11
Hoja ya Sofari#11:1-20 Kwa jumla, hoja ya Sofari inasisitiza juu ya ukuu wa hekima ya Mungu isiyoweza kuchunguzika (11:1-12) kisha Sofari anamgeukia Yobu na kumwalika ajinasue kutoka dhambi, apate kufaidi baraka za Mungu (11:13-20).
1Kisha Sofari, Mnaamathi, akamjibu Yobu:
2“Je, wingi huu wa maneno uachwe tu bila kujibiwa?
Je, mtu wa maneno mengi aonesha kuwa hana hatia?
3Je, kuropoka kwako kutanyamazisha watu?
Na kama ukidhihaki, je, hamna atakayekuaibisha?
4Wewe wadai: ‘Ninachosema ni kweli,
naam, sina lawama mbele ya Mungu.’
5Laiti Mungu angefungua kinywa chake
akatoa sauti yake kukujibu!
6Angekueleza siri za hekima,
maana yeye ni mwingi wa maarifa.#11:6 Maana yeye ni mwingi wa maarifa: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.
Jua kwamba Mungu hakuhesabu makosa yako yote.
7“Je, unaweza kugundua siri zake Mungu
na kujua ukomo wake yeye Mungu mwenye nguvu?
8Ukuu wake wapita mbingu, wewe waweza nini?
Kimo chake chapita Kuzimu,#11:8 Kuzimu: Neno hili linatafsiri neno la Kiebrania “sheol” (taz 3:17 na 10:22 ambamo maana hiyo inasemwa kwa maneno “kwa wafu” na “nchi ya huzuni”).
wewe waweza kujua nini?
9Ukuu huo wapita marefu ya dunia,
wapita mapana ya bahari.
10Kama Mungu akipita,
akamfunga mtu na kumhukumu,
nani awezaye kumzuia?
11Mungu anajua watu wasiofaa;
akiona maovu yeye huchukua hatua.
12“Mpumbavu hawezi kuwa na maarifa,
pundamwitu ni pundamwitu tu.#11:12 Maneno ya aya hii yana shabaha ya kumkemea Yobu kwa kutumia lugha ya kukebehi.
13“Yobu, ukiufanya moyo wako mnyofu,
utainua mikono yako kumwomba Mungu!
14Kama una uovu, utupilie mbali.
Usikubali ubaya uwemo nyumbani mwako.
15Hapo utajitokeza mbele ya watu bila lawama,
utakuwa thabiti bila kuwa na hofu.
16Utazisahau taabu zako zote;
utazikumbuka tu kama mafuriko yaliyopita.
17Maisha yako yatang'aa kuliko jua la adhuhuri,
giza lake litabadilika kuwa mng'ao wa pambazuko.
18Utakuwa na ujasiri maana lipo tumaini;
utalindwa na kupumzika salama.
19Utalala bila kuogopeshwa na mtu;
watu wengi watakuomba msaada.
20Lakini waovu macho yao yatafifia,
njia zote za kutorokea zitawapotea;
tumaini lao la mwisho ni kukata roho!”