Yeremia 2
BHNTLK

Yeremia 2

2
Mungu awalinda Waisraeli
1Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: 2“Nenda ukawatangazie waziwazi wakazi wote wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Naukumbuka uaminifu wako ulipokuwa kijana,
jinsi ulivyonipenda kama mchumba wako,#2:2 Naukumbuka uaminifu wako …ulivyonipenda kama mchumba wako: Yeremia, kama vile manabii wengine (hasa Hos 1—3), anatumia mfano wa muungano wa ndoa kudokezea uhusiano kati ya Mungu na watu wake. “Jangwani”: Waisraeli kule jangwani hawakushawishwa sana kuiabudu miungu ya rutuba kiasi kikubwa kama walivyofanya walipoingia nchini Kanaani (rejea Yer 2:7-8). Mtazamo huu lakini hauwiani na hali yenyewe inavyosimuliwa katika vitabu vitano vya kwanza vya Biblia (Kut 17:1-7; 32; Hes 20:1-13) taz pia Ezekieli sura ya 16. Kwa Ezekieli Waisraeli walikosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu tangu kule jangwani (Eze 20:13).
ulivyonifuata jangwani
kwenye nchi ambayo haikupandwa kitu.
3Israeli, wewe ulikuwa mtakatifu kwangu,
ulikuwa matunda ya kwanza ya mavuno yangu.#2:3 Matunda ya kwanza ya mavuno yangu: Matunda ya kwanza ya mavuno yalikuwa yake Mungu peke yake na yaliwekwa wakfu kwa Mungu (Kumb 26:1-11). Kwa hiyo ni Mungu peke yake aliyekuwa na mamlaka ya kuwatumia watu wake kwani aliwateua miongoni mwa mataifa yote wawe waliowekwa wakfu kwa ajili ya utumishi wake Mwenyezi-Mungu (rejea Kumb 7:7-11).
Wote waliokudhuru walikuwa na hatia,
wakapatwa na maafa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Dhambi ya wazee wa Israeli
4Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Yakobo. Sikilizeni enyi jamaa zote za wazawa wa Israeli.
5Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Wazee wenu waliona kosa gani kwangu
hata wakanigeuka na kuniacha,
wakakimbilia miungu duni,
hata nao wakawa watu duni?
6Hawakujiuliza:
‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu aliyetutoa nchini Misri,
aliyetuongoza nyikani
katika nchi ya jangwa na makorongo,
nchi kame na yenye giza nene,
nchi isiyopitiwa na mtu yeyote,
wala kukaliwa na binadamu?’
7Niliwaleta katika nchi yenye rutuba,
muyafurahie mazao yake na mema yake mengine.
Lakini mlipofika tu mliichafua nchi yangu,
mkaifanya chukizo nchi niliyowapa iwe yenu.
8Nao makuhani hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu?’
Wataalamu wa sheria hawakunijua,
viongozi#2:8 Viongozi: Kiebrania “wachungaji”. Aya hii inawakabili hasa wenye mamlaka wa watu: makuhani, viongozi, manabii waliokiuka wito wao wa kutangaza neno sahihi la Mungu (rejea Yer 23:9-40; 28:1-17). “Baali”: taz Amu 2:13 maelezo. wa watu waliniasi;
manabii nao walitabiri kwa jina la Baali
na kuabudu sanamu zisizo na faida yoyote.”
Mashtaka ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya watu wake
9Mwenyezi-Mungu asema,
“Kwa hiyo, mimi nitawalaumu nyinyi,
na nitawalaumu wazawa wenu.
10Haya, vukeni bahari hadi Kupro#2:10 Kupro: Au mwambao wa nchi za Ugiriki na Italia. “Kedari”: Makazi ya mabedui katika jangwa la Siria na Arabia. mkaone,
au tumeni watu huko Kedari wakachunguze,
kama jambo kama hili limewahi kutokea:
11kwamba kuna taifa lililowahi kubadilisha miungu yake
ingawa miungu hiyo si miungu!
Lakini watu wangu wameniacha mimi, utukufu wao,#2:11 Fahari yao: Neno fahari yao hapa ni sawa na neno “utukufu”, neno ambalo latumika kudokezea kuweko kwa Mungu kwa namna ya kuweza kuonekana kwa macho au kusikika katika tukio la kuumba (rejea 20b, 19:1; Isa 6:3), hekaluni (Isa 6:3-4; Eze 10:4) au miongoni mwa watu wake (Kut 40:34-38; Eze 1:27-28). Taz Yoh 1:14 maelezo ya “Akakaa kwetu … utukufu”.
wakafuata miungu isiyofaa kitu.
