Ezekieli 15
BHNTLK

Ezekieli 15

15
Mfano wa mzabibu#15:1-8: Matumizi ya mzabibu kama mfano au kielezo hutumika mara kadhaa katika Biblia (Hos 10:1; Isa 5:1-7; Yer 2:21 Eze 17:6-8; 19:10-14; Marko 12:1-11 mfano wa watu wa Mungu); lakini hapa Ezekieli anautumia kwa kuonesha hali yake hafifu na dhaifu.
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Je, mti wa mzabibu ni bora kuliko miti mingine msituni? 3Je, mti wake wafaa kutengenezea kitu chochote? Je, watu huweza kutengeneza kigingi kutoka mti huo ili waweze kutundikia vitu? 4Huo wafaa tu kuwashia moto. Tena moto unapoteketeza sehemu yake ya mwanzo na ya mwisho na kuikausha sehemu ya katikati, je, hiyo yafaa kwa kitu chochote?#15:4 Hapa tunapewa picha ya hali ya Yerusalemu ambao umekwisha kabiliwa na uhamisho wa kwanza (taz aya ya 6). 5Ulipokuwa haujachomwa ulikuwa haufai kitu, sembuse sasa baada ya kuteketezwa kwa moto na kuwa makaa! Haufai kitu kabisa. 6Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kama vile nilivyoutoa mti wa mzabibu kati ya miti ya msituni, ukateketezwa motoni, ndivyo nilivyotoa wakazi wa Yerusalemu. 7Nitawakabili vikali. Hata kama wataukimbia moto, huo moto utawateketeza. Hapo nitakapowakabili vikali, ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. 8Kwa kuwa wamekosa uaminifu kwangu, nitaifanya nchi yao kuwa ukiwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza