Yobu 6
BHNTLK

Yobu 6

6
1Yobu akamjibu Elifazi:
2“Laiti mahangaiko yangu yangepimwa uzani wake,
mateso yangu yote yakawekwa katika mizani!
3Yangekuwa mazito kuliko mchanga wa pwani.
Ndio maana maneno yangu ni ya kuropoka!#6:3 Katika simulizi hili la pili (6:1—7:2) Yobu anaanza kulalamika kuhusu hali yake ngumu (6:1-7).
4Naam, mishale ya Mungu Mwenye Nguvu imenichoma;#6:4 Mishale ya Mungu Mwenye Nguvu imenichoma: Rejea Yobu 16:12-13; Zab 38:2.
nafsi yangu imekunywa sumu yake.
Vitisho vya Mungu vimenikabili.#6:4 Vitisho vya Mungu vimenikabili: Rejea Zab 88:16.
5Je, pundamwitu hulia akiwa na majani,
au ng'ombe akiwa na malisho?
6Je, kitu kisicho na ladha chaweza kuliwa bila chumvi?#6:6 Je, kitu kisicho na ladha chaweza kuliwa bila chumvi?: Maneno ya Yobu katika aya ya 5 na 6 yanaweza kuhusishwa na hoja ya Yobu dhidi ya rafiki zake katika 6:14-30 na hivyo “chakula bila chumvi” ni maneno yao ambayo hayakumletea kitulizo chochote.
Je ute wa yai una utamu wowote?
7Sina hamu ya kuvigusa vyakula hivyo,
hivyo ni vyakula vyangu vichukizavyo.”
8“Laiti ningejaliwa ombi langu,
Mungu akanipatia kile ninachotamani:
9kwamba angekuwa radhi kunipondaponda,
angenyosha mkono wake anikatilie mbali!
10Hiyo ingekuwa faraja yangu,
ningefurahi katika maumivu yasiyo na huruma.
11Lakini sina nguvu ya kuweza kuendelea;
sijui mwisho wangu utakuwaje, nipate kuvumilia.
12Je, nguvu zangu ni kama za mawe?
Au mwili wangu kama shaba?
13Kweli kwangu hamna cha kunisaidia;
msaada wowote umeondolewa kwangu.
14“Anayekataa kumhurumia rafiki yake,
anakataa kumcha Mungu#6:14 Anayekataa …anakataa kumcha Mungu: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania. Wengine hutafsiri: “Mwenye kuteseka anastahili kufarijiwa na rafiki yake, hata kama ameacha kumcha Mungu Mwenye Nguvu.” mwenye nguvu.#6:14-20 Katika kisehemu hiki Yobu anasema juu ya udanganyifu unatokana na maneno ya rafikize.
15Rafiki zangu wamenidanganya kama kijito,
wamenihadaa kama mitaro isiyo na maji.
16Ambayo imejaa barafu,
na theluji imejificha ndani yake.
17Lakini wakati wa joto hutoweka,
wakati wa hari hubaki mito mikavu.
18Misafara hupotea njia wakitafuta maji,
hupanda nyikani na kufia huko.
19Misafara ya Tema hutafuta tafuta,
wasafiri wa Sheba#6:19 Misafara ya Tema …Sheba: Tema ni eneo kaskazini-magharibi ya Arabia na Sheba labda ilikuwa pande za kusini-magharibi ya Arabia hata mpaka eneo fulani la Afrika. Maeneo hayo yalisifika kwa dhahabu yake na ubani (Isa 60:6). hutumaini.
20Huchukizwa kwa kutumaini bure,
hufika kwenye vijito hivyo na kuudhika.
21Nyinyi mmekuwa kama vijito hivyo,#6:21 Nyinyi …kama vijito hivyo: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.
mwaona balaa yangu na kuogopa.
22Je, nimesema mnipe zawadi?
Au mnitolee rushwa kwa mali zenu?
23Au mniokoe makuchani mwa adui?
Au mnikomboe mkononi mwa wadhalimu?
24“Nifundisheni, nami nitanyamaza.
Nielewesheni jinsi nilivyokosea.
25Maneno ya kweli yana nguvu kubwa!
Lakini makaripio yenu yananikosoa nini?
26Je, mnadhani kwamba mwaweza kuyakosoa maneno?
Maneno ya mtu aliyekata tamaa ni upepo tu.
27Nyinyi mnathubutu hata kuwapigia yatima kura;
mnawapigia bei hata marafiki zenu!
28Lakini sasa niangalieni tafadhali.
Mimi sitasema uongo mbele yenu.
29Acheni tafadhali, kusiwe na uovu;
acheni sasa, kwani mimi ni mnyofu.
30Je, mnadhani kwamba nimesema uovu?
Je, mnafikiri mimi siyatambui machungu?

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza