Yobu 18
BHNTLK

Yobu 18

18
Hoja ya pili ya Bildadi#18:1-21 Hii ni hoja au hotuba ya pili ya Bildadi (ya kwanza ilikuwa sura ya 8). Hapa anaeleza tu adhabu anazopata mtu mwovu.
1Kisha Bildadi, Mshuhi, akajibu:
2“Utawinda maneno ya kusema hadi lini?
Tafakari vizuri nasi tutasema.
3Kwa nini unatufanya kama ng'ombe?
Mbona unatuona sisi kuwa wapumbavu?
4Wewe unajirarua mwenyewe kwa hasira zako.
Kwani, dunia itaachwa tupu kwa ajili yako
au miamba ihamishwe toka mahali pake?
5“Naam, mwanga wa mtu mwovu utazimishwa;
mwali wa moto wake hautang'aa.
6Nyumbani kwake mwanga ni giza,
taa inayomwangazia itazimwa.
7Hatua zake ndefu zitafupishwa;
mipango yake itamwangusha chini.
8Nyayo zake mwenyewe zitamtia mtegoni;
kila akitembea anakumbana na shimo.
9Mtego humkamata kisiginoni,
tanzi humbana kabisa.
10Amefichiwa kitanzi ardhini;
ametegewa mtego njiani mwake.
11Hofu kuu humtisha kila upande,
humfuata katika kila hatua yake.
12Alikuwa na nguvu, lakini sasa njaa imembana;
maafa yako tayari kumwangusha.
13“Ugonjwa mbaya unakula ngozi yake,
maradhi ya kifo#18:13 Maradhi ya kifo: Neno kwa neno “mzaliwa wa kwanza wa kifo” namna moja ya kimfano ya kuonesha uhusiano thabiti uliopo kati ya maradhi na kifo. hula viungo vyake.
14Anang'olewa katika nyumba aliyoitegemea,
na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.#18:14 Mfalme wa vitisho: Picha nyingine ya kifo. Maneno haya yanatumiwa hapa tu katika Biblia na huenda yanamtaja “Mot”, mungu wa kifo wa watu wa Kanaani.
15Nyumba yake tupu, wengine wataishi humo;
madini ya kiberiti yametawanywa katika makao yake.#18:15 Madini ya kiberiti yametawanywa katika makao yake: Madini ya kiberiti yalitumiwa hapo kale kusafisha vyumba ambavyo vilikuwa na maiti au kama kitendo cha kidini cha kuondoa pepo wabaya.
16Yeye ni kama mti uliokauka mizizi,
matawi#18:16 Matawi: Matumizi ya matawi hapa (na hata “mizizi”) huenda ni ya mfano kuashiria wazawa wa mtu. yake juu yamenyauka.
17Nchini hakuna atakayemkumbuka;
jina lake halitatamkwa tena barabarani.
18Ameondolewa mwangani akatupwa gizani;
amefukuzwa mbali kutoka duniani.
19Hana watoto wala wajukuu;
hakuna aliyesalia katika makao yake.
20Watu wa magharibi wameshangazwa na yaliyompata,
hofu imewakumba watu wa mashariki.
21Hayo ndio yanayowapata wasiomjali Mungu;
hapo ndipo mahali pa wasiomjua Mungu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza