16
Jibu la Yobu#16:1—17:16 Katika sehemu hii ya maneno ya Yobu, kwanza ni jibu kwa hoja ya Elifazi ambamo anasema rafikize hawafikirii sawa na wanatoa picha isiyo sawa na ya Mungu badala ya kutilia maanani hali ya mwenye kuteseka (16:1-22) kisha linafuata lalamiko la Yobu kwa Mungu (17:1-16).
1Hapo Yobu akajibu:
2“Mambo kama hayo nimeyasikia mengi;
nyinyi ni wafariji duni kabisa!
3Mwisho wa maneno haya matupu ni lini?
Au ni kitu gani kinachowachochea kujibu?
4Kama nyinyi mngekuwa mimi, na mimi nyinyi,
ningeweza kusema kama nyinyi
ningeweza kubuni maneno dhidi yenu,
na kutikisa kichwa changu.
5Ningeweza kuwatia moyo kwa maneno yangu,
na maneno yangu ya faraja yangewatuliza.
6“Lakini nikisema maumivu yangu hayatulii,
na nikikaa kimya hayaondoki.
7Kweli Mungu amenichakaza
ameharibu kila kitu karibu nami.
8Amenifanya ninyauke, na huo ni ushindi dhidi yangu.
Kukonda kwangu kumenikabili
na kushuhudia dhidi yangu.
9Amenirarua kwa hasira na kunichukia;
amenisagia meno;
na adui yangu ananikodolea macho.
10Watu wananidhihaki na kunicheka;
makundi kwa makundi hunizunguka,
na kunipiga makofi mashavuni.
11Mungu amenitia mikononi mwa wajeuri,
na kunitupa mikononi mwa waovu.
12Nilikuwa nimestarehe, lakini akanivunjavunja,
alinikaba shingo na kunipasua vipandevipande;
alinifanya shabaha ya mishale yake,
13akanipiga mishale kutoka kila upande.
Amenipasua figo bila huruma,
na nyongo yangu akaimwaga chini.
14Hunivunja na kunipiga tena na tena;
hunishambulia kama askari.
15“Nimejishonea mavazi ya gunia,#16:15 Mavazi ya gunia: Mavazi hayo yalivaliwa wakati wa huzuni na maombolezo.
fahari yangu nimeibwaga mavumbini.
16Uso wangu ni mwekundu kwa kulia,
kope zangu zimekuwa nyeusi ti;
17ingawa sijafanya dhuluma kwa mkono wangu,
na sala zangu kwa Mungu ni safi.
18“Ewe dunia, usiifunike damu yangu iliyomwagika;
kilio changu kienee kila mahali.
19Nina hakika ninaye shahidi wangu mbinguni,
mwenye kunitetea yuko huko juu.#16:19 Yobu 19:25. Neno “shahidi” laweza pia kutafsiriwa kwa neno “mtetezi”.
20Rafiki zangu wanidharau;
nabubujika machozi kumwomba Mungu.#16:20 Rafiki …kumwomba Mungu: Au: “Mungu ni rafiki yangu na ndiye ninayemwomba”.
21Laiti mtu angenitetea mbele ya Mungu,
kama ifanyikavyo duniani kati za watu wawili.
22Naam, miaka yangu ni michache,
nami nitakwenda huko ambako sitarudi.