45
Ahadi ya Mungu kwa Baruku
1Haya ndiyo maneno aliyotamka nabii Yeremia mnamo mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu#45:1 Mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu: Taz Yer 36:1. mwana wa Yosia naye Baruku mwana wa Neria akawa anayaandika kitabuni.
Yeremia alimwambia Baruku: 2“Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi juu yako wewe Baruku: 3Wewe ulisema, ‘Ole wangu! Mwenyezi-Mungu ameniongezea uchungu juu ya maumivu yangu. Nimechoka kupiga kite, wala sipati pumziko.’ 4Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia nikuambie hivi: Tazama, yale niliyojenga nayabomoa, na yale niliyopanda nayang'oa;#45:4 Niliyojenga nayabomoa …niliyopanda nayang'oa: Taz Yer 1:9-10 maelezo. nitafanya hivyo katika nchi yote. 5Je, wewe unajitakia mambo makubwamakubwa? Usiyatafute! Achana nayo, maana, ninaleta maangamizi juu ya wanadamu wote. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe tuzo lako ni hili: nitayaokoa maisha yako kila mahali utakapokwenda.”#45:5 Haisemwi hapa ni mambo gani makubwa ambayo Baruku alikuwa anataka kuyafanya. Lakini wazo lililopo ni dhahiri: Katika hali yenyewe haitafaa kitu kutafuta makubwa; yatosha tu kuokoa maisha yake. Rejea Yer 38:2.