12Shangaeni enyi mbingu, juu ya jambo hili,
mkastaajabu na kufadhaika kabisa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
13Maana, watu wangu wametenda maovu mawili;
wameniacha mimi niliye chemchemi ya maji ya uhai,#2:13 Maji ya uhai: Rejea Yoh 4:10; 7:37-38. “Visima vyenye nyufa”: Huko Palestina ambamo maji hayapatikani kwa wingi watu walichimba au kutengeneza visima vya kuhifadhi maji (rejea 2Sam 2:13). Mara nyingi maji hayo yalivuja na hata yaliyohifadhiwa hayakuwa safi kama maji yaliyotiririka miferejini.
wakajichimbia visima vyao wenyewe,
visima vyenye nyufa, visivyoweza kuhifadhi maji.
Matokeo ya utovu wa imani ya Israeli
14“Je, Israeli ni mtumwa,#2:14 Mtumwa: Hapo kale mtu aliweza kuwa mtumwa kwa kuuzwa, au kwa kuchukuliwa mateka vitani au kwa kuzaliwa na wazazi walio watumwa. Maana hii ya mwisho ndiyo inayohusika hapa.
ama amezaliwa utumwani?
Mbona basi amekuwa kama mawindo?
15Simba wanamngurumia,#2:15 Simba wanamngurumia: Dokezo ambalo labda lahusu jeshi la Ashuru lilipokuwa linawatishia Waisraeli (rejea 2Fal 16:17—17:6; 18:9—19:37).
wananguruma kwa sauti kubwa.
Nchi yake wameifanya jangwa,
miji yake imekuwa magofu, haina watu.
16Isitoshe, watu wa Memfisi na Tahpanesi,#2:16 Memfisi na Tahpanesi: Miji maarufu ya Misri (rejea Yer 44:1).
wameuvunja utosi wake.
17Israeli, je, hayo yote si umejiletea mwenyewe,
kwa kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
niliyekuwa ninakuongoza njiani?
18Na sasa itakufaa nini kwenda Misri,
kunywa maji ya mto Nili?
Au itakufaa nini kwenda Ashuru,
kunywa maji ya mto Eufrate?#2:18 Kunywa maji …mto Eufrate: Lugha ya mfano au picha yenye madhumuni ya kudokezea ushirikiano wa Waisraeli na tawala kubwa za Ashuru na Misri jambo ambalo Yeremia na manabii wengine waliliona kuwa ishara ya ukosefu wa uaminifu na tegemeo kwa Mwenyezi-Mungu (rejea Isa 30:1-5; Hos 7:11-12).
19Uovu wako utakuadhibu;
na uasi wako utakuhukumu.
Ujue na kutambua kuwa ni vibaya mno
kuniacha mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
na kuondoa uchaji wangu ndani yako.
Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi#2:19 Mwenyezi-Mungu wa majeshi: Jina la sifa la Mungu. Taz 1Sam 1:3 maelezo. nimesema.
Israeli yakataa kumwabudu Mwenyezi-Mungu
20“Tangu zamani wewe ulivunja nira yako,
ukaikatilia mbali minyororo yako,
ukasema, ‘Sitakutumikia’.
Juu ya kila kilima kirefu
na chini ya kila mti wa majani mabichi,
uliinamia miungu ya rutuba kama kahaba.#2:20 Kama kahaba: Katika Biblia kuabudu miungu mingine mara nyingi kulifananishwa na ukahaba (Yer 3:1-4; 5:7; 13:27; Hos 2:5; 4:10-13).
21Lakini mimi nilikupanda kama mzabibu mteule,
mzabibu wenye afya na wa mbegu safi;
mbona basi umeharibika,
ukageuka kuwa mzabibu mwitu?#2:21 Ukageuka kuwa mzabibu mwitu: Rejea Isa 5:1-7; Luka 13:6-9.
22Hata ukijiosha kwa magadi,
na kutumia sabuni nyingi,
madoa ya uovu wako bado yatabaki mbele yangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
23“Unawezaje kusema, ‘Mimi si najisi;
sijawafuata Mabaali?’
Tazama ulivyotenda dhambi kule bondeni;#2:23 Bondeni: Labda dokezo kwa bonde la “Ben-hinomu” karibu na Yerusalemu ambapo ibada za wasiomjua Mungu wa kweli zilifanyika ikiwa pamoja na kuwatambika watoto wachanga. Rejea Yer 7:31-32; 19:5-6.
angalia ulivyofanya huko!
Wewe ni kama mtamba wa ngamia,
akimbiaye huko na huko;#2:23-24 Picha tunayosoma hapa inasemwa kwa maneno mengine katika Hos 2:5; 4:12-14.
24kama pundamwitu aliyezoea jangwani.
Katika tamaa yake hunusanusa upepo;
nani awezaye kuizuia hamu yake?
Amtakaye hana haja ya kujisumbua;
wakati wake ufikapo watampata tu.
25Israeli, usiichakaze miguu yako
wala usilikaushe koo lako.
Lakini wewe wasema: ‘Hakuna tumaini lolote.
Nimeipenda miungu ya kigeni,
hiyo ndiyo nitakayoifuata.’
Israeli astahili kuadhibiwa
26“Kama vile mwizi aonavyo aibu akishikwa,
ndivyo Waisraeli watakavyoona aibu;
wao wenyewe, wafalme wao, wakuu wao,
makuhani wao na manabii wao.
27Hao huuambia mti:#2:27 Mti: Labda yahusu kinyago kilichoashiria Mungu wa kike aitwaye “Ashera”, mamake Baali (taz Amu 2:13 maelezo). “Jiwe”: Mwandishi labda anadokezea nguzo ambazo ziliwakilisha miungu ya rutuba ya Kanaani. ‘Wewe u baba yangu,’
na jiwe: ‘Wewe ndiwe uliyenizaa;’
kwa maana wamenipa kisogo,
wala hawakunielekezea nyuso zao.
Lakini wakati wa shida husema: ‘Inuka utuokoe!’
28“Lakini iko wapi miungu yako uliyojifanyia?
Iinuke basi, kama inaweza kukusaidia,
wakati unapokuwa katika shida.
Ee Yuda, idadi ya miungu yako
ni sawa na idadi ya miji yako!
29Mbona mnanilalamikia?
Nyinyi nyote mmeniasi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
30Niliwaadhibu watu wako bila kufanikiwa,
wao wenyewe walikataa kukosolewa.
Upanga wako uliwamaliza manabii wako
kama simba mwenye uchu.
31Enyi watu! Sikilizeni ninachosema mimi Mwenyezi-Mungu:
Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli
au nchi yenye giza nene?
Kwa nini basi watu wangu waseme:
‘Sisi tu watu huru;
hatutakuja kwako tena!’
32Kijana msichana aweza kusahau mapambo yake
au bibi arusi mavazi yake?
Lakini watu wangu wamenisahau
kwa muda wa siku zisizohesabika.
33Kweli wewe ni bingwa wa kutafuta wapenzi!
Hata wanawake wabaya huwafundisha njia zako.
34Nguo zako zina damu ya maskini wasio na hatia,#2:34 Damu ya maskini wasio na hatia: Mashtaka dhidi ya uvunjaji wa haki katika jamii ni moja ya mambo makuu ya mahubiri ya manabii. Rejea Isa 1:17; Hos 4:1-3; Amo 2:6-8; 4:1; 5:24.
japo hukuwakuta wakivunja nyumba yako.#2:34 Japo hukuwakuta wakivunja nyumba yako: Kipengele kinachodokezea jambo linalotajwa katika Kut 22:2-3 ambapo kitendo cha kumuua mwizi usiku anapofumaniwa wakati huohuo wa wizi hakikulaumiwa (lakini kumuua baadaye ilikatazwa).
“Lakini licha ya hayo yote,
35wewe wasema: ‘Mimi sina hatia;#2:35 Sina hatia: Namna hiyohiyo katika Yer 2:23.
hakika hasira yake imegeuka mbali nami.’
Lakini mimi nitakuhukumu kwa sababu unasema:
‘Sikutenda dhambi.’
36Kwa nini unajirahisisha hivi,
ukibadilibadili mwenendo wako?
Utaaibishwa na Misri,
kama ulivyoaibishwa na Ashuru.
37Na huko pia utatoka,
mikono kichwani kwa aibu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa wale uliowategemea,
wala hutafanikiwa kwa msaada wao.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza