1
Maisha ni bure kabisa
1Yafuatayo ni maneno ya Mhubiri#1:1 Mhubiri: Taz pia 1:12. Jina hili la sifa linatafsiri kile tulicho nacho katika Kiebrania kama “Kohelethi”, neno ambalo lina uhusiano na “kahal” kanisa (“eklesiastes” katika tafsiri ya Kigiriki). mwana wa Daudi, aliyekuwa mfalme huko Yerusalemu.
2Bure kabisa, bure kabisa,#1:2 Bure kabisa: Maneno haya yanatafsiri msemo wa Kiebrania ambao una maana ya kitu ambacho hakina maana, si cha kudumu na hakina sababu ya kuweko, kama vile ndoto au pumzi Kiebrania “hebel” - pumzi ya binadamu hutoweka upesi na haidumu. Wazo hilo linatiliwa mkazo kwa kuonesha undani wa hali ya binadamu wa kupita tu hapa duniani, wazo ambalo linapatikana pia katika Zab 62:9. Kutokana na mtindo huo, inawezekana kutafsiri pia kama: “Kila kitu hakifai, hakifai kabisa!”
nakuambia mimi Mhubiri!
Kila kitu ni bure kabisa!
3Binadamu hufaidi nini#1:3 Binadamu hufaidi nini …?: Hili ni swali lisilodai majibu. Lengo la maswali ya mtindo huu ni kusisitiza jambo na kuliimarisha. Mwandishi anarudia wazo hilo; yaani mambo anayotenda binadamu, hata yale ya kuwaza na kuwazua ni ya bure, hayafai kabisa (2:22), na yeye mwandishi mwenyewe, hekima yake haifai kitu (1:16-12; 2:1).
kwa jasho lake lote hapa duniani?#1:3 Hapa duniani: Neno kwa neno “chini ya jua”. Mwandishi anarudia msemo huu hapa na pale katika kitabu chake mara 25. Ndio kusema anasisitiza kwamba tatizo analolishughulikia na kuliwaza ni la hapa hapa duniani tunapoishi.
4Kizazi chapita na kingine chaja,
lakini dunia yadumu daima.#1:4-7 Kwanza mwandishi anachunguza matukio ya maumbile ambamo binadamu anaishi (aya 4-11); humo kila kitu kimo daima katika mizunguko lakini kutokana na mizunguko hiyo hamna lolote jipya katika marudio ya mizunguko hiyo. Ingawa mizunguko hiyo ya maumbile inakinaisha, au inasababisha uchovu (1:8), ni mizunguko hiyohiyo ambayo hufanikisha uhai wa vitu. Taz Mwa 8:22; Zab 104:30.
5Jua lachomoza na kutua;
laharakisha kwenda machweoni.
6Upepo wavuma kusini,
wazunguka hadi kaskazini.
Wavuma na kuvuma tena,
warudia mzunguko wake daima.
7Mito yote hutiririkia baharini,
lakini bahari kamwe haijai;
huko ambako mito hutiririkia
ndiko huko inakotoka tena.
8Mambo yote husababisha uchovu,
uchovu mkubwa usioelezeka.
Jicho halichoki kuona,
wala sikio kusikia.
9Yaliyokuwako ndio yatakayokuwako,
yaliyotendeka ndio yatakayotendeka;
duniani hakuna jambo jipya.
10Watu husema, “Tazama jambo jipya,”
kumbe lilikwisha kuwako zama za kale.
11Hakuna mtu anayekumbuka#1:8-11 Yote husababisha uchovu …hakuna mtu anayekumbuka …: Wengine wanafikiri mwandishi anaona kuwa mambo hayo yanasababisha uchovu na kukinaisha kutokana na kurudiarudia kwake kwa sababu ameshindwa kufahamu mpango wa Mungu. Hata hivyo katika 3:11 mwandishi anaamini kwamba Mungu hufanya kila kitu kitukie kwa wakati wake alioupanga tangu zama za kale. Kwa hiyo mwandishi anajiona hawezi kitu. ya zamani
wala atakayekumbuka yatakayotukia baadaye.
