2
Sala ya Yona#2:1-10 Sala ya Yona ina muundo wa zaburi za shukrani ambapo mshairi anamkiri Mwenyezi-Mungu kama Mwokozi na kumalizia na ahadi ya kumtolea sadaka hekaluni Yerusalemu. Rejea Zab 30; 116; 118 na taz pia Utangulizi wa kitabu cha Zaburi.
1Basi, Yona, akiwa tumboni mwa samaki huyo, akawa akimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, 2akisema:
“Kwa sababu ya taabu yangu,
nilikuomba, ee Mwenyezi-Mungu,
nawe ukanisikiliza;
toka chini kuzimu, nilikulilia,
nawe ukasikiliza kilio changu.
3Ulinitupa katika kilindi, katikati ya bahari,
gharika ikanizunguka,
mawimbi na gharika vikapita juu yangu.
4Nilidhani kwamba nimetengwa nisiwe mbele yako;
nisiweze kuliona tena hekalu lako takatifu.#2:4 Hekalu …takatifu: Yona aliamini kwamba Mungu kwa namna ya pekee alikuwa katika hekalu la Yerusalemu (Kut 25:10-22; 2Sam 6:2; 1Sam 8:6-13; Eze 10:1-5).
5Maji yalinizunguka na kunisonga;
kilindi kilinifikia kila upande,
majani ya baharini yakanifunika kichwa.
6Niliteremka hadi kwenye misingi ya milima,
katika nchi ambayo milango yake imefungwa milele.
Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,
umenipandisha hai kutoka humo shimoni.#2:2-6 Toka chini …shimoni: Waebrania wa kale waliamini kwamba kulikuwa na bahari kuu chini ya dunia na kuzimu ilikuwa chini ya hiyo bahari kuu. Jina la Kiebrania la mahali hapo ni “Sheol” ambalo linaelezwa katika Biblia kama mahali pa ukimya ambapo waliomo (yaani wafu) hawajisikii au kujua kitu (taz Yobu 10:21,22; Zab 88:12; 94:17). Yona anatumia picha hiyo kuonesha kwamba alijisikia ametengwa mbali na Mungu.
7Roho yangu ilipoanza kunitoka,
nilikukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu,
sala yangu ikakufikia,
katika hekalu lako takatifu.
8Watu wanaoabudu sanamu za miungu batili,
huutupilia mbali uaminifu wao kwako.
9Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani,
nitakutolea sadaka,
na kutimiza nadhiri zangu.
Mwenyezi-Mungu, ndiye aokoaye.”#2:9 Nitakutolea sadaka …Mwenyezi-Mungu, ndiye aokoaye: Linganisha 2:9 na 1:6 na maelezo yake. Inapokuwa ni yeye anatakiwa kuokolewa, Yona yuko radhi kuamini Mungu ndiye aokoaye; lakini baadaye hatapendezwa sana na huruma ya Mungu kwa watu wa Ninewi (taz 4:1-3).
10Basi, Mwenyezi-Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona kwenye nchi kavu.