Kutoka 15
BHNTLK

Kutoka 15

15
Wimbo wa Mose#15:1-18 Wimbo wa Mose: Utenzi au wimbo huu wa ushindi ni shairi. Wenyewe unarudia matukio ya sura iliyotangulia na waweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza (aya 1-12) inashangilia ushindi wa Mwenyezi-Mungu juu ya jeshi la Wamisri; sehemu ya pili (aya 13-18) inaonesha Mungu anavyowaongoza Waisraeli kule jangwani hadi nchini Kanaani. Ufu 15:3 inagusia utenzi huu.
1Hapo, Mose pamoja na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi-Mungu wimbo huu,
“Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari,
farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.
2Mwenyezi-Mungu#15:2 Mwenyezi-Mungu: Kiebrania ni “Yah”, kifupisho cha jina “Yahweh”. Taz Kut 3:15 maelezo. hunijalia nguvu na uwezo,
yeye mwenyewe ndiye anayeniokoa.
Yeye ni Mungu wangu nami nitamsifu,
ni Mungu wa baba yangu#15:2 Baba yangu: Msemo wa jumla wa kuwataja wazee (mababu) wa Waisraeli (taz 3:16). nami nitamtukuza.
3Mwenyezi-Mungu ni shujaa vitani;
Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake.
4“Magari na majeshi ya Farao ameyatumbukiza baharini,
maofisa wake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.
5Vilindi vya maji vimewafunika,
wameporomoka baharini kama jiwe.
6“Mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu watukuka kwa nguvu;
kwa mkono wako wa kulia#15:6 Mkono wako wa kulia: Hapo kale msemo “upande wa kulia” na hapa “mkono wa kulia” ulifikiriwa kuwa ndio upande wa heshima (au mkono) wenye nguvu. ee Mwenyezi-Mungu wawaponda adui.
7Kwa wingi wa ukuu wako wawaangamiza wapinzani wako;
wawapulizia ghadhabu yako nayo yawateketeza kama makapi.
8Kwa pumzi ya pua yako#15:8 Kwa pumzi ya pua yako: Lugha ya kishairi ya kusema upepo mkali wa mashariki (taz pia 14:21). maji yalirundikana,
mawimbi yakasimama wima kama ukuta;
vilindi katikati ya bahari vikagandamana.
9Adui alijisemea, ‘Nitawafuata na kuwakamata;
nitagawanya nyara mpaka hamu yangu iishe.
Tutaufuta upanga wetu,
tutawaangamiza kwa mkono wetu.’
10Lakini wewe uliuvumisha upepo wako,
nayo bahari ikawafunika.
Walizama majini kama risasi.
11“Ewe Mwenyezi-Mungu,
ni nani kati ya miungu anayelingana nawe?
Ni nani aliye kama wewe uliye mtakatifu mkuu,
utishaye kwa matendo matukufu,
unayetenda mambo ya ajabu?
12Uliunyosha mkono wako wa kulia,
nayo nchi ikawameza maadui zetu.
13 # 15:13-17 Kuhusu uongozi wa Mwenyezi-Mungu kama mchungaji taz Zab 23. Picha tunayopewa katika aya hizi hasa aya 17 ni ya hali ya baadaye, baada ya kutoka Misri na kuhamia nchini Kanaani. “Kwa fadhili zako kuu umewaongoza watu uliowakomboa,
kwa nguvu yako umewaongoza kwenye makao yako matakatifu.#15:13 Makao yako matakatifu: Neno “makao” linatafsiri neno la Kiebrania ambalo mara kwa mara hutumiwa kutaja makazi ya wachungaji au shamba la majani mabichi (Zab 23:2); mara nyingine linatumika kutaja nchi ya Kanaani ambayo Waisraeli waliahidiwa (13:5).
14Watu wa mataifa wamesikia hayo wakatetemeka;
wakazi wa Filistia wamekumbwa na kitisho.
15Wakuu wa Edomu wamefadhaishwa;
viongozi wa Moabu#15:14-15 Filistia …Edomu …Moabu: Taz Kut 13:17 maelezo. Mara nyingi Wafilisti walipigana na Waisraeli nyakati za Waamuzi. Nchi ya Edomu (inaitwa pia Seiri) ilikuwa kusini-mashariki ya Bahari ya Chumvi na wakazi wake walikuwa wazawa wa Esau (Mwa 36:1-43). Wamoabu nao walikaa katika eneo la mashariki ya Bahari ya Chumvi. Wao, pamoja na Waamoni wanatajwa kama maadui wakubwa wa Waisraeli (taz Amu 10:11-18; 1Sam 14:48; 2Fal 3:21-27). wamekumbwa na woga mkuu;
wakazi wote wa Kanaani wamevunjika moyo.
16Kitisho na hofu vimewavamia.
Kwa sababu ya ukuu wa nguvu zako,
wao wamenyamaza kimya kama jiwe,
mpaka watu wako ee Mwenyezi-Mungu, wapite,
naam, mpaka watu hao uliowakomboa wamewapita.
17Wewe utawaleta watu wako na kuwapanda mlimani pako;#15:17 Mlimani pako: Mlima hapa yawezekana kuwa ni neno la kutaja Mlima Siyoni kule Yerusalemu. Mfalme Solomoni alimjengea Mwenyezi-Mungu hekalu huko yapata mwaka 350 baada ya Waisraeli kutoka Misri.
pale ulipochagua ee Mwenyezi-Mungu pawe makao yako,
mahali patakatifu ee Mwenyezi-Mungu ulipojenga kwa mikono yako.
18Wewe, ee Mwenyezi-Mungu,
watawala milele na milele.”
19Wakati farasi wa Farao na magari yake pamoja na wapandafarasi wake walipoingia mahali pakavu baharini, Mwenyezi-Mungu aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika. Lakini Waisraeli waliendelea kutembea pakavu katikati ya bahari.
20Basi nabii Miriamu,#15:20 Miriamu: Miriamu ambaye anatajwa pia kama nabii, yamkini alikuwa dada mkubwa wa Mose na ambaye alisaidia kumwokoa mtoto Mose na kumpatia mama Mwebrania (mama yao mwenyewe) wa kumnyonyesha na kumlea kwa niaba ya binti Farao ambaye alimgundua mtoni Nili (Kut 2:1-10). Kuhusu watu wanaoitwa manabii taz orodha ya manabii katika Utangulizi kwa Vitabu vya manabii. dada yake Aroni, akachukua kingoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vingoma vyao wakicheza. 21Miriamu akawaongoza kwa kuimba,
“Mwimbieni Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari,
farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.”#15:21 Mwimbieni …amewatosa baharini: Utenzi wa Miriamu karibu ni sawa na ule wa Mose (rejea aya 1) na huu utenzi, hasa aya hii yamkini ulitumiwa kama kiini cha wimbo wote ambao uliongezwa hapo baadaye.
Maji machungu
22Kisha, Mose aliwaongoza Waisraeli kutoka bahari ya Shamu, wakaenda mpaka jangwa la Shuri.#15:22 Jangwa la Shuri: Jangwa hilo lilikuwa mashariki ya Gosheni, kwenye sehemu ya kaskazini ya Peninsula ya Sinai (taz ramani). Walisafiri kwa muda wa siku tatu jangwani bila kuona maji yoyote. 23Walipofika mahali panapoitwa Mara, hawakuweza kuyanywa maji ya Mara kwa sababu yalikuwa machungu. Kwa sababu hiyo mahali hapo pakaitwa Mara.#15:23 Mara: Kiebrania maana yake ni “chungu” (taz pia Rut 1:20). 24Basi, watu wote wakamlalamikia Mose#15:24 Wakamlalamikia Mose: Kuhusu malalamiko ya Waisraeli taz 14:11-12 maelezo. wakisema, “Sasa tutakunywa nini?” 25Hapo Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamwonesha kipande cha mti, na Mose akakitumbukiza katika maji; maji hayo yakawa mazuri.
Huko Mungu aliwapa Waisraeli amri na agizo, ili ajue uthabiti wao, 26akawaambia, “Ikiwa mtaisikiliza kwa makini sauti yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kutenda yaliyo sawa mbele yangu, na kuheshimu amri na maagizo yangu yote, basi, mimi sitawaletea yale magonjwa niliyowaletea Wamisri. Kwa sababu, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya#15:26 Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya: Tamko muhimu katika Biblia juu ya Mungu na ambalo hutumika mara kwa mara (Kumb 7:15; 32:39; Yer 17:14; 30:17; Zab 41:3-4). Yahusu sio tu kuponya magonjwa ya mwili, bali pia msamaha wa dhambi na kuokolewa kwa jumla (taz Yak 5:15). nyinyi.”
27Kisha Waisraeli wakawasili huko Elimu#15:27 Elimu: Mahali penyewe siku hizi hapajulikani. Lakini yamkini ni Wadi Gharandel (taz pia 16:1; Hes 33:9-10), yapata kilomita mia moja na thelathini kusini-mashariki ya Mfereji wa Suezi. Katika Hes 33:9 inasemwa kuwa huko kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende kwa wingi. ambako kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende sabini. Wakapiga kambi yao huko karibu na maji.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza