10
1Nzi waliokufa husababisha marashi kunuka;#10:1 Nzi waliokufa …marashi kunuka: Maana ya methali hii ni dhahiri kama Mwanafalsafa mwenyewe anavyotamka kwa maneno mengine katika mstari wa pili ambao ni sambamba na huo wa kwanza.
upumbavu kidogo hubatilisha hekima na heshima.#10:1-20 Baada ya mwandishi kutoa mfano wa jinsi maskini mwenye hekima anavyoweza kupuuzwa (9:13-18), huyu Mwanafalsafa anatupatia methali kadha wa kadha ambazo kwa wingi zinahusu tofauti iliyopo kati ya watu wenye hekima na wapumbavu.
2Moyo wa mwenye hekima humwongoza kutenda yaliyo sawa;
lakini mtu mpumbavu moyo wake humpotosha.
3Hata apitapo njiani, mpumbavu hutambulikana hivyo,
humjulisha kila mtu kwamba yeye ni mpumbavu.
4Mtawala akikuwakia hasira, usijiuzulu;
makosa makubwa huweza kufutwa ukiwa mnyenyekevu.
5Kuna uovu niliogundua hapa duniani, uovu unaosababishwa na watawala: 6Kwamba wapumbavu wanapewa kazi za madaraka ya juu, na matajiri wanachukua nafasi za mwisho. 7Nimeona watumwa wanapanda farasi, na wakuu wanatembea kwa miguu kama watumwa.
8Mchimba shimo hutumbukia mwenyewe,#10:8-9 Mchimba shimo hutumbukia mwenyewe: Hii ni methali ambayo inajulikana hata katika lugha zetu. Kuhusu mitego inayowanasa walioitega taz Zab 7:15.
abomoaye ukuta huumwa na nyoka.
9Mchonga mawe huumizwa nayo,
mkata kuni hukabiliwa na hatari.
10Nguvu nyingi zaidi zahitajika
kwa mtumiaji shoka butu lisilonolewa,
lakini kutumia hekima humfanya mtu afanikiwe.
11Nyoka akiuma kabla hajachochewa,
mchochezi #10:11 Mchochezi: Huyu alikuwa mtu ambaye aliweza kumthibiti nyoka afanye anachotaka, desturi iliyokuwa kawaida katika Mashariki ya Kati ya Kale. Katika Kiebrania neno lilotafsiriwa hapa kama “mchochezi” ni “mwenye kuuthibiti ulimi” ikimaanisha au ulimi wa nyoka ambao ulidhaniwa ndio wenye sumu, au huyo mtu na namna alivyotumia sauti yake kumthibiti huyo nyoka. Iwe iwavyo aya 10:11 ni mwito wa mtu kutumia hekima maana hata wenye ujuzi hushindwa wasipotumia ujasiri.hahitajiki tena.
12Maneno ya mwenye hekima humnufaisha asemaye;
lakini midomo ya mpumbavu humwangamiza.
13Mpumbavu huanza kusema kwa maneno ya kijinga,
na kumaliza kauli yake kwa wazimu mbaya.
14Mpumbavu hububujika maneno.
Binadamu hajui yatakayokuwako,
wala yale yatakayotukia baada yake.
15Mpumbavu huchoshwa na kazi yake
hata asijue njia ya kurudia nyumbani.
16Ole wako, ewe nchi, mtawala wako akiwa kijana,
na viongozi wako wakifanya sherehe asubuhi.
17Heri yako, ewe nchi, mtawala wako akiwa mtu wa heshima,
na viongozi wako wakifanya sherehe wakati wa kufaa,
ili kujipatia nguvu na si kujilewesha.#10:16-17 Viongozi …si kujilewesha: Kunywa mapema ni ishara ya utovu wa nidhamu (Isa 5:11). Rejea pia Isa 5:22-23. Hatari za hali ya namna hiyo zilitajwa pia katika mawaidha kwa Lemueli (Meth 31:4-5).
18Kutokana na uvivu wa mtu, paa hubonyea;
kwa sababu ya uzembe, nyumba huvuja.
19Chakula ni kwa ajili ya kujifurahisha,
divai huchangamsha maisha;
na fedha husababisha hayo yote.#10:19 Fedha husababisha hayo yote: Tafsiri yamkini na maana yake si dhahiri. Inaonekana lakini kwamba mwandishi anataka kusema kwamba wenye fedha, yaani matajiri hawataweza daima kujinasua na maisha ya namna hiyo.
20Usimwapize mtawala hata moyoni mwako,
wala usimwapize tajiri hata chumbani mwako unakolala,
kwa kuwa ndege ataisikia sauti yako,
au kiumbe arukaye atatangaza maneno yako.