2
1Basi, waiteni kaka zenu, “Watu wangu,” na dada zenu, “Waliohurumiwa.”#2:1 Watu wangu …Waliohurumiwa: Majina haya ni kinyume cha yale yaliyotangulia ambayo yalitamka kukataliwa kwa Waisraeli kama watu wa Mungu (1:6,8-9). Kiebrania majina haya ni “Ami” na “Ruhama”.
Mke mzinzi — taifa potovu la Israeli
2Mlaumuni mama yenu#2:2 Mlaumuni mama yenu: Hapa inaonekana kwamba watu wa Israeli (mama yenu) wako hukumuni mbele ya Mungu. Lakini kesi hiyo ni ya kupata upatanisho au ya kuwavuta wamrudie Mungu. mlaumuni,
maana sasa yeye si mke wangu
wala mimi si mume wake.
Mlaumuni aondokane na uasherati wake,
ajiepushe na uzinzi wake.
3La sivyo, nitamvua nguo abaki uchi,#2:3 Nitamvua nguo abaki uchi …: Hapa tena nabii anatumia lugha ya mfano. Dhambi ya Waisraeli ni lazima ionekane hadharani na hivyo kama aya iliyotangulia walau waweze kumrudia Mungu (Eze 16:36-39; Nah 3:5; Ufu 17:16).
nitamfanya awe kama alivyozaliwa.
Nitamfanya awe kama jangwa,
nitamweka akauke kama nchi kavu.
Nitamuua kwa kiu.
4Na watoto wake sitawahurumia,
maana ni watoto wa uzinzi.#2:4-5 Watoto wa uzinzi …mama yao amefanya uzinzi: Hawa watoto wanaitwa hivyo kinyume cha “watoto wa Mungu aliye hai” katika 1:10. “wapenzi wangu”: fungu la maneno ambayo yanadokezea miungu ya Kanaani ya rutuba, hasa mungu Baali (2:8,13).
5Mama yao amefanya uzinzi,
aliyewachukua mimba amefanya mambo ya aibu.
Alisema; “Nitaambatana na wapenzi wangu,
ambao hunipa chakula na maji,
sufu na kitani, mafuta na divai.”
6Basi, nitaiziba njia yake kwa miiba,
nitamzungushia ukuta,
asipate njia ya kutokea nje.
7Atawafuata wapenzi wake,
lakini hatawapata;
naam, atawatafuta,
lakini hatawaona.
Hapo ndipo atakaposema,
“Nitarudi kwa mume wangu wa kwanza;
maana hapo kwanza nilikuwa nafuu kuliko sasa.”
8Hakujua kwamba ni mimi
niliyempa nafaka, divai na mafuta,
niliyemjalia fedha na dhahabu kwa wingi,
ambazo alimpelekea Baali.
9Kwa hiyo wakati wa mavuno nitaichukua nafaka yangu,
nitaiondoa divai yangu wakati wake.
Nitamnyang'anya nguo zangu za sufu na kitani,
ambazo zilitumika kuufunika uchi wake.
10Nitamvua abaki uchi mbele ya wapenzi wake,
wala hakuna mtu atakayeweza kunizuia.
11Nitazikomesha starehe zake zote,
sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato,#2:11 Sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato: Sikukuu ya mwezi mwandamo ilifanyika kila siku ya kwanza kabisa mwezi mpya ulipoonekana (Kut 20:8-11; 23:14-17; Hes 28:11-15). Sikukuu hizo hazikukubalika tena kwa sababu zilikuwa zinachanganyikana na ibada kwa Baali.
na sikukuu zote zilizoamriwa.
12Nitaiharibu mizabibu yake na mitini,
anayosema ni malipo kutoka kwa wapenzi wake.
Nitaifanya iwe misitu,
nao wanyama wa porini wataila.
13Nitamlipiza sikukuu za Baali alizoadhimisha,
muda alioutumia kuwafukizia ubani,#2:13 Kuwafukizia ubani: Ubani au uvumba ulitengenezwa kutoka utomvu wenye harufu nzuri wa mti fulani na kuchomwa juu ya mahali pa kutambikia au madhabahu hekaluni.
akajipamba kwa pete zake na johari,
na kuwaendea wapenzi wake,
akanisahau mimi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nasema.
