3
Hosea na mwanamke mzinzi
1Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Nenda tena ukampende mwanamke anayependwa na mwanamume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama mimi Mwenyezi-Mungu ninavyowapenda Waisraeli, ingawa wao wanaigeukia miungu mingine na kuwa na uchu wa maandazi ya zabibu kavu.”#3:1 Uchu wa maandazi ya zabibu kavu: Hayo maandazi yaliliwa katika taratibu za tambiko kwa miungu (taz Yer 7:18).
2Basi, nikamnunua huyo mwanamke#3:2 Nikamnunua huyo mwanamke: Maneno hayo yanaweza kumaanisha kwamba mwanamke huyo alikuwa mtumwa wa mtu fulani au mtumwa wa uzinzi katika hekalu la miungu. kwa vipande kumi na vitano vya fedha na magunia mengi ya shayiri. 3Kisha nikamwambia, “Lazima uwe wangu kwa siku nyingi bila kufanya uzinzi au kuwa mke wa mtu mwingine; nami pia nitakuwa mwaminifu.”#3:3 Masharti anayowekewa yana shabaha ya kuondoa ile hali ya uzinzi na hivyo kumrudisha katika hali ya uaminifu tena. Kwa namna hiyo Waisraeli wanaweza kumrudia Mungu tena. 4Hivyo ndivyo Waisraeli watakavyokuwa: watakaa kwa muda mrefu bila mfalme au mkuu; bila tambiko, wala mnara wala kizibao cha kifuani wala kinyago.#3:4 Aya hii inatoa maana ya vitendo hivyo vya ishara vilivyotajwa katika aya iliyotangulia kwa watu wa Israeli. Watakaa bila mfalme, bila tambiko na bila mnara … Katika aya hii hatua za adhabu ni wazi na lengo lake ni kurekebishwa kwa watu wa Israeli (aya ya 5). 5Baadaye, Waisraeli watarudi na kumtafuta Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, na kumtafuta mfalme wao, mzawa wa Daudi. Ndipo watakapomcha Mwenyezi-Mungu, na kutazamia wema wake siku za mwisho.