Yeremia 26
BHNTLK

Yeremia 26

26
Yeremia mahakamani#26:1-24 Sura hii ni mojawapo ya sehemu kadhaa za kitabu cha Yeremia ambazo zinatupa fursa ya kujua jinsi Yeremia alivyokabili upinzani mkali kutoka kwa wakuu na hasa manabii wa uongo (rejea k.m. Yer 27—28). Katika sura hii tunapewa mazingira ya mahubiri ya Yeremia kule hekaluni (7:1—8:3) na upinzani mkali uliofuata baada ya kutamka kwamba hilo hekalu litateketezwa (aya 8-9).
1Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia,#26:1 Yehoyakimu mwana wa Yosia: Huyu alitawala badala ya nduguye, Yehoahazi, ambaye aliondolewa madarakani na Farao Neko wa Misri (rejea 2Fal 23:34; 2Nya 36:4). Alitawala mnamo 609-608 K.K. katika nchi ya Yuda, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yeremia hivi: 2“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Simama katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, uwatangazie watu wa miji yote ya Yuda wanaofika kuabudu katika nyumba ya Mungu, mambo yote niliyokuamuru uwaambie, bila kuacha hata neno moja. 3Labda watasikiliza na kuacha njia zao mbaya. Wakifanya hivyo, huenda nikabadili nia yangu kuhusu maafa niliyonuia kuwaletea kwa sababu ya matendo yao maovu.
4“Utawaambia hivi: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Msiponisikiliza na kufuata sheria zangu nilizowawekea, 5na msipoyajali wanayosema watumishi wangu manabii ambao nimekuwa nikiwatuma kwenu kila mara, ingawa hamkuwajali, 6basi, nitaiharibu nyumba hii kama nilivyoharibu ile ya Shilo, na nitaufanya mji huu kuwa laana kwa mataifa yote ya dunia.”
7Makuhani, manabii na watu wote walimsikia Yeremia akisema maneno haya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 8Basi Yeremia alipomaliza kutangaza mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwamuru ayatangaze kwa watu wote, makuhani, manabii na watu wote walimkamata na kusema, “Utakufa! 9Kwa nini umetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu na kusema, nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa, bila wakazi?” Watu wote wakamzingira Yeremia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
10Basi, wakuu wa Yuda waliposikia mambo hayo, walipanda kutoka katika nyumba ya mfalme, wakaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu,#26:10 Walipanda kutoka …nyumba ya mfalme … nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Nyumba hizo mbili zilikuwa zimepakana (rejea 2Fal 11:19) na ilikuwa rahisi kwa wakuu, yaani maofisa wa serikali, kupata habari hiyo bila shida. Rejea Yer 36:10-12. “Wakaketi penye Lango Jipya”: Kitendo hiki kinaashiria kwamba hao wakuu walikusudia kufanya kikao cha mahakama. wakaketi penye Lango Jipya. 11Hapo makuhani na manabii wakawaambia wakuu na watu wote: “Mtu huyu anastahili hukumu ya kifo kwa maana amehubiri dhidi ya mji huu, kama nyinyi wenyewe mlivyosikia kwa masikio yenu.”
12Ndipo Yeremia akawaambia wakuu na watu wote: “Mwenyezi-Mungu alinituma niwatabirie mambo yote mliyosikia nikiyasema dhidi ya hekalu hili na mji huu. 13Sasa basi, rekebisheni mienendo yenu na matendo yenu na kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mkifanya hivyo, Mwenyezi-Mungu atabadili nia yake na kuacha kuwaletea maafa aliyotamka dhidi yenu. 14Lakini mimi, tazama nimo mikononi mwenu. Nitendeeni kama mnavyoona vema na haki. 15Ila jueni kwa hakika kwamba mkiniua, mtakuwa mmejiletea laana nyinyi wenyewe kwa kumwaga damu isiyo na hatia, na kuuletea laana mji huu na wakazi wake. Maana, ni kweli kwamba Mwenyezi-Mungu alinituma niwaambieni mambo hayo muyasikie.”
16Hapo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani na manabii: “Mtu huyu hastahili hukumu ya kifo, kwa kuwa amesema nasi kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” 17Basi, baadhi ya wazee wa nchi wakasimama na kuwaambia watu waliokuwa wamekusanyika: 18“Wakati Hezekia alipokuwa mfalme wa Yuda, Mika wa Moreshethi,#26:18 Mika wa Moreshethi: Huyu nabii, kama vile Yeremia, alihubiri dhidi ya Yerusalemu, viongozi wake wapotovu na manabii waongo (Mika 3:1-12). “Hezekia”: Huyu alikuwa mfalme wa Yuda kati ya mwaka 716 na 687 K.K. (rejea 2Fal 18—20). aliwatangazia watu wote kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi alisema hivi:
‘Mji wa Siyoni utalimwa kama shamba
mji wa Yerusalemu utakuwa magofu,
nao mlima wa hekalu utakuwa msitu.’
19Je, Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda walimuua Mika? La! Badala yake Hezekia alimwogopa Mwenyezi-Mungu na kuomba fadhili zake. Naye Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake ya kuwaletea balaa. Lakini sisi tuko mbioni kujiletea wenyewe maafa.”
20(Kulikuwa na mtu mwingine pia aliyetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo alikuwa anaitwa Uria mwana wa Shemaya,#26:20-23 Uria mwana wa Shemaya: Huyu hatajwi mahali pengine katika Agano la Kale. “Kiriath-yearimu”: taz Yos 9:17 maelezo. “Elnathani”: huyu baadaye, akiwa na wengine (Delaya na Gemaria), alimsihi mfalme Yehoyakimu asichome kitabu ambamo maneno ya Yeremia yalikuwa yameandikwa (Yer 36:25). kutoka mji wa Kiriath-yearimu. Yeye alitabiri dhidi ya mji huu na dhidi ya nchi hii kama alivyofanya Yeremia. 21Naye mfalme Yehoyakimu pamoja na mashujaa wake na wakuu wote waliposikia mambo aliyosema Uria, mfalme alitaka kumuua. Lakini Uria alipopata habari, alishikwa na hofu, akatoroka na kwenda Misri. 22Mfalme Yehoyakimu alimpeleka Elnathani mwana wa Akbori, pamoja na watu kadhaa huko Misri. 23Wao walimrudisha Uria kutoka Misri, wakampeleka kwa mfalme Yehoyakimu. Mfalme akamuua kwa upanga na maiti yake ikazikwa kwenye makaburi ya watu wa kawaida.)
24Lakini Yeremia alikuwa akilindwa na Ahikamu#26:24 Ahikamu: Huyu Ahikamu na baba yake, Shafani, walikuwa viongozi katika yale marekebisho ya mfalme Yosia (rejea 2Fal 22:12,14); Shafani alikuwa mwandishi na karani wa Yosia. Alisoma mbele ya mfalme maneno ya kitabu cha sheria kilichogunduliwa hekaluni (2Fal 22:8-10). Rejea Yer 29:3; 36:11-13; 39:14; 40:5. mwana wa Shefani, ili asitiwe mikononi mwa watu na kuuawa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza