Ezekieli 7
BHNTLK

Ezekieli 7

7
Mwisho wa Israeli ni karibu
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu, waambie wakazi wa nchi ya Israeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Sasa ni mwisho!
Mwisho umeifikia nchi yote kutoka pande zote nne!
3Sasa mwisho umewafikia;
sasa mtausikia ukali wa hasira yangu juu yenu.
Nitawahukumu kadiri ya mwenendo wenu.
Nitawaadhibu kwa machukizo yenu yote.
4Sitawaachia wala sitawahurumia;
nitawaadhibu kulingana na mienendo yenu,
maadamu machukizo bado yapo kati yenu.
Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
5Ninachosema mimi Bwana Mwenyezi-Mungu ni hiki:
Mtapatwa na maafa mfululizo!#7:5 Maafa mfululizo: Labda hivyo kutoka Kiebrania kigumu cha aya hii.
6Mwisho umekuja!
Naam, mwisho umefika!
Umewafikia nyinyi!
7Enyi wakazi wa nchi hii, maangamizi yenu yamewajia!
Wakati umekuja;
naam, siku imekaribia.
Hiyo ni siku ya msukosuko
na siyo ya sauti za shangwe mlimani.#7:7 Aya ya 7 maana yake katika Kiebrania si dhahiri.
8Sasa mtausikia uzito wa hasira yangu juu yenu.
Nitawahukumu kulingana na mwenendo wenu;
nitawaadhibu kadiri ya machukizo yenu.
9Sitawaachilia wala sitawaonea huruma.
Nitawaadhibu kulingana na mienendo yenu
maadamu machukizo yapo bado miongoni mwenu.
Ndipo mtakapotambua kuwa ni mimi Mwenyezi-Mungu ninayewaangamiza.
10“Tazameni, siku ile inakuja!
Maangamizi yenu yamekuja.
Ukatili uko kila mahali na kiburi kimechanua.#7:10 Ukatili …kiburi kimechanua: Labda hivyo. Kiebrania, “fimbo imechanua” (rejea aya 11). Maneno haya aghalabu yanaonesha jinsi uvunjaji wa haki za watu ulivyoongezeka. Manabii wengi walipiga vita hali hiyo (taz Amo 2:6-8; 4:1; 5:10-13; Isa 1:16-17,21-23; 5:8-23).
11Ukatili unaendelea kuwa mbaya zaidi.
Hakuna hata mmoja wenu atakayebaki,
wala vitu mlivyojirundikia kwa wingi au utajiri wenu;
hatakuwako mtu mwenye heshima miongoni mwenu.#7:11 Makala ya Kiebrania ya sehemu ya tatu ya aya hii si dhahiri.
12Wakati umewadia,
naam, ile siku imekaribia.
Mnunuzi asifurahi wala mwuzaji asiomboleze;
kwa sababu ghadhabu yangu itaukumba umati wote.
13Wauzaji hawataweza kurudia mali yao waliyouza
hata kama wakibaki hai.
Kwani maono haya yahusu umati wote na hayatabatilishwa.
Kutokana na uovu huo, hakuna mtu atakayesalimisha maisha yake.
14Tarumbeta imepigwa na kuwafanya wote wawe tayari.
Lakini hakuna anayekwenda vitani,
kwani ghadhabu yangu iko juu ya umati wote.
15Nje kuna kifo kwa upanga
na ndani ya mji kuna maradhi mabaya na njaa.
Walioko shambani watakufa kwa upanga;
walio mjini njaa na maradhi mabaya yatawaangamiza.
16Wakiwapo watu watakaosalimika
watakimbilia milimani kama hua waliotishwa bondeni.#7:16 Hua …bondeni: Picha tunayopewa hapa si dhahiri. “ataomboleza”: Kiebrania; hati mbili za kale zina “atakufa”.
Kila mmoja wao ataomboleza kwa dhambi zake.
17Kila mtu, mikono yake itakuwa dhaifu
na magoti yake yatakuwa maji.
18Watavaa mavazi ya gunia,
hofu itawashika,
nao watakuwa na aibu,
vichwa vyao vyote vitanyolewa.#7:18 Watavaa mavazi ya gunia …vichwa … vitanyolewa: Ishara ya kuomboleza; taz Isa 15:2-3; Amo 8:10.
19Watatupa fedha yao barabarani
na dhahabu yao itakuwa kama kitu najisi.
Fedha na dhahabu zao hazitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu;
wala hawataweza kushiba
au kuyajaza matumbo yao fedha na dhahabu waliyojirundikia;
kwani mali hiyo ndiyo chanzo cha dhambi yao.
20Kwa kuwa walijifanyia utukufu usio na maana kwa njia ya vikuku,
wakajifanyia sanamu za miungu zinazochukiza
pamoja na vitu vyao vya aibu;
vyote hivyo nitavifanya kuwa najisi kwao.
21Utajiri wao nitautia mikononi mwa mataifa mengine,
watu waovu wa dunia watauteka na kuutia najisi.
22Uso wangu nitaugeuzia mbali nao
ili walitie najisi hekalu langu.#7:22 Hekalu langu: Kiebrania “hazina yangu” msemo ambao waweza kueleweka kama hekalu, Yerusalemu au hata watu wa Israeli wenyewe.
Wanyang'anyi wataingia humo ndani na kulitia najisi.
23Tengeneza mnyororo.#7:23 Tengeneza mnyororo: Mwito huo wa kutengeneza mnyororo unatolewa kwa kuashiria kuchukuliwa mateka siku za usoni maana kwa kawaida wafungwa walifungwa minyororo.
Kwa kuwa nchi imejaa makosa ya jinai ya umwagaji damu
na mji umejaa dhuluma kupindukia,
24nitayaleta mataifa mabaya sana
nao watazimiliki nyumba zao. Kiburi chao nitakikomesha,
na mahali pao pa ibada patatiwa unajisi.
25Uchungu mkali utakapowajia,
watatafuta amani, lakini haitapatikana.
26Watapata maafa mfululizo;
nazo habari mbaya zitafuatana.
Watamwomba nabii maono.
Makuhani hawatakuwa na sheria yoyote;
na wazee watakosa shauri la kuwapatia.
27Mfalme#7:27 Mfalme: Kihebrania “mfalme na mwana mfalme” labda kama rejeo kwa Yehoyakini na Sedekia. ataomboleza,
mkuu atakata tamaa
na watu watatetemeka kwa hofu.
Nitawatenda kadiri ya mienendo yao,
nitawahukumu kama nilivyowahukumu wengine.
Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza