1
1Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo, nawaandikia nyinyi mlioitwa na Mungu na ambao mnapendwa naye Mungu Baba, na kuwekwa salama kwa ajili ya Yesu Kristo.#1 Taz Utangulizi.
2Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.
Waalimu wa uongo#3-16 Sehemu hii inafanana sana na 2Pet 2:1-22, kama itakavyoonekana katika maelezo yanatolewa katika aya zinazofuata.
3Ndugu wapenzi, nilikuwa na mpango wa kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, lakini nimeona lazima ya kuwaandikieni nikiwahimizeni mwendelee na juhudi kwa ajili ya imani#3 Imani: Taz 2Pet 1:1, maelezo; rejea Yuda 20. ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote. 4Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake Kiongozi na Bwana wetu. Lakini, Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu zamani hukumu inayowangojea watu hao.
5Sasa nataka kuwakumbusheni mambo fulani, ingawaje haya mlikwisha fahamishwa kikamilifu mara moja: kumbukeni jinsi Bwana#5 Bwana: Yaani, Mungu. alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe siku ile kuu.#6 2Pet 2:4. Labda yahusu Mwa 6:1-4. 7Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote.#7 2Pet 2:6. Rejea Mwa 19:1-24.
8Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. Ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu. 9Hata Mikaeli,#9 Mikaeli: Anatajwa katika Dan 10:13,21; 12;1; Ufu 12:7. malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi juu ya mwili wa Mose,#9 Mwili wa Mose: Kumb 34:5-6. Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi, ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.”#9 Bwana …akukaripie: Rejea Zek 3:2; 2Pet 2:11. Kadiri ya mapokeo ya Kiyahudi, Mose alipofariki, Malaika Mkuu Mikaeli alikuja kuuchukua mwili wake, naye Shetani akajaribu kuunyakua mwenyewe. 10Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; wataangamizwa kwa mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama wajuavyo wanyama wasio na akili. 11Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini.#11 Kaini: Mwa 4:3-9; Ebr 11:4; 1Yoh 3:12. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Balaamu.#11 Rejea 2Pet 2:15-16 ambapo ni dhahiri zaidi. Kuhusu “Balaamu” rejea Hes 22:4-35; Ufu 2:14. Wameasi kama Kora#11 Kora: Hes 16:1-35. alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa. 12Kwa makelele yao yasiyo na adabu, na kwa kujipendelea wao wenyewe, watu hao ni kama madoa machafu kwenye karamu mnazoshiriki kwa upendo.#12 Karamu …kwa upendo: Yaani, karamu ambazo waliadhimisha Karamu ya Bwana (taz 1Kor 11:20-22, maelezo). Rejea mwenendo wa baadhi ya Wakorintho katika karamu hizo (1Kor 11:17-21). Wako kama mawingu yasiyo na mvua yanayopeperushwa na upepo. Wao ni kama miti iliyopukutika isiyozaa matunda, iliyokufa kabisa, iliyong'olewa.#12-13 Maneno yanayosemwa katika aya hizi ni mfano na ambayo yametolewa kutoka kitabu kimoja cha maandishi ya Kiyahudi kiitwacho kitabu cha Henoki. Katika kitabu hicho kunasimuliwa habari za kukosekana kwa mvua na mavuno na pia kutaja kufungwa jela kwa nyota. Kitabu hicho si cha Biblia. 13Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanatoka kama povu. Wao ni kama nyota zinazotangatanga ambazo zimewekewa milele mahali pa giza kuu.
14Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu#14-15 Nukuu kutoka kitabu cha Henoki (taz Yuda 12-13, maelezo), ambapo kunasimuliwa njozi au maono ambayo Henoki (Mwa 5:18,21-24) aliyaona baada ya kuchukuliwa mbinguni (rejea Ebr 11:5). 15kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”
16Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe.
Maonyo na maagizo
17Lakini nyinyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo. 18Waliwaambieni: “Siku za mwisho, watatokea watu watakaowadhihaki nyinyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.” 19Hao ndio wanaosababisha mafarakano,#19 Wanaosababisha mafarakano: Rom 16:17; 1Kor 1:10; Tito 3:10. watu wa fikira za kidunia, wasio na Roho wa Mungu. 20Lakini nyinyi, wapenzi wangu, jijengeni wenyewe juu ya imani yenu takatifu kabisa. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, 21na kudumu katika upendo wa Mungu, mkimngojea Bwana wetu Yesu Kristo ambaye, kwa huruma yake, atawajalieni uhai wa milele.
22Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka; 23waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni.#23 Waokoeni …kutoka motoni: Rejea ile adhabu kwa moto iliyowapata watu wa Sodoma na Gomora (aya 7) na ile ya Kora (aya 11); rejea pia Mat 13:42-50. Lakini kwa wengine muwe na huruma pamoja na tahadhari, mkichukia hata mavazi yao yenye madoa ya tamaa zao mbaya.
Sala ya sifa
24Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake, 25kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.