20
Hoja ya tatu ya Sofari#20:1-29 Kwa mara nyingine Sofari anafafanua tena fundisho linalojulikana: kwamba waovu hupata adhabu wanayostahili.
1Kisha Sofari, Mnaamathi, akajibu:
2“Fikira zangu zanifanya nikujibu,
wala siwezi kujizuia tena.
3Nasikia maonyo nisiyoweza kuvumilia,
lakini akili yangu yanisukuma nijibu.
4“Wewe labda umesahau jambo hili:
kwamba tangu zamani Mungu alipomuumba mtu duniani,
5mwovu atajiona ameshinda kwa muda tu,
furaha yake asiyemcha Mungu ni ya muda mfupi tu!
6Mwovu aweza kufana hata kufikia mbingu,
kichwa chake kikafika kwenye mawingu,#20:6 Kufikia mbingu …kwenye mawingu: Picha ya kuonesha upeo wa mwovu.
7lakini atatupiliwa mbali kama mavi yake.
Waliopata kumjua watajiuliza: ‘Yuko wapi?’
8Atatoweka kama ndoto, asionekane tena,
atafutika kama maono ya usiku.
9Aliyemwona, hatamwona tena,
wala pale alipoishi hapatatambuliwa tena.
10Yeye mwenyewe itambidi kurudisha mali yake yote,
watoto wake wataomba huruma kwa maskini.#20:10 Yeye mwenyewe …huruma kwa maskini: Tafsiri nyingine yamkini: “Watoto wake wataomba huruma kwa maskini ambao aliwaibia”. Jambo la kuwakandamiza maskini ni uhalifu mkuu wa sheria (taz Kumb 24:10-22; Zab 10:2; Isa 3:14-15; Eze 18:12; Amo 4:1).
11Japo alijisikia amejaa nguvu za ujana,
lakini zote zitalala pamoja naye mavumbini.
12“Mdomoni mwake uovu ni mtamu kama sukari,
anauficha chini ya ulimi wake;
13hataki kabisa kuuachilia,
bali anaushikilia kinywani mwake.
14Lakini ufikapo tumboni huwa mchungu,
mkali kama sumu ya nyoka.
15Mwovu humeza mali haramu na kuitapika;
Mungu huitoa tumboni mwake.
16Anachonyonya mtu mwovu ni sumu ya nyoka;
atauawa kwa kuumwa na nyoka.
17Hataishi kuiona mitiririko ya fanaka,
wala vijito vya mafanikio na utajiri.
18Matunda ya jasho lake atayaachilia,
hatakuwa na uwezo wa kuyaonja,
19kwa sababu amewaangamiza maskini na kuwaacha,
amenyakua nyumba ambazo hakuzijenga.
20“Kwa vile ulafi wake hauna mwisho,#20:20 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.
hataweza kuokoa chochote anachothamini.
21Baada ya kula hakuacha hata makombo,
kwa hiyo fanaka yake yote haitadumu.
22Kileleni mwa fanaka dhiki itamvamia,
balaa itamkumba kwa nguvu zote.
23Akiwa anajishughulisha kushibisha tumbo,
Mungu atamletea ghadhabu yake
imtiririkie kama chakula chake.#20:23 Imtiririkie kama chakula chake: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania ya aya hii ya 23.
24Labda ataweza kuepa upanga wa chuma,
kumbe atachomwa na upanga wa shaba.
25Mshale utachomolewa kutoka mwilini mwake;
ncha yake itatolewa mgongoni mwake iking'aa,
vitisho vya kifo vitamvamia.
26Hazina zake zitaharibiwa,
moto wa ajabu utamteketeza;
kilichobaki nyumbani mwake kitateketezwa.
27Mbingu zitaufichua uovu wake,
dunia itajitokeza kumshutumu.
28Mali zake zitanyakuliwa
katika siku ya ghadhabu ya Mungu.
29Hicho ndicho apewacho mtu mwovu kutoka kwa Mungu,
ndicho mwovu alichopangiwa na Mungu.”