13
Jinsi ya kumpendeza Mungu
1Endeleeni kupendana kindugu. 2Msisahau kuwakaribisha wageni; maana kwa kufanya hivyo watu wengine walipata kuwakaribisha malaika#13:2 Kuwakaribisha malaika: Mwa 18:1-8; 19:1-3; tazama Rom 12:13. bila kujua. 3Wakumbukeni wale waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao. Wakumbukeni wale wanaoteseka kana kwamba nanyi mnateseka kama wao.#13:3 Mat 25:35-46; Rejea Ebr 10:32-34. Wakristo wengi nyakati hizo za mwanzo walipata kufungwa gerezani kwa sababu ya imani yao.
4Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi.
5Msiwe watu wa kupenda fedha;#13:5 Msiwe watu wa kupenda fedha …: 1Tim 6:6-10; rejea pia Fil 4:11. toshekeni na vile vitu mlivyo navyo. Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” 6Ndiyo maana tunathubutu kusema:
“Bwana ndiye msaada wangu,
sitaogopa.
Binadamu atanifanya nini?”
7Wakumbukeni viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu.#13:7 Viongozi wenu waliowatangazieni neno la Mungu: Yamkini yahusu viongozi wa jumuiya za Kikristo ambao wakati wa kuandikwa kwa barua hii walikuwa wamekwisha fariki. Fikirini juu ya mwenendo wao, mkaige imani#13:7 Imani: Neno la Kigiriki linamaanisha pia “uaminifu”. yao. 8Yesu Kristo ni yuleyule jana, leo na milele. 9Msipeperushwe huku na huku kwa mafundisho tofauti ya kigeni. Neema ya Mungu ndiyo inayoimarisha roho zetu na wala si masharti juu ya chakula; masharti hayo hayakumsaidia kamwe mtu yeyote aliyeyafuata.
10Sisi tunayo madhabahu#13:10 Madhabahu: Neno linalotumiwa hapa kwa mfano wa kifo cha Kristo kama tambiko au kafara ya kuwaondolea watu dhambi (aya 12). ambayo wale wanaotumikia bado katika hema la Wayahudi hawana haki ya kula vitu vyake. 11Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.#13:11-12 Rejea Lawi 16. Katika ibada ya upatanisho ambayo iliadhimishwa kila mwaka, haikuruhusiwa kula sehemu zilizobaki za wanyama waliotolewa kuwa tambiko ya kuondoa dhambi; badala yake, mabaki hayo yaliteketezwa nje ya kambi au nje ya mahali patakatifu kusudi watu wasitiwe najisi (rejea Hes 5:1-4). Ilifanyika hivyo kwa sababu dhambi za watu zilikuwa zimekwisha chukuliwa na kuwekwa katika kafara hizo za kuondoa dhambi (Lawi 16:27; taz Ebr 9:7). Mwandishi wa barua hii kwa Waebrania anachukua ibada hiyo na kuifanya kuwa kielelezo cha tukio hilo maalumu la kifo cha Yesu Kristo nje ya mji wa Yerusalemu (neno kwa neno: nje ya mlango au nje ya kuta), kifo ambacho ni sadaka au tambiko ya kuondoa dhambi za watu. Rejea Yoh 19:7-20 na sehemu sambamba za Injili. 12Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji. 13Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake. 14Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja. 15Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake. 16Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu.
17Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu.
18Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima. 19Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.
Sala
20Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo#13:20 Mchungaji Mkuu wa kondoo: Rejea Isa 40:11; Eze 34; Luka 15:4-7; Yoh 10:1-16; 1Pet 5:4. kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele.#13:20 Damu …iliyothibitisha agano la milele: Tazama Ebr 9:20. 21Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.
Maneno ya mwisho
22Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni. 23Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo#13:23 Timotheo: Taz Mate 16:1 maelezo. amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu.
24Wasalimuni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni. 25Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.#13:25 Hati nyingine za kale zinamalizia aya hii ya mwisho kwa neno: “Amina”.