9
Jibu la Yobu
1Kisha Yobu akajibu:#9:1—10:22 Hii ni sehemu ya pili ya mazungumzo ya Yobu. Katika sehemu hii Yobu anasema kwamba haiwezekani kumshinda Mungu katika kesi (9:2-4,14-16,19-31), kisha anasema juu ya nguvu kuu ya Mungu (9:5-13,17-19,32-35).
2“Kweli najua hivyo ndivyo ilivyo.
Lakini mtu awezaje kuwa mwema mbele ya Mungu?
3Kama mtu angethubutu kushindana naye,
hataweza kufika mbali;
hata kujibu swali moja kati ya elfu.
4Yeye ni mwenye hekima mno na nguvu nyingi,
nani aliyepingana naye, akashinda?
5Yeye huiondoa milima bila yenyewe kutambua,
huibomolea mbali kwa hasira yake.
6Yeye huitikisa dunia kutoka mahali pake,
na nguzo zake zikatetemeka.
7Huliamuru jua lisichomoze
huziziba nyota zisiangaze.
8Yeye peke yake alizitandaza mbingu,
na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9Ndiye aliyezifanya nyota angani:
Dubu, Orioni, Kilimia, na nyota za kusini.
10Ndiye atendaye makuu yasiyoeleweka,
mambo ya ajabu yasiyo na idadi.
11Loo! Hupita karibu nami nisimwone,
kisha huenda zake bila ya mimi kumtambua.
12Tazama! Yeye huchukua anachotaka;
nani awezaye kumzuia?
Nani awezaye kumwuliza: ‘Unafanya nini?’
13“Mungu hatazuia hasira yake;
chini yake wainama kwa hofu Rahabu na wasaidizi wake.#9:13 Rahabu na wasaidizi wake: Jina “Rahabu” linamtaja mnyama mkubwa wa ajabu katika hadithi za kale na hutumika kama kielelezo cha nguvu zinazopingana na Mungu. Katika Zab 87:4 Rahabu ni jina lingine la Misri; rejea Yobu 7:12; 26:12; Isa 51:9.
14Nitawezaje basi kumjibu Mungu?
Nitachagua wapi maneno ya kumwambia?
15Ingawa sina hatia, siwezi kumjibu.
Lazima kumwomba anihurumie huyo mshtaki wangu.#9:15 Mshtaki wangu: Au, “mpinzani wangu.”
16Hata kama ningemwita naye akajibu,
nisingeweza kuamini kuwa ananisikiliza.
17Yeye huniponda kwa dhoruba;
huongeza majeraha yangu bila sababu.
18Haniachi hata nipumue;
maisha yangu huyajaza uchungu.
19Kama ni kushindana, yeye ana nguvu mno!
Na kama ni kutafuta juu ya haki,
nani atakayemleta#9:19 Atakayemleta: Makala ya Kiebrania ina mtendewa katika nafsi ya kwanza, yaani “atakayenileta”, lakini mazingira ya maandishi hapa yanawiana zaidi na tafsiri inayotolewa hapa. mahakamani?
20Ingawa sina hatia, maneno yangu yenyewe yangenihukumu;
ingawa sina lawama, angenithibitisha kuwa mpotovu.
21Sina lawama, lakini sijithamini.
Nayachukia maisha yangu.
22Yote ni mamoja, kwa hiyo nasema;
Mungu huwaangamiza wema na waovu.#9:22 Mungu huwaangamiza wema na waovu: Yobu hawezi kuelewa kwa nini mtu mwadilifu anateseka (rejea 10:2-7).
23Maafa yaletapo kifo cha ghafla,
huchekelea balaa la wasio na hatia.
24Nchi ikitiwa watu waovu katika utawala wa mwovu,
Mungu huyafumba macho ya mahakimu wake!
Kama si yeye afanyaye hivyo, ni nani basi?
25“Siku zangu zaenda mbio#9:25 Siku zangu zaenda mbio: Taz pia 7:7-10 ambapo Yobu anaeleza jinsi maisha yanavyopita mbio. kuliko mpiga mbio;
zinakimbia bila kuona faida.
26Zapita kasi kama mashua ya matete;
kama tai anayerukia mawindo yake.
27Nasema: ‘Nitasahau lalamiko langu,
niondoe uso wangu wa huzuni na kuwa na furaha!’
28Lakini nayaogopa maumivu yangu yote,
kwani najua Mungu hataniona kuwa sina hatia.
29Ikiwa nitahukumiwa kuwa na hatia,
ya nini basi nijisumbue bure?
30Hata kama nikitawadha kwa theluji,
na kujitakasa mikono kwa sabuni,
31hata hivyo, atanitumbukiza shimoni kwenye uchafu,
na mavazi yangu yataniona kuwa kinyaa.
32Mungu si mtu kama mimi niweze kumjibu,
hata tuweze kwenda mahakamani pamoja.
33Hakuna msuluhishi kati yetu,
ambaye angeamua kati yetu sisi wawili.
34Mungu na aniondolee hiyo fimbo ya kunipiga,
na kitisho chake kisinitie hofu!
35Hapo ningeweza kusema bila kumwogopa;
kwani sivyo nilivyo nafsini mwangu.#9:35 Kwani sivyo nilivyo nafsini mwangu: Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania. Tafsiri ya kale ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) ina “kwani sijifikirii nimemkosea haki.”