Upendo wa Mwenyezi-Mungu kwa watu wake
14Kwa hiyo, nitamshawishi,
nitampeleka jangwani#2:14 Nitampeleka jangwani: Wafafanuzi wengine wanafikiri matumizi ya “jangwani” yanakumbusha makazi ya Waisraeli huko walipotoka Misri na hawakuwa wamejifunza kuabudu Baali. Lakini inaonekana kwamba “jangwani” hapa panapaswa kuchukuliwa kama mahali pa majaribio ambapo Waisraeli watajifunza kumrudia Mwenyezi-Mungu, waweze mwishowe kumwita Mungu kuwa Bwana wao na sio Baali (aya 16).
na kusema naye kwa upole.
15Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu,
bonde la Akori#2:15 Bonde la Akori: Jina “Akori” Kiebrania maana yake ni “taabu”, kwa hiyo tafsiri nyingine ni “Bonde la Taabu”. Mahali penyewe hapajulikani kwa uhakika lakini Akani alifanya kosa lake hapo na kufia huko (Yos 7:24-26; 15:7). Mahali hapo sasa patarekebishwa kuwa mfano wa tumaini. nitalifanya lango la tumaini.
Atanifuata kwa hiari kama alipokuwa kijana,
kama wakati alipotoka katika nchi ya Misri.
16“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku hiyo, wewe utaniita ‘Mume wangu,’ na sio tena ‘Baali wangu.’#2:16 Utaniita ‘mume wangu’ … sio… ‘Baali wangu’: Katika utamaduni wa Waisraeli mwanamume licha ya kuwa na mke wake ambaye alimwita ‘mumewe’ aliweza pia kuwa na mke au wake wengine (suria) ambao ingawa walichukuliwa kuwa wake zake hawakuwa na haki kamili za mke wa kwanza na hao walimwita yeye ‘bwana wao’. Ndiyo maana nabii anachezea maneno hayo mawili akichukua uhusiano wa Waisraeli na Baali kuwa kama uhusiano wa suria na bwana wake na sio uhusiano wa mume na mkewe. Nabii kwa kusema hivyo anaonesha umuhimu wa kukata uhusiano na miungu ya uongo (hapa Baali). 17Maana, nitalifanya jina la Baali lisitamkike tena kinywani mwako. 18Nitafanya agano na wanyama wa porini,#2:18 Nitafanya agano na wanyama wa porini: Kurekebishwa kwa Israeli kutajumuisha mkataba na wanyama (taz Isa 11:6-9) na amani kamili ya kudumu (taz Isa 2:4). Mawazo haya yanafanana kiasi fulani na mambo yanayosemwa kuhusu utawala wa baadaye wa Masiha. Rejea Isa 9:5-6; 65:25; Zek 9:9-10. ndege wa angani pamoja na vyote vitambaavyo, wasikuumize. Nitatokomeza upinde, upanga na silaha za vita katika nchi, na kukufanya uishi kwa usalama. 19Nitakufanya mke wangu milele; uwe wangu kwa uaminifu na haki, kwa fadhili na huruma. 20Naam, nitakuposa kwa uaminifu, nawe utanijua mimi Mwenyezi-Mungu.
21“Siku hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema,
nitaikubali haja ya mbingu ya kunyesha mvua,
mbingu nazo zitaikubali haja ya ardhi.
22Ardhi itaikubali haja ya nafaka, divai na mafuta,
navyo vitatosheleza mahitaji ya Yezreeli.#2:22 Yezreeli: Taz 1:4 maelezo.
23Nitamwotesha Yezreeli katika nchi;
nitamhurumia ‘Asiyehurumiwa’,
na wale walioitwa ‘Siwangu’,
nitawaambia, ‘Nyinyi ni watu wangu.’
Nao watasema, ‘Wewe ni Mungu wetu.’”