5
Wimbo wa Debora#5:1-31 Utenzi huu ni wa kale na unafanana kwa muundo wake na tenzi za kale za ushindi zilizoimbwa nyakati hizo huko Misri na Ashuru na inafikiriwa kwamba utenzi huo ni wa wakati huo wa Debora na Baraki, yapata mwaka 1200 K.K. Utenzi wenyewe ni mgumu kuufuata na pengine si dhahiri lakini ni utenzi wa ajabu wa nyakati za kale.
1Siku hiyo, Debora na Baraki, mwana wa Abinoamu, wakaimba wimbo huu:
2“Viongozi walijitokeza kuongoza Israeli,
watu walijitolea kwa hiari yao.
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu!
3“Sikilizeni, enyi wafalme!
Tegeni sikio, enyi wakuu!
Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
4“Ee Mwenyezi-Mungu, ulipotoka huko Seiri,#5:4 Seiri: Jina lingine la Edomu ambalo lahusu sehemu ya vilima kusini mwa Bahari ya Chumvi.
ulipoteremka mlimani Edomu,
nchi ilitetemeka,
mbingu zilidondosha maji,
naam, mawingu yakaiangusha mvua.
5Milima ilitikisika mbele yako Mwenyezi-Mungu,
naam, mlima Sinai mbele yako Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
6“Katika siku za Shamgari,#5:6 Shamgari: Taz Amu 3:31. mwana wa Anathi,
katika wakati wa Yaeli,
misafara ilikoma kupita nchini,
wasafiri walipitia vichochoroni.
7Wakulima walikoma kuwako,
walikoma kuwako katika Israeli,
mpaka nilipotokea mimi Debora,
mimi niliye kama mama wa Israeli.#5:7 Mimi niliye kama mama wa Israeli: Katika Isa 66:10-13 picha hii unatumika juu ya Mungu ambaye anawatunza Waisraeli; taz pia picha hiyohiyo katika Mat 23:37.
8Walijichagulia miungu mipya,
kukawa na vita katika nchi.
Lakini hakukupatikana mwenye upanga au ngao
kati ya watu 40,000 wa Israeli.
9Nawapa heshima makamanda wa Israeli
waliojitoa kwa hiari yao kati ya watu.
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu!
10“Tangazeni, enyi wapandapunda#5:10 Wapandapunda: Au wapandanyumbu. “Punda” au “nyumbu” walikuwa wanyama ambao wakuu kama vile wafalme waliwatumia kupanda badala ya farasi (taz 2Sam 13:29 maelezo). weupe,
enyi mnaokalia mazulia ya fahari,
nyinyi mnaotembea njiani, tangazeni jambo hilo.
11Imbeni kupita wanamuziki kwenye visima vya maji,
tangazeni ushindi wa Mwenyezi-Mungu,
ushindi kwa wakulima wake katika Israeli.
Ndipo watu wa Mwenyezi-Mungu waliposhuka malangoni.#5:11 Inaonekana kutoka aya hii kwamba yahusu maandamano kama yale ya Zab 68:24-27.
12“Amka, amka, Debora!
Amka! Amka uimbe wimbo!
Amka, Baraki mwana wa Abinoamu,
uwachukue mateka wako.
13Mashujaa waliobaki waliteremka,
watu wa Mwenyezi-Mungu walikwenda kumpigania
dhidi ya wenye nguvu.
14 # 5:14 Kuanzia hapa mwandishi anawasifu watu wa makabila yaliyoitikia wito wa Debora wa kujiunga naye (aya 14:15a); hali makabila mengine ambayo hayakuitikia wito huo au hayakuutilia maanani yanakosolewa (aya 15-17). Kutoka Efraimu waliteremka bondeni,#5:14 Bondeni: Makala ya Kiebrania yanasema “katika Maaleki”.
wakafuata ndugu zao watu wa Benyamini;
kutoka Makiri#5:14 Makiri: Hapa jina “Makiri” linahusu kabila la Manase. Makiri alikuwa mtoto wa kwanza wa kiume wa Manase. Taz Yos 13:31 na pia Hes 32:39-40. walishuka makamanda,
kutoka Zebuluni maofisa wakuu.
15Wakuu wa Isakari wakafuatana na Debora,
watu wa Isakari waaminifu kwa Baraki;
wakamfuata mbio mpaka bondeni.
Lakini miongoni mwa koo za Reubeni
kulikuwamo kusitasita kwingi.
16Kwa nini walibaki mazizini?
Ili kusikiliza milio ya kondoo?
Miongoni mwa koo za Reubeni
kulikuwamo kusitasita kwingi.
17Kabila la Gileadi lilibaki ng'ambo ya Yordani.
Kabila la Dani, kwa nini mlibaki merikebuni?
Kabila la Asheri lilitulia huko pwani ya bahari,
lilikaa bandarini mwake.#5:16-17 Kuhusu makabila haya taz Kumb 2:36 na Yos 13:15; 19:24,40.
18Watu wa Zebuluni ni watu
waliohatarisha maisha yao katika kifo.
Hata wa Naftali walikikabili kifo
kwenye miinuko ya mashamba.
19“Huko Taanaki, kando ya chemchemi za Megido,#5:19 Taanaki …Megido: Megido ulikuwa mahali palipofanyika mapambano makubwa ya mara kwa mara kupita mahali pengine pote katika Palestina kwani ulikuwa mahali ambapo njia kuu ilitenga milima ya Galilaya na ile ya Efraimu.
wafalme walikuja, wakapigana;
wafalme wa Kanaani walipigana,
lakini hawakupata nyara za fedha.
20Nyota kutoka mbinguni zilishiriki vita,
zilifuata njia zao, zilipigana na Sisera.
21Mafuriko ya mto Kishoni yaliwachukua mbali,
naam, mafuriko makali ya mto Kishoni.
Songa mbele kwa nguvu, ee nafsi yangu!#5:20-21 Nyota …mafuriko ya mto: Itakumbukwa kwamba hapo kale mara nyingine nyota (na mwezi na jua) zilifikiriwa kuwa ni viumbe hai wasio wa ulimwengu huu. Utenzi wenyewe hapa unatupa picha kwamba mbingu za juu na maji ya chini ya nchi vinashirikiana na Mungu kwa faida ya Waisraeli. Taz pia Yos 10:12-14.
22“Farasi walipita wakipiga shoti;,
walikwenda shoti na kishindo cha kwato zao.
23Malaika wa Mwenyezi-Mungu asema hivi:
‘Uapizeni mji wa Merosi,
waapizeni vikali wakazi wake;
maana hawakuja kumsaidia Mwenyezi-Mungu
hawakumsaidia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wenye nguvu’.
24“Abarikiwe kuliko wanawake wote
Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni.
Naam, amebarikiwa kuliko wanawake wote
wanaokaa mahemani.
25Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa;
alimletea siagi katika bakuli ya heshima.
26Kwa mkono mmoja alishika kigingi cha hema,
na kwa mkono wake wa kulia nyundo ya fundi;
alimponda Sisera kichwa,
alivunja na kupasuapasua paji lake.
27Sisera aliinama, akaanguka;
alilala kimya miguuni pake.
Hapo alipoinama ndipo alipoanguka, amekufa!#5:27 Linganisha na 4:21 ambapo Sisera aliuawa akiwa amelala.
28“Mama yake Sisera alitazama dirishani
alichungulia katika viunzi vyake, akalalamika:
‘Kwa nini gari lake limechelewa?
Mbona vishindo vya magari yake vimechelewa kusikika?’
29Jibu akalipata kwa wanawake wenye hekima:
akajituliza tena na tena kwa jibu hilo:
30‘Bila shaka wanatafuta na kugawana nyara;
msichana mmoja au wawili kwa kila askari,
vazi la sufu ya rangi kwa ajili ya Sisera.
Vazi la sufu iliyotariziwa,
na mikufu miwili ya nakshi kwa ajili ya shingo yangu!’
31“Ee Mwenyezi-Mungu, waangamie adui zako wote!
Lakini rafiki zako na wawe kama jua,
wakati linapochomoza kwa mwanga mkubwa!”
Nayo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini.