Waebrania 2
BHNTLK

Waebrania 2

2
Wokovu mkuu
1Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia kwa makini yote tuliyosikia,#2:1 Yote tuliyosikia: Yaani, Habari Njema juu ya Yesu Kristo (aya 3; rejea 1Kor 11:23; 15:1-2). tusije tukayakosa. 2Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika#2:2 Waliopewa …na malaika: Taz Mate 7:53 maelezo na rejea Gal 3:19. ulioneshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili.#2:2 Aliadhibiwa kama alivyostahili: Rejea Ebr 3:16-19; 10:28,30-31. 3Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu,#2:3 Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu: Taz Marko 1:14-15 na sambamba zake. na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli. 4Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.
Mkurugenzi wa wokovu
5Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake. 6Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko:
“Mtu ni nini, hata umfikirie;
mwanadamu ni nini hata umjali?#2:6-8 Zab 8:4-7. Aya hizi za Zaburi hii ya nane zinahusu ukuu wa binadamu miongoni mwa viumbe; lakini sasa, katika A.J., aya hizo zinatumiwa kwa Yesu Kristo ambaye ndiye mkuu juu ya viumbe vyote.
7Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika;
umemvika taji ya utukufu na heshima,
8ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.”
Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa. 9Lakini twamwona Yesu ambaye alifanywa kwa kitambo kidogo kuwa chini kuliko malaika, ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote.#2:9 Ili kwa neema ya Mungu afe kwa ajili ya watu wote: Mat 20:28; Marko 10:45; Efe 1:7; Fil 2:6-11; 1Tim 2:6; Tito 2:14; Ebr 12:2 Sasa tunamwona ametawazwa kwa utukufu na heshima kwa sababu ya kifo alichoteseka. 10Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa#2:10 Alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa: Wazo hili linatiliwa mkazo katika Ebr 5:8-10; 7:19,28; 9:9; 10:1,14; 11:40; 12:23. kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu.
11Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake; 12kama asemavyo:
“Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako.
Nitakusifu katika kusanyiko lao.”#2:12 Zab 22:22. Zaburi hii yote ilifikiriwa kuwa inamhusu Masiha.
13Tena asema:
“Nitamwekea Mungu tumaini langu.”
Na tena:
“Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.”#2:13 Nukuu hizi zimetolewa kutoka Isa 8:17-18 na zinatumiwa kumhusu Yesu.
14Basi, kwa vile watoto hao, kama awaitavyo, ni watu wenye mwili na damu, Yesu mwenyewe akawa kama wao na kushiriki ubinadamu wao. Alifanya hivyo ili, kwa njia ya kifo chake, amwangamize Ibilisi ambaye ana mamlaka juu ya kifo, 15na hivyo awaokoe wale waliokuwa watumwa maisha yao yote kwa sababu ya hofu yao ya kifo. 16Maana ni wazi kwamba yeye hakuja kuwasaidia malaika, bali kama yasemavyo Maandiko: “Anawasaidia wazawa wa Abrahamu.” 17Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake kwa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe.#2:17 Yesu Kristo anasemwa hapa kuwa ni Kuhani mwenye kutimiza kikamilifu huduma yake: kujitoa yeye mwenyewe tambiko na hivyo kusababisha watu wasamehewe dhambi; (ling Ebr 1:3). Hili ni wazo kuu na la kipekee la barua hii hasa katika Ebr 4:14—5:10; 6:20—10:18. 18Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza