Hosea 4
BHNTLK

Hosea 4

4
Mungu awalaumu watu wake#4:1-3 Aya hizi zinatangulia sehemu ya pili ya kitabu cha Hosea na zinataja mambo ya msingi kabisa ambayo yanalaumiwa na Mungu. Orodha hiyo ya makosa inaongozwa na mambo mawili makuu: ukosefu wa uaminifu na kutomjua Mungu.
1Msikilizeni Mwenyezi-Mungu,
enyi Waisraeli.
Mwenyezi-Mungu anawashutumu wakazi wa nchi hii.
“Hamna tena uaminifu wala wema nchini;
hamna anayemjua Mungu katika nchi hii.
2Kuapa, uongo, mauaji, wizi na uzinzi huzuka humo.
Umwagaji damu hufuatana mfululizo.#4:2 Makosa yote yanayotajwa hapa yanahusu vitendo visivyokubalika dhidi ya jirani: kuapa (dhidi ya jirani) labda kwa kutumia jina la Mungu, uongo (kumdanganya jirani) taz pia 7:3; 10:13; 12:1, mauaji ya mtu (taz 6:9) kwa makusudi, kuiba (mali ya jirani au pia kuiba mtu yaani kumteka mtu nyara), na uzinzi (4:13-14).
3Kwa hiyo, nchi yote ni kame,
wakazi wake wote wanaangamia
pamoja na wanyama wa porini na ndege;
hata samaki wa baharini wanaangamizwa.#4:3 Dhambi za watu zinasababisha uharibifu katika maumbile (Yer 12:4; 23:10; Isa 24:4-6; Rom 8:19-22).
Mungu anawashutumu makuhani#4:4-10 Makuhani kama viongozi wa dini wanatajwa hapa moja kwa moja kwa vile wao hasa ndio wangepaswa kuwafundisha watu kushika sheria ya Mungu. Matumizi ya umoja hapa (kuhani) yanapaswa kueleweka kama kama umoja unaowakilisha makuhani wote.
4“Lakini watu wasilaumiwe, wasishutumiwe;
maana mimi nakushutumu wewe kuhani.
5Wewe utajikwaa mchana,
naye nabii atajikwaa pamoja nawe usiku.
Nitamwangamiza mama yako Israeli.#4:5 Mama yako Israeli: Katika Kiebrania kuna neno “mama” peke yake na wafafanuzi wengi wanafikiri linatumiwa hapa kwa maana ya taifa la Israeli au watu wote wa Israeli. Taz 2:2 ambapo picha ya “mama” inawakilisha watu wote wa Israeli.
6Watu wangu wameangamia kwa kutonijua,
maana wewe kuhani umekataa mafundisho.
Nimekukataa kuwa kuhani wangu.
Kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako,
nami pia nitawasahau watoto wako.
7“Kadiri makuhani walivyoongezeka,
ndivyo wote walivyozidi kuniasi.
Basi, nitaigeuza fahari yao kuwa aibu.
8Wanajishibisha kwa sadaka za watu wangu wenye dhambi.
Wana hamu sana ya kuwaona wametenda dhambi.
9Lakini yatakayowapata watu yatawapata makuhani;
nitawaadhibu kwa sababu ya mwenendo wao,
nitawalipiza matendo yao wenyewe.
10Watakula, lakini hawatashiba;
watazini, lakini hawatapata watoto,
kwa sababu wameniacha mimi Mwenyezi-Mungu,
na kufuata miungu mingine.
Mungu alaani ibada za miungu
11“Divai mpya na ya zamani
huondoa maarifa.
12Watu wangu huomba shauri kutoka kwa mti;#4:12 huomba shauri kutoka kwa mti: Nabii hapa anatumia lugha ya dhihaka kudhihaki mungu wa uongo “mti” na “kijiti”. Neno “mti” hapa laweza kuwa linatumiwa kutaja kinyago cha mungu kama katika Kumb 4:28. Lakini hapa huenda ni mti wa kweli ambao uliwakilisha mungu wa kike Ashera ambaye alikuwa mke wa mungu Baali. Na hicho “kijiti” kilitumiwa kujaribu kujua matakwa ya Mungu.
kijiti chao cha ramli ndicho kinachowapa kauli.
Nia ya kufanya uzinzi imewapotosha;
wamefanya uzinzi kwa kufuata miungu mingine,
wakaniacha mimi Mungu wao.
13Wanatambikia kwenye vilele vya milima;
naam, wanatoa tambiko vilimani,
chini ya mialoni, migude na mikwaju,
maana kivuli chao ni kizuri.
“Kwa hiyo binti zenu hufanya uzinzi,
na bibiarusi wenu hufanya uasherati.
14Lakini sitawaadhibu binti zenu wanapofanya uzinzi,#4:14 binti zenu wanapofanya uzinzi: Neno la Kiebrania la uzinzi ni “zenah”. Ndiyo kusema, neno letu la Kiswahili la “mzinzi” limetufikia katika msamiati wetu kutokana na lugha ya awali ya dhambi hiyo, labda kwa kupitia Kiarabu.
wala bibi arusi wenu wanapofanya uasherati,
maana, wanaume wenyewe ndio wanaofuatana na wazinzi,
na kutambikia pamoja nao katika ibada za uzinzi.
Watu hawa watovu wa akili hakika wataangamia!
15“Ama kweli nyinyi Waisraeli ni wazinzi!
Lakini, msiwafanye watu wa Yuda wawe na hatia!
Msiende mahali patakatifu huko Gilgali,#4:15 Gilgali: Gilgali ulikuwa mahali maarufu pa ibada karibu na Yeriko (Taz Yos 4:19-20)
wala msiende kule Beth-aveni.#4:15 Beth-aveni: Neno kwa neno: “Nyumba ya uovu.” Hosea anatumia jina hilo la dharau kwa Betheli, jina ambalo katika Kiebrania lina maana ya “Nyumba ya Mungu” na mji huo ulikuwa ni mahali pa ibada maarufu kwa Israeli (1Fal 12:28-30). Taz pia Hos 5:8; 10:5; Amo 4:4; 5:5.
Wala msiape mkisema,
‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo!’”
16Waisraeli ni wakaidi kama punda.
Kwa nini basi Mungu ashughulike kuwachunga,
kama kondoo kwenye malisho mapana?
17“Watu wa Efraimu#4:17 Efraimu: Taz Yos 16:4-10. Kabila la Waisraeli lililokuwa kaskazini. Walikugeuka wakaabudu sanamu ya ndama wa dhahabu. (Taz 8:5, 13:2; 1Fal 12:28). Mungu wa Baali (Hos 2:8,13). wamejifunga na sanamu.
Haya! Waache waendelee tu!#4:17 Haya! Waache waendelee tu: Taz 4:16, wamezama kuabudu sanamu kiasi ambacho hawasikii kitu chochote, hivyo niafadhali kutowaambia kabisa. “Sikio la kufa halisikii dawa.” Taz pia Ufu 22:11 ling Hos 11:8. Wanalinganishwa na mkate usiogeuzwa (7:8), njiwa mjinga 8:11-13. Ling Isa 28:7-8 pia 2Sam 16:11; 2Fal 23:8.
18 # 4:18 Aya hii katika makala ya Kiebrania si dhahiri. Kama vile genge la walevi,#4:18 Genge la walevi: Au, “Kundi la walevi”.
wanajitosa wenyewe katika uzinzi;
wanapendelea aibu kuliko heshima yao.#4:18 Wanapendelea aibu kuliko heshima yao: Israeli wakiwa taifa teule la Mungu wamemuacha na kumkimbilia Baali. Kama alivyo Gomeri, kumuacha Hosea mumewe na kukimbilia wanaume wengine. Wamekuwa vipofu wa maadili. Taz 12:17.
19Basi, kimbunga kitawapeperusha,#4:19 Kimbunga kitawapeperusha: Taz Zab 18:10; 104:3; Jer 4:11-12. Huonesha hali ya ugomvi utakaoletwa na mashujaa watakaoiteka Israeli. Hatimaye wapate kutambua miungu waliyoifuata haina uwezo wowote. Taz Hos 10:6. Ling aya ya 16.
na watayaonea aibu matambiko yao#4:19 Watazionea aibu dhambi zao: Tafsiri nyingine, “watahayari kwa sababu ya tambiko zao.” Taz 6:6; ling Meth 21:3; Mat 12:27; Zab 50:8; Yoh 17:3; Mika 6:6-8. kwa miungu ya uongo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza