28
Sifa za hekima#28:1-28 Sura hii, ingawa haina manung'uniko na majibizano kati ya Yobu na rafikize, inayo uhusiano na sura 11 kuhusu dhamira au wazo la hekima ya Mungu ambayo binadamu hawezi kuipata bila kupewa na Mungu mwenyewe. Makala ya Kiebrania haioneshi ni nani anayeongea katika sura hii.
1“Hakika kuna machimbo ya fedha,
na mahali ambako dhahabu husafishwa.
2Watu huchimba chuma ardhini,
huyeyusha shaba kutoka mawe ya madini.
3Wachimba migodi huleta taa gizani,
huchunguza vina vya ardhi
na kuchimbua mawe yenye madini gizani.
4Binadamu huchimba mashimo mbali na makazi ya watu,
mbali na watu mahali kusipofikika,
wachimba madini huning'inia wamefungwa kamba.
5Kutoka udongoni chakula hupatikana,
lakini chini yake kila kitu huvurugwa kwa moto.
6Katika mawe yake ndimo vilimo vito vya rangi ya samawati
na udongo wake una vumbi la dhahabu.#28:6 Dhahabu: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania ya aya hii ya 6.
7“Njia za kwenda kwenye migodi hiyo
hakuna ndege mla nyama azijuaye;
na wala jicho la tai halijaiona.
8Wanyama waendao kwa madaha hawajazikanyaga
wala simba hawajawahi kuzipitia.
9Binadamu huchimbua miamba migumu kabisa,
huichimbua milima na kuiondolea mbali.
10Hupasua mifereji kati ya majabali,
na jicho lake huona vito vya thamani.
11Huziba chemchemi#28:11 Huziba chemchemi: Tafsiri ya makala ya Kiebrania. Kulingana na tafsiri nyingine za kale ni “Hufunua vianzio.” zisitiririke,
na kufichua vitu vilivyofichika.
12“Lakini hekima itapatikana wapi?
Ni mahali gani panapopatikana maarifa?
13Hakuna mtu ajuaye thamani ya hekima,
wala hekima haipatikani nchini mwa walio hai.
14Vilindi vyasema, ‘Hekima haimo kwetu,’
na bahari yasema, ‘Haiko kwangu.’
15Hekima haiwezi kupatikana kwa dhahabu,
wala kwa kupima kiasi kingi cha fedha.
16Haiwezi kupimwa kwa dhahabu ya Ofiri,
wala kwa vito vya Sardoniki au vya rangi ya samawati,
17dhahabu au kioo#28:17 Kioo: Hapo kale kioo na vitu vilivyotengenezwa nacho vilihesabiwa miongoni mwa vitu vya thamani. havilingani nayo,
wala haiwezi kubadilishwa na vito vya dhahabu safi.
18Hekima ina thamani kuliko matumbawe#28:18 Matumbawe …marijani … lulu Vitu hivi ni vito vya thamani. Kadhalika na “topazi” katika aya inayofuata. na marijani,
thamani yake yashinda thamani ya lulu.
19Topazi ya Kushi#28:19 Kushi: Eneo la Afrika Kaskazini kuanzia kusini mwa Misri kuelekea sehemu ambayo sasa ni Ethiopia na Eritrea hadi Sudani na hata sehemu ya kaskazini ya Afrika Mashariki. haiwezi kulinganishwa nayo,
wala haiwezi kupewa bei ya dhahabu safi.
20“Basi, hekima yatoka wapi?
Ni wapi panapopatikana maarifa?
21Imefichika machoni pa viumbe vyote hai,
na ndege wa angani hawawezi kuiona.
22Abadoni na Kifo wasema,
‘Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.’
23“Mungu aijua njia ya hekima,
anajua mahali inapopatikana.
24Maana yeye huona mpaka upeo wa dunia,
huona kila kitu chini ya mbingu.
25Alipoupa upepo uzito wake,
na kuyapimia maji mipaka yake;
26alipoamua mvua inyeshe wapi,
umeme na radi vipite wapi;
27hapo ndipo alipoiona hekima na kuitangaza,
aliisimika na kuichunguza.”
28Kisha Mungu akamwambia mwanadamu:
“Tazama! Kumcha Bwana ndio hekima;
na kujitenga na uovu ndio maarifa.”#28:28 Aya hii inakamilisha kwa upeo utenzi wa sura hii ya 28. Hekima hupatikana katika kumcha Bwana (yaani Mungu). Taz Kumb 6:13. Taz pia Yobu 1:1; Zab 111:10; Meth 1:7; 9:10; 15:33.