. Jumla tuliiteka miji sitini, yaani eneo lote la Argobu ambalo lilitawaliwa na mfalme Ogu wa Bashani. 5Miji yote hii ilikuwa na ngome zenye kuta ndefu, zilizokuwa na malango na makomeo. Kulikuwa pia na vijiji vingi ambavyo havikuzungukwa na kuta. 6Tuliteketeza kila kitu huko, tukaharibu kila mji na kuua wanaume, wanawake na watoto#3:3-6 Tuliteketeza kila kitu …wanaume, wanawake na watoto: Neno moja la Kiebrania “herem” linatumika kuelezea hali ya maangamizi ya kivita ambapo vitu vyote: miji, watu na wanyama, vilifikiriwa kuwa mali yake huyo anayeshinda na kwamba vitu hivyo ilibidi vitokomezwe kabisa. Hapa aghalabu panaonesha uwezo wa kutisha wa Mungu wa Waisraeli. Hiyo ilikuwa hali ya hapo kale ambapo kila kitu ilibidi kitengwe kwa ajili ya kutokomezwa kabisa. Wengine wanafikiri kwamba lengo lingine lilikuwa kuondolea mbali chochote ambacho kiliweza kuwazuia Waisraeli kumwabudu Mungu wao. kama tulivyofanya katika miji ya mfalme Sihoni wa Heshboni. 7Lakini mifugo yote na mali tulichukua nyara.
8“Wakati huo tuliitwaa nchi hiyo ya wale wafalme wawili wa Waamori waliokuwa wanakaa ng'ambo ya mto Yordani, katikati ya mto Arnoni na mlima Hermoni. 9(Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri). 10Tuliiteka miji yote katika sehemu tambarare za mwinuko, na pia eneo lote la Gileadi na Bashani mpaka Saleka na Edrei, miji ya mfalme Ogu huko Bashani.”
11(Mfalme Ogu ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa Warefai. Kitanda chake kilichotengenezwa kwa chuma,#3:11 Kitanda …chuma: Wengine wanafikiri “kitanda” hapa ni sawa na “sanduku la kuzikia maiti”. Majeneza makubwa yaligunduliwa kule Bashani. Ukubwa wa “kitanda” hicho unazingatia mazingira ya aya hii ambapo “Warefai” wanatajwa ambao walifikiriwa kuwa watu wa umbo kubwa sana. Taz tena 2:11 maelezo. kilikuwa na urefu wa mita nne na upana wa karibu mita mbili, kadiri ya vipimo vya kawaida. Kitanda hicho bado kipo katika mji wa Waamori wa Raba.)
Makabila yaliyokaa mashariki ya Yordani
(Hes 32:1-42)
12“Tulipoitwaa nchi hiyo, niliwapa makabila ya Reubeni na Gadi eneo la kuanzia kaskazini mwa Aroeri karibu na Arnoni na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake. 13Kisha nililipatia nusu ya lile kabila la Manase#3:13 Nusu …kabila la Manase: Kabila la Manase (mwanawe Yosefu) ambaye alipata baraka ya pekee ya babu yake, yaani Yakobo (Mwa 48), liligawanyika sehemu mbili: kundi moja lilipewa eneo lake upande wa mashariki ya mto Yordani na baadaye lingine likapewa eneo lake magharibi ya Mto Yordani. sehemu iliyobaki ya Gileadi pamoja na Bashani yote iliyotawaliwa na Ogu, yaani eneo lote la Argobu. (Nchi yote ya Bashani ilijulikana kama nchi ya Warefai.) 14Yairi, mtu wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu, yaani Bashani, hadi kwenye mpaka wa Geshuri na Maaka. Vijiji vyote alivipa jina lake, na hadi leo vinajulikana kama vijiji Hawoth-yairi.#3:14 Vijiji vya Yairi: Kiebrania ni “Hawoth-yairi”. Yairi alikuwa mtoto wa Manase. 15Watu wa ukoo wa Makiri wa kabila la Manase niliwapa Gileadi, 16na watu wa makabila ya Reubeni na Gadi niliwapa nchi yote kutoka Gileadi hadi mto Arnoni. Mpaka wao wa kusini ulikuwa katikati ya mto na wa kaskazini ulikuwa mto Yaboki ambao ndio unaopakana na nchi ya Waamori. 17Upande wa magharibi nchi yao ilienea hadi mto Yordani, toka ziwa Galilaya#3:17 Ziwa Galilaya: Kiebrania hapa kuna “Kinerethi”, jina lingine la ziwa hilo. upande wa kaskazini, ukashuka hadi bahari ya Araba,#3:17 Bahari ya Araba: Jina lingine ni “Bahari ya Chumvi”. yaani Bahari ya Chumvi, mpaka miteremko ya Pisga, upande wa mashariki.
18“Wakati ule niliwapa maagizo haya: ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni nchi hii mashariki ya mto Yordani iwe mali yenu. Sasa nyinyi mashujaa kati ya ndugu zenu, chukueni silaha mvuke mto Yordani mkiwa mbele ya ndugu zenu Waisraeli. 19Lakini wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu, najua mnayo mifugo mingi, watabaki kwenye miji niliyowapeni. 20Wasaidieni ndugu zenu Waisraeli mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowajalia watulie mahali pao kama nanyi mlivyotulia, yaani nao pia waimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapatia huko ng'ambo ya Yordani. Baada ya hayo, mtaweza kurejea katika nchi yenu hii ambayo nimewapeni iwe yenu!’#3:18-20 Kabla ya yale makabila ya Reubeni, Gadi na Manase (mashariki) kutulia kwenye maeneo yao, mashariki ya mto Yordani walitakiwa kusaidia majeshi ya makabila mengine ya Waisraeli kuyateka maeneo yao magharibi ya mto Yordani (taz pia Yos 1:12-15).
21“Kisha nikamwamuru Yoshua, ‘Wewe umeona kwa macho yako mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amewatendea wafalme hawa wawili, Sihoni na Ogu; basi, yeye atawatendea vivyo hivyo wafalme wa nchi zote mtakazopitia.#3:21 Katika Kiebrania majina ya hao wafalme wawili hayatajwi lakini ni dhahiri ni hao wanaohusika hapa (Kumb 2:26—3:11). 22Msiwaogope maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayepigana kwa ajili yenu.’#3:21-22 Mwenyezi-Mungu …ndiye atakayepigana kwa ajili yenu: Taz Kumb 2:24,34.
Mose akatazwa kuingia Kanaani
23“Wakati huo nilimsihi Mwenyezi-Mungu nikisema, 24‘Ee Bwana, Mwenyezi-Mungu, ninajua umenionesha mimi mtumishi wako mwanzo tu wa ukuu wako na uwezo wako. Maana, kuna mungu gani huko mbinguni au duniani awezaye kufanya mambo makuu na ya ajabu kama ulivyofanya wewe? 25Nakuomba nivuke mto Yordani, niione nchi hiyo nzuri magharibi ya Yordani; naam, nchi nzuri ya kupendeza ya milima, pamoja na milima ya Lebanoni’.
26“Lakini Mwenyezi-Mungu alinikasirikia kwa sababu yenu,#3:26 Kwa sababu yenu: Taz Hes 20:12 maelezo. Kadiri ya sehemu hii Mose hakuweza kuingia katika nchi ya Kanaani kwa vile Mungu alikasirika kwa sababu ya mwenendo wa watu wake. Taz Kumb 1:37; 4:21. akakataa kunisikiliza. Badala yake aliniambia, ‘Inatosha! Usiseme tena jambo hili. 27Panda mpaka kilele cha mlima Pisga, utazame vizuri upande wa magharibi, kaskazini, kusini na mashariki, na kuiona nchi hiyo; ila wewe hutavuka huu mto wa Yordani.#3:27 Mlima Pisga ulikuwa mojawapo ya vilele vya safu ya milima kaskazini-mashariki ya Bahari ya Chumvi, karibu na mlima Nebo (taz Hes 21:20); kutoka huko Mose aliweza kuiona nchi ya Kanaani. 28Lakini mpe Yoshua#3:28 Yoshua: Yeye alikuwa msaidizi mwaminifu wa Mose; alikuwa pamoja naye mlimani Sinai wakati Mose alipopewa ile sheria ya Mungu (Kut 32:17); tunaambiwa pia kwamba alikuwa kamanda wa jeshi (Kut 17:8-13) na mmoja wa watu wale ambao Mose aliwapeleka kuipeleleza nchi ya Kanaani (Hes 13). Yoshua na Kalebu ndio peke yao miongoni mwa kizazi chote kilichotoka Misri waliowahi kuingia nchini Kanaani. maagizo, umtie moyo na kumuimarisha, maana yeye ndiye atakayewaongoza watu hawa hadi ng'ambo, kuimiliki nchi utakayoiona’.
29“Basi, tukabaki hapa bondeni mbele ya Beth-peori.”#3:29 Beth-peori: Yaani “Nyumba (au hekalu) ya Peori”. Mahali karibu na mlima Pisga (taz Yos 13:20). Jina hili linakumbusha kisa cha “Baali-peori” ambapo Waisraeli walimwasi Mungu wakamwabudu mungu wa watu wa Kanaani aliyejulikana kama Baali (Hes 25:3; 31:16; Yos 22:17).