Aliyoyaona Mhubiri
12Mimi Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli, huko Yerusalemu.#1:12 Nilikuwa mfalme wa Israeli, huko Yerusalemu: Taz utangulizi kwa kitabu hiki cha Mhubiri. Katika sehemu hii vitu ambavyo vilisemwa juu ya Solomoni katika vitabu vya Wafalme vinarudiwa. Kuhusu hekima yake (1:16), taz 1Fal 4:29-31; kuhusu utajiri wake (2:4-8) taz 1Fal 10:10,14-22,23-27, n.k. Katika Meth 1:16-17 msomaji hataacha kumfikiria Solomoni wakati anafuata wazo linalotolewa katika aya hizo. Si ajabu basi kwamba wengi walifikiri Solomoni ndiye aliyekuwa mwandishi wa kitabu hiki. 13Nilipania kuchunguza na kutafuta kwa hekima kila kitu kinachotukia duniani. Hiyo ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu.
14Nimeyaona yote yanayofanywa duniani; yote ni bure: ni sawa na kufukuza upepo!#1:13-14 Nilipania kuchunguza …nimeyaona yote … kufukuza upepo “Nilipania”, au, neno kwa neno: “Niliutia moyo wangu”, neno “moyo” likitumika katika maana yake ya kikao cha mawazo na maamuzi ya binadamu kulingana na utamaduni wa lugha ya Waebrania (na pia kwa Waswahili – moyo ni kikao cha mawazo, uamuzi, n.k.). Fungu la maneno “kufukuza upepo” ni msemo ulioongezwa katika ule wa kawaida: “Bure kabisa, bure kabisa” ili kutilia mkazo zaidi wazo hilo hilo. Tafsiri nyingine yamkini: “ni sawa na kukimbizana na upepo” au, “ni shughuli ya bure” (2:11,17,26; 4:4,6; 6:9).
15Kilichopindika hakiwezi kunyoshwa,
kisichokuwapo hakiwezi kuhesabiwa.
16Basi, nikatafakari nikisema, “Nimejipatia hekima nyingi zaidi kupita wote waliopata kutawala Yerusalemu kabla yangu. Naam, nina uzoefu wa hekima na maarifa.”#1:16-17 Mwandishi wa kitabu hiki anachunguza yanayomwafiki yeye binafsi na maamuzi anayotoa kuhusu la kufanya, lakini anagundua ukweli wake (taz pia 2:1-2).
17Nilipania kubainisha kati ya hekima, wazimu na upumbavu. Lakini niligundua kwamba kufanya hivyo ni sawa na kufukuza upepo.
18Maana katika kuwa na hekima nyingi mna wasiwasi;
na aongezaye maarifa zaidi huongeza huzuni zaidi.#1:18 Hekima nyingi mna wasiwasi …maarifa zaidi huongeza huzuni zaidi: Hapa “hekima” na “maarifa” ni maneno sambamba yenye maana ileile. Katika methali ya Kiswahili “hekima nyingi huondoa maarifa” maneno hayo yanatumika kwa namna tofauti, “maarifa” likiwa ni uzoefu wa kufanya kitu. Katika Mhub 7:5,11,12,19 hekima inayopatikana kwa kuchunguza vitu na kufikiria barabara ni ya kutamanika. Lakini hekima hiyo haitoshelezi suala kubwa lenye kumkera binadamu - kuelewa mambo ya Mungu (Mhub 3:11). Mtazamo huu kidogo unasaidia tusimmwone Mhubiri kuwa kabisa mtu asiye na rajua au mkosa tumaini lolote. Kulingana na Methali hekima ya kweli yatoka kwa Mungu na hupewa wale wanaomtii Mungu (Meth 2:6-7; taz pia Mhu 12:13-14).