Yoeli 2
BHNTLK

Yoeli 2

2
Nzige: onyo juu ya siku ya Mwenyezi-Mungu
1Pigeni tarumbeta huko Siyoni;
pigeni baragumu#2:1 Pigeni tarumbeta …pigeni baragumu: Tarumbeta au baragumu ilitumiwa kutangaza tukio maalumu, mara nyingi tukio hatari (Amu 3:27; 1Sam 13:3; 2Sam 2:28; Yer 6:1; Hos 5:8); au mwito kwa watu kukutana hekaluni (Hes 10:2-10; Isa 27:13; Yoe 2:15). Rejea pia picha hiyo katika 1Thes 4:16. juu ya mlima mtakatifu!
Tetemekeni enyi wakazi wa Yuda,
maana siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja,
naam, siku hiyo iko karibu!
2Hiyo ni siku ya giza na huzuni;
siku ya mawingu na giza nene.#2:2 Siku ya giza …nene: Taz pia 2:10,31 na Sef 1:15.
Jeshi kubwa la nzige linakaribia
kama giza linalotanda milimani.
Namna hiyo haijapata kuweko kamwe
wala haitaonekana tena
katika vizazi vyote vijavyo.
3Kama vile moto uteketezavyo
jeshi hilo laharibu kila kitu mbele yake
na kuacha nyuma kila kitu kinateketezwa;
kabla hawajapita, nchi ni kama bustani ya Edeni,#2:3 Nchi ni kama bustani ya Edeni: Rejea Mwa 2:8. taz pia Eze 36:35 ambapo kuna ulinganisho kama huu lakini kinyume chake.
lakini wakisha pita, ni jangwa tupu.
Hakuna kiwezacho kuwaepa!
4Wanaonekana kama farasi,
wanashambulia kama farasi wa vita,
5Wanaporukaruka kwenye vilele vya milima,
wanarindima kama magari ya farasi,
wanavuma kama mabua makavu motoni.
Wamejipanga kama jeshi kubwa
tayari kabisa kufanya vita.
6Wakaribiapo, watu hujaa hofu,
nyuso zao zinawaiva.
7Wanashambulia kama mashujaa wa vita;
kuta wanazipanda kama wanajeshi.
Wote wanakwenda mbele moja kwa moja,
bila hata mmoja wao kubadilisha njia.
8Hakuna amsukumaye mwenziwe;
kila mmoja anafuata mkondo wake.
Wanapita kati ya vizuizi vya silaha,
wala hakuna kiwezacho kuwazuia.
9Wanauvamia mji,
wanapiga mbio ukutani;
wanaziparamia nyumba na kuingia,
wanapenya madirishani kama wezi.
10Nchi inatetemeka mbele yao,
mbingu zinatikisika.
Jua na mwezi vyatiwa giza,
nazo nyota zinaacha kuangaza.
11Mwenyezi-Mungu anaamuru jeshi lake kwa sauti;
askari wake ni wengi mno,
wanaomtii hawahesabiki.
Siku ya Mwenyezi-Mungu kweli ni kuu na ya kutisha sana!
Nani atakayeweza kuistahimili?#2:11 Nani atakayeweza kustahimili?: Taz Nah 1:6; Mal 3:2; Ufu 6:17.
Wito wa toba
12“Lakini hata sasa,”
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
“Nirudieni kwa moyo wote,
kwa kufunga, kulia na kuomboleza.
13Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni
bali nirudieni kwa moyo wa toba.”
Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu;
yeye amejaa neema na huruma;#2:13 Mwenyezi-Mungu …amejaa neema na huruma: Kut 34:6; Neh 9:17; Zab 86:15; 103:8; Yona 4:2.
hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili;
daima yu tayari kuacha kuadhibu.
14Huenda#2:14 Huenda: Rejea Amo 5:15; Yona 3:9; Sef 2:3. Uamuzi wa kusamehe ni wa Mungu peke yake. Tendo la binadamu la kutubu haliwezi kuhimiza uamuzi wa kimungu, ila linampa binadamu tumaini la kupata huruma yake Mungu (rejea 2Sam 12:22; Omb 3:29). Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia
na kuwapeni baraka ya mazao,
mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji.
15Pigeni tarumbeta huko Siyoni!
Toeni amri watu wafunge;#2:15 Watu wafunge: Taz Yoe 1:14 na 2:1. Katika 2:1 Tarumbeta inapigwa kuashiria kufika tukio la hatari; hapa kuwaita watu wafunge na kuomba toba.
itisheni mkutano wa kidini.
16Wakusanyeni watu wote,
wawekeni watu wakfu.
Waleteni wazee,
wakusanyeni watoto,
hata watoto wanyonyao.
Bwana arusi na bibi arusi
na watoke vyumbani mwao.
17Kati ya madhabahu#2:17 Madhabahu: Hiyo madhabahu au mahali pa kutambikia ni ile ya shaba ambapo watu waliteketeza kafara walizomtolea Mungu (2Nya 4:1). na lango la hekalu,
makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu,
walie na kuomba wakisema:
“Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Usiyaache mataifa mengine yatudharau
na kutudhihaki yakisema,
‘Yuko wapi basi Mungu wao?’”#2:17 Yuko wapi …Mungu wao?: Taz Zab 42:3.
Mungu ataifanikisha nchi
18Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake
akawahurumia watu wake.
19Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema,
“Sasa nitawapeni tena nafaka,
sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa.
20Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini,#2:20 Adui watokao kaskazini: Kwa wingi, maadui wa Waisraeli kama vile Waashuru na Wababuloni waliwavamia walitoka kaskazini (Yer 1:14-15; 4:6; 6:1; Eze 26:7; 38:6,15; 39:2). Eneo hilo liliwatisha Waisraeli na lilikuwa mfano wa nguvu za kutisha.
nitawafukuza mpaka jangwani;
askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi
na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea.
Watatoa uvundo na harufu mbaya,
hao ambao wamefanya maovu makubwa.
21“Usiogope, ewe nchi,
bali furahi na kushangilia,
maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu.
22Msiogope, enyi wanyama.
malisho ya nyikani yamekuwa mazuri,
miti inazaa matunda yake,
mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi.
23“Furahini, enyi watu wa Siyoni,
shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
maana amewapeni mvua za masika,#2:23 Mvua za masika: Au: mvua za masika kwa kuwa ni mwenye haki.
amewapeni mvua ya kutosha:
mvua za masika na mvua za vuli kama hapo awali.
24Mahali pa kupuria patajaa nafaka,
mashinikizo yatafurika divai na mafuta.
25Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige,
kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu,
hilo jeshi kubwa nililowaletea!
26Mtapata chakula kingi na kutosheka;
mtalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
aliyewatendea mambo ya ajabu.
Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.
27Mtatambua kwamba mimi nimo miongoni mwenu,
enyi Waisraeli;
kwamba mimi Mwenyezi-Mungu,
ndimi Mungu wenu wala hakuna mwingine.#2:27 Mungu wenu wala hakuna mwingine: Kut 20:1-2 na Kumb 4:35 zinasisitiza kwamba Mungu ni Mungu wa pekee. Taz pia Isa 42:8; 45:5-6,18; Eze 36:11.
Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.
Siku ya Mwenyezi-Mungu#2:28-32 Baadaye: Yaani wakati ahadi hizo zitakapokuwa zimetimia (taz Mate 2:17-21).
28“Kisha hapo baadaye
nitaimimina roho yangu#2:28 Nitaimimina roho yangu: Taz Isa 42:1 maelezo. Mazingira ya maandishi ya hapa yanaelekea kuhusu zawadi ya Mungu ya kusema ujumbe wake au ya kinabii (rejea Mika 3:8). juu ya binadamu wote.
Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri,#2:28 Watatabiri: Wakati uliopita, kipaji hicho cha unabii walipewa wachache, lakini katika siku za usoni wote watapewa tena kwa wingi. 2:28-32 imenukuliwa katika Mate 2:17-21, kama tukio ambalo limekalika katika kuja kwake Roho Mtakatifu baada ya kufufuka kwake Yesu Kristo.
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.#2:28 Katika makala ya Kiebrania sura ya 3 inaanza hapa.
29Hata juu ya watumishi wa kiume na wa kike,
nitaimimina roho yangu wakati huo.
30“Nitatoa ishara mbinguni na duniani;
kutakuwa na damu, moto na minara ya moshi.
31Jua litatiwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kufika siku ya Mwenyezi-Mungu,
siku iliyo kuu na ya kutisha.
32Hapo watu wote watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa.#2:32 Watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa: Rejea Mate 2:17-21 na maelezo yake.
Maana katika mlima Siyoni na Yerusalemu,
watakuwako watu watakaosalimika,
kama nilivyosema mimi Mwenyezi-Mungu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza