Yobu 32
BHNTLK

Yobu 32

32
Elihu anatoa hoja zake#32:1—37:24 Wakati inaonekana kwamba simulizi na hoja za Yobu zimefikia mwisho wake, anatokea Elihu, tena kwa ghafla, kwani inaonekana kwamba Yobu amewashinda rafikize kuhusu jambo la mateso ya mtu asiye na hatia. Katika 31:35-37 Yobu aliomba apewe jibu kutoka kwa Mungu kama jambo la mwisho. Zaidi ya hayo Elihu hajapata kutajwa mahali pengine katika kitabu hiki na wala hatajwi wakati Mungu anapotoa kauli yake dhidi ya Elifazi na rafiki zake wawili (42:7). Tena ni vema kuzingatia yanayosemwa katika 32:1 ambapo mwandishi anasema hakuna hoja nyingine baada ya Yobu kuonesha kwamba hana hatia. Naye Elihu pia anadokezea kwamba kuingilia kati kwa upande wake katika hoja hizo ni kwa vile hao wengine wameshindwa na Yobu amefana (taz 32:13).
(32:1—37:24)
1Basi hawa watu watatu: Elifazi, Bildadi na Sofari, wakaacha kumjibu Yobu kwa vile alijiona kuwa mwema. 2Ndipo Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa ukoo wa Rama,#32:2 Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa ukoo wa Rama: Tofauti na wale rafikize Yobu watatu, Jina la Elihu ni la Kiebrania na maana yake ni “El (mungu) wangu ndiye”. Kuhusu “Buzi” rejea Yer 25:23 ambapo linatajwa pamoja na Dedani na Tema na, yawezekana kwamba ni mojawapo ya makabila ya Kiarabu. akakasirika. Alimkasirikia Yobu kwa sababu Yobu alijiona yeye mwadilifu na sio Mungu. 3Pia, aliwakasirikia rafiki watatu wa Yobu kwa sababu hawakuwa na la kumjibu Yobu, na hivyo kuonesha kwamba Mungu amekosa.#32:3 Kuonesha kwamba Mungu amekosa: Tafsiri hii inatokana na kusahihishwa kwa makala ya Kiebrania. 4Elihu alikuwa amekaa kimya wakati hao wazee waliposema na Yobu kwa kuwa yeye alikuwa kijana kuliko wao. 5Lakini alipoona hao watu watatu wameshindwa kumjibu Yobu, aliwaka hasira.
6Basi, Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi akaanza kusema:
“Mimi ni kijana, nyinyi ni wazee zaidi;
kwa hiyo niliogopa kuwaambieni mawazo yangu.
7Nilisema moyoni: ‘Waache wenye siku nyingi waseme,
wenye miaka mingi wafundishe hekima.’
8Lakini hiyo roho iliyomo ndani ya mtu,
hiyo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu,
ndio inayomwezesha mwanadamu kufahamu.
9Si lazima kuwa mzee ili uwe na hekima
wala wazee siyo wenye kufahamu lililo sawa.
10Kwa hiyo nasema, ‘Nisikilizeni,
acheni nami nitoe maoni yangu.’
11“Basi, mimi nilingojea mlichotaka kusema,
nilisikiliza misemo yenu ya hekima,
mlipokuwa mnajaribu kutafuta la kusema.
12Niliwasikiliza kwa makini sana,
lakini hakuna mmoja wenu aliyemshinda Yobu;
nyote mlishindwa kuyajibu maneno yake.
13Jihadharini msije mkasema, ‘Sasa tumepata hekima.
Atakayemshinda ni Mungu, sio binadamu.’
14Maneno ya Yobu hayakuwa kwa ajili yangu,
kwa hiyo sitamjibu kama mlivyomjibu nyinyi.
15“Nyinyi mmeduwaa; mmeshindwa,
nyinyi hamna cha kusema zaidi.
16Je, ningoje tu kwa vile hamsemi,
kwa sababu mnakaa tu bila kujibu kitu?
17Mimi pia nitatoa jibu langu;
mimi nitatoa pia maoni yangu.
18Ninayo maneno mengi sana,
roho yangu yanisukuma kusema.
19Moyo wangu umefurika kama divai iliyozibwa,
kama kiriba cha divai mpya tayari kupasuka.#32:19 Kama kiriba cha divai mpya tayari kupasuka: Picha tunayopewa hapa ni ya hali ambayo haiwezi kuzuilika. Wakati utomvu wa divai ambayo iliwekwa katika viriba ulipoanza kuchacha, uliweza hata kuvipasua viriba hivyo vya ngozi.
20Ni lazima niseme ili nipate nafuu;
yanipasa kufungua kinywa changu na kujibu.
21Sitampendelea mtu yeyote
wala kutumia maneno ya kubembeleza mtu.
22Maana mimi sijui kubembeleza mtu,
la sivyo, Muumba wangu angeniangamiza.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza