3
MAJADILIANO YA YOBUNA RAFIKI ZAKE
Yobu analalamika#3:1-26 Sura hii yahusu lalamiko la kwanza la Yobu kutokana na hali ngumu ya mateso iliyompata. Yobu anamlalamikia Mungu, lakini, kinyume na alivyosema Shetani (2.5), Yobu hamtukani wala kumlaani, ila anailaani siku aliyozaliwa hata kufikia mateso hayo (Yer 20:14-18). Katika 3:20-23 Yobu analalamika kwamba watu wanaoteseka huendelea kuishi katika mateso hayo, kama yeye mwenyewe.
1Hatimaye Yobu aliamua kuongea,#3:1 Hatimaye Yobu aliamua kuongea: Baada ya siku saba za kukaa kimya Yobu hawezi tena kujizuia (taz pia mfano wa yule anayeteseka katika Zab 39). akailaani siku aliyozaliwa. 2Yobu akasema:
3“Ilaaniwe siku ile niliyozaliwa;
usiku ule iliposemwa, ‘Mwana amechukuliwa mimba’
4Siku hiyo na iwe giza!
Mungu juu asijishughulishe nayo!#3:4 Asijishughulishe nayo: Neno kwa neno “asiikumbuke”, msemo wenye maana ya “asiijali”, na kama Mungu asipoijali hiyo siku basi itakuwa haipo kabisa, na mwenye kuhusika angetoweka.
Wala nuru yoyote isiiangaze!
5Mauzauza na giza nene yaikumbe,
mawingu mazito yaifunike.
Giza la mchana liitishe!
6Usiku huo giza nene liukumbe!
Usihesabiwe katika siku za mwaka,
wala usitiwe katika idadi ya siku za mwezi.#3:6 Usihesabiwe …usitiwe katika idadi ya siku za mwezi: Msemo mwingine wa maana sawa na 3:4 na hivyo, kuhusu maana, aya hii ni sambamba na hiyo ya nne.
7Naam, usiku huo uwe tasa,
sauti ya furaha isiingie humo.
8Walozi wa siku#3:8 Walozi wa siku: Hapo kale walozi au wachawi walifikiriwa kuwa na uwezo wa kulaani siku na kusababisha kupatwa kwa jua na mwezi na hivyo waliitwa “wenye kulaani siku”. waulaani,
watu stadi wa kuligutua dude Lewiyathani#3:8 Lewiyathani: Jina la mnyama mkubwa na wa ajabu katika hadithi za kale. Alifikiriwa kuishi majini na pengine maelezo yake yalifanana na ya mamba au kiboko (Yobu 41:1-26). Rejea Zab 74:14; 104:26; Isa 27:1. waulaani!
9Nyota zake za pambazuko zififie,
utamani kupata mwanga, lakini usipate,
wala usione nuru ya pambazuko.#3:9 Nyota zake za pambazuko: Huenda hapa yahusu sayari au nyota Merkurio au Veno.
10Maana usiku huo haukulifunga tumbo la mama,
wala kuficha taabu nisizione.
11Mbona sikufa nilipozaliwa,
nikatoka tumboni na kutoweka?
12Kwa nini mama yangu alinizaa?
Kwa nini nikapata kunyonya?
13Maana ningekuwa nimezikwa, kimya;
ningekuwa nimelazwa na kupumzika,
14pamoja na wafalme na watawala wa dunia,
waliojijengea upya magofu yao;#3:14 Magofu yao: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.
15ningekuwa pamoja na wakuu waliokuwa na dhahabu,
waliojaza nyumba zao fedha tele.
16Au, mbona sikuwa kama mimba iliyoharibika,
naam, kama mtoto aliyezaliwa mfu?
17Huko kwa wafu waovu hawamsumbui mtu,
huko wachovu hupumzika.
18Huko wafungwa hustarehe pamoja,
hawaisikii kamwe sauti ya mnyapara.
19Wakubwa na wadogo wako huko,
nao watumwa wamepata uhuru mbali na bwana zao.
20Ya nini kumjalia nuru yule aliye taabuni;
na uhai yule aliye na huzuni moyoni?#3:20-26 Katika aya hizi Yobu anaelekeza maneno yake kwa Mungu.
21Mtu atamaniye kifo lakini hafi;
hutafuta kifo kuliko hazina iliyofichika.
22Mtu kama huyo atashangilia mno na kufurahi,
atafurahi atakapokufa na kuzikwa!
23Ya nini kumjalia uhai mtu ambaye njia zake zimefungwa,
mtu ambaye Mungu amemwekea kizuizi?
24Kwa maana kusononeka ndio mkate wangu,
kupiga kite kwangu kunatiririka mithili ya maji.
25Kile ninachokiogopa kimenipata,
ninachokihofia ndicho kilichonikumba.
26Sina amani wala utulivu;
sipumziki, taabu imenijia.”