1
1Kauli ya Mungu aliyoiona nabii Habakuki.
Lalamiko la nabii#1:2-4 Aya hizi ziko katika mtindo wa maandishi ya maombolezo. Zinaeleza wasiwasi wa nabii kuhusu uvumilivu wa Mwenyezi-Mungu kwa watu waovu (rejea Yobu 19:1-7; 21; Zab 73:1-14; Yer 12:1-4; Ufu 6:10). Habakuki anajizuia kukubali kwamba Wakaldayo (taz Yer 1:14-15 maelezo) ambao walikuwa wakandamizaji wa Waisraeli, ni chombo cha ghadhabu ya Mungu (rejea Isa 10:5).
2“Ee Mwenyezi-Mungu, nitakulilia mpaka lini,
nawe usinisikilize na kunisaidia?
Kwa nini nalia: ‘Dhuluma’
nawe hutuokoi?
3Kwa nini wanifanya nishuhudie mabaya na taabu?
Uharibifu na ukatili vinanizunguka,
ugomvi na mashindano yanazuka.
4Hivyo sheria haina nguvu,
wala haki haitekelezwi.
Waovu wanawazunguka waadilifu,
hivyo hukumu hutolewa ikiwa imepotoshwa.”
Jibu la Mungu#1:5-11 Aya hizi zina jibu la Mungu kwa masuala machungu aliyouliza nabii.
5Mungu akasema:
“Yaangalie mataifa, uone!
Utastaajabu na kushangaa.
Maana ninatenda kitu ukiwa bado unaishi,
kitu ambacho ungeambiwa hungesadiki.#1:5 Taz Mate 13:41 ambapo imekaririwa lakini kulingana na makala ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX).
6Maana ninawachochea Wakaldayo,#1:6 Wakaldayo: Utawala wa wakaldayo ulichukuliwa na Waisraeli kuwa ni mfano wa ukatili na maangamizi. Rejea 2Fal 24:2; Yer 6:22-23; 10:22.
taifa lile kali na lenye hamaki!
Taifa lipitalo katika nchi yote,
ili kunyakua makao ya watu wengine.
7Wao ni watu wa kuchukiza na kutisha;
wao hujiamulia wenyewe nini haki na adhama.
8“Farasi wao ni wepesi kuliko chui;
wakali kuliko mbwamwitu wenye njaa.
Wapandafarasi wao wanatoka mbali,
wanaruka kasi kama tai arukiavyo mawindo.
9“Wote wanakuja kufanya ukatili;
kwa nyuso kakamavu wanasonga mbele,
wanakusanya mateka wengi kama mchanga.
10Wanawadhihaki wafalme,
na kuwadharau watawala.
Kila ngome kwao ni mzaha,
wanairundikia udongo na kuiteka.
11Kisha wanasonga mbele kama upepo,
wafanya makosa na kuwa na hatia,
maana, nguvu zao ndizo mungu wao!”
Habakuki analalamika tena
12“Je, wewe si ndiwe Mwenyezi-Mungu,
tangu kale na kale?
Wewe ndiwe Mungu wangu, Mtakatifu wangu, usiyekufa#1:12 Usiyekufa: Tafsiri kulingana na mapokeo ya kale. Kiebrania: “hatutakufa”.
Ee Mwenyezi-Mungu, umewateua Wakaldayo watuhukumu;
Ewe Mwamba, umewaimarisha ili watuadhibu!
13Wewe ni mtakatifu kabisa, huwezi kutazama uovu,
huwezi kustahimili kamwe kuona mabaya.
Mbona basi wawaona wafanya maovu na kunyamaza,
kwa nini unanyamaza waovu wanapowamaliza
wale watu walio waadilifu kuliko wao?#1:13 Kwa mara nyingine tena (taz 1:2-4) nabii anauliza juu ya matendo ya Mungu mwenyewe ambayo hayawezi kueleweka.
14“Umewafanya watu kama samaki baharini,
kama viumbe vitambaavyo visivyo na kiongozi!
15Wakaldayo huwavua watu kwa ndoana,
huwavutia nje kwa wavu wao,
huwakusanya wote katika jarife lao,
kisha hufurahi na kushangilia.
16Kwa hiyo, wanazitambikia nyavu zao,
na kuzifukizia ubani;
maana kwa hizo huweza kuishi kwa anasa,
na kula chakula cha fahari.
17“Je, hawataacha kamwe kuvuta upinde wao?#1:17 Upinde wao: Tafsiri kulingana na hati ya Kumrani ya Habakuki. Kiebrania: “wavu”.
Je, wataendelea tu kuwanasa watu,
na kuyaangamiza mataifa bila huruma?