Kutoka 19
BHNTLK

Kutoka 19

19
Waisraeli mlimani Sinai#19:1-25 Waisraeli mlimani Sinai: Kwa sura hii tunafikia sehemu na mazingira mapya katika kitabu hiki cha Kutoka. Sehemu yenyewe (sura 19—24) ni muhimu kwa namna ya pekee kwa sababu inasimulia jinsi Mungu alivyoweka uhusiano wa pekee na watu wake na kufanya nao agano au mkataba.
1Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu tangu walipotoka nchini Misri, watu wa Israeli walifika katika jangwa la Sinai.#19:1-2 Jangwa la Sinai: Eneo lote la Sinai lina milimamilima na kuna mlima mmoja ambao ni mrefu kuliko mingine, karibu katikati ya hiyo peninsula unaoitwa Jebel Musa, wenye urefu upatao mita 22 mpaka 85. Kulingana na mapokeo mlima huo, ndio unaohusika hapa. 2Walipoondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, huko walipiga kambi mbele ya mlima Sinai. 3Basi, Mose akapanda juu mlimani kwa Mungu.#19:3 Mlimani kwa Mungu: Katika Mashariki ya Kati ya Kale, kama katika mahali pengine Afrika, milima ilifikiriwa kuwa makao ya miungu. Nao Waisraeli waliamini kuwa Mwenyezi-Mungu alikaa juu ya mlima Sinai (au Horebu). Taz pia maelezo ya 3:1. Na kuhusu Mose kupanda juu mlimani kwa Mungu ni jambo linalorudiwa mara kwa mara katika sehemu hii; Mose anasemekana kwenda kwa Mungu na kurudi tena kwa watu wake. Vitendo hivi vinamweka Mose kuwa aghalabu mjumbe au mpatanishi kati ya Mungu na Waisraeli. Na, kuhusu “Mwenyezi-Mungu” taz tena 3:15 maelezo. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwita Mose kutoka huko juu mlimani, akamwambia, “Hivi ndivyo utakavyowaambia wazawa wa Yakobo, hao Waisraeli, 4‘Nyinyi wenyewe mmeona nilivyowatenda Wamisri na jinsi nilivyowachukua kama tai#19:4 Nilivyowachukua kama tai: Tai alijulikana kama ndege mwenye nguvu, na alidhaniwa kuyabeba makinda yake katika mabawa yake (taz pia Kumb 32:11). Picha hiyo ni mwafaka kabisa hapa na inaonesha nguvu ya Mwenyezi-Mungu na ulinzi anaowapa watu wake. Taz pia Isa 49:15 ambapo Mungu anaelezwa kama mama na watoto wake. anavyochukua watoto wake kwa mabawa, nikawaleta kwangu. 5Sasa basi, kama mkiitii sauti yangu na kulishika agano langu,#19:5 Agano langu: Agano au mkataba, linaweza kuwa mapatano kati ya watu wawili au vikundi vya watu walio katika hali ya usawa kwa mfano Mwa 31:44; 1Fal 15:19. Au, na hasa maana hii ndiyo inayoafiki hapa, linaweza kuwa mkataba ambao mkuu anamwekea mdogo. Mkuu anamtaka mdogo kuwa mwaminifu kwake na wakati huohuo huyo mkuu mwenye kuweka agano hilo au mkataba anaahidi kumlinda huyo mdogo. Mwenyezi-Mungu anajionesha kuwa yeye ndiye mkombozi wa watu wake (aya 4) na hivyo anawaalika kushiriki agano lake. Kwa upande wao, Waisraeli sharti watambue kwamba Mungu anayo haki ya kuwa mkuu wao na wanapaswa kuahidi kutimiza matakwa yake (24:3) na hivyo kukamilisha ahadi ya Kut 6:7: “Nitawafanyeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu”. mtakuwa watu wangu wateule#19:5 Watu wangu wateule: Au: “watu wangu wa pekee”. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa kwa “wateule” linachukua pia maana ya kitu cha thamani kubwa. kati ya mataifa yote, maana dunia yote ni yangu. 6Mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani#19:6 Ufalme wa makuhani: Katika A.K. makuhani walikuwa wazawa wa Aroni ambaye ndiye babu wa Walawi (Kut 28:1; Hes 18:20-32). Lakini watu wote wa Mungu ni watu wake watakatifu, yaani waliotengwa kwa ajili yake Mungu wamtumikie mithili ya makuhani. Hiyo ilikuwa kwa Waisraeli. Vilevile katika A.J. Wakristo wote nao pia wametengwa kumtumikia Mungu kama vile makuhani (1Pet 2:9; Ufu 1:6). na taifa takatifu.’ Hayo ndiyo maneno utakayowaambia Waisraeli.”
7Basi, Mose akarudi, akawakusanya pamoja wazee wa Waisraeli na kuwaambia maneno hayo aliyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 8Watu wote wakaitikia kwa pamoja wakisema, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.”#19:8 Mambo yote aliyosema Mwenyezi-Mungu tutayafanya: Maneno haya ni muhimu kabisa katika shughuli hiyo ya kuratibisha agano. Waisraeli wanakubali kufungwa na masharti hayo ya agano. Taz pia Kut 24:3. Mose akamjulisha Mwenyezi-Mungu jibu hilo la watu. 9Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Haya, mimi nitakujia katika wingu zito ili Waisraeli wapate kunisikia ninaposema nawe na kukuamini siku zote.”
Kisha Mose akamwambia Mungu jinsi watu walivyosema. 10Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa watu uwatakase leo na kesho. Waambie wayafue mavazi yao 11wawe tayari kwa kesho kutwa, maana siku hiyo ya tatu mimi Mwenyezi-Mungu nitashuka juu ya mlima Sinai mbele ya watu wote. 12Tena wewe utawawekea watu mpaka kuzunguka mlima. Utawakanya wajihadhari sana wasipande juu mlimani wala kuugusa mpaka wake. Yeyote atakayeugusa mlima, atauawa. 13Mtu asimguse mtu huyo; atauawa kwa kupigwa mawe au mshale awe ni mtu au ni mnyama, hataishi. Wakati mbiu itakapopigwa mfululizo, watu wote watakaribia mlimani.”#19:12-13 Yanayosemwa hapa yananukuliwa katika Ebr 12:18-23. “Mbiu” mara nyingine hutafsiriwa kwa neno “tarumbeta” (au pia “baragumu”, au hata “parapanda”) na ilitumiwa kuashiria sikukuu za kidini
14Basi, Mose akashuka mlimani na kuwaendea watu, akawatakasa, nao wakayafua mavazi yao. 15Kisha akawaambia watu wote, “Kesho kutwa muwe tayari, na mwanamume yeyote asimkaribie mwanamke.”
16Basi, siku ya tatu asubuhi, kukatokea ngurumo na umeme#19:16-18 Ngurumo na umeme: Taz Ufu 4:5 na Kut 9:23 maelezo. Katika Biblia matukio kama hayo na pia moto na moshi mara nyingi yaliashiria kuweko kwa Mungu. na wingu zito juu ya mlima. Ikasikika pia sauti kubwa ya mbiu ambayo iliwatetemesha watu wote kambini. 17Kisha Mose akawaongoza watu wote kutoka kambini, wakaenda kukutana na Mungu. Wote walikwenda wakajipanga chini ya mlima.
18Mlima wa Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi wa tanuri kubwa na mlima wote ulitetemeka kwa nguvu. 19Sauti ya mbiu ilizidi kuongezeka, na Mose akaongea na Mungu. Mungu naye akamjibu katika ngurumo.
20Mwenyezi-Mungu alishuka juu ya mlima Sinai, akamwita Mose kutoka huko juu, naye Mose akapanda mlimani. 21Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Shuka chini ukawaonye watu wote wasije kunitazama; la sivyo wengi wao wataangamia. 22Hata makuhani ambao hunikaribia wanapaswa kujitakasa; la sivyo nitawaadhibu.” 23Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Watu hawa hawawezi kuupanda mlima wa Sinai kwani wewe mwenyewe ulituamuru tuweke mpaka kuuzunguka mlima.” 24Mwenyezi-Mungu akasema, “Teremka chini kisha urudi pamoja na Aroni. Lakini usiwaruhusu makuhani na watu wengine wapite mpaka na kuja kwangu, la sivyo nitawaadhibu.” 25Basi, Mose akashuka na kuwaambia Waisraeli mambo yote aliyoagizwa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza