1
1 # 1:1-22 Maombolezo ya kwanza linahusu kuteketezwa kwa Yerusalemu na majeshi ya Babuloni mnamo mwaka 586 K.K. na kupelekwa uhamishoni wengi wa raia wake hadi Babuloni. Katika 1:1-11 mshairi mwenyewe anaomboleza; katika 1:12-22 wakazi wa mji wa Yerusalemu (au mji wenyewe) wanaomboleza. Ajabu#1:1 Ajabu: Kiebrania ni “ekah” neno ambalo ni lalamiko juu ya hali ya sasa kwa kulinganisha na hali iliyokuwa hapo awali (Taz 2Sam 1:19, 25, 27; Isa 1:21; Yer 48:17; Eze 26:17). mji uliokuwa umejaa watu,
sasa wenyewe umebaki tupu!
Ulikuwa maarufu kati ya mataifa;
sasa umekuwa kama mama mjane.
Miongoni mwa miji ulikuwa kama binti mfalme;
sasa umekuwa mtumwa wa wengine.
2Walia usiku kucha;
machozi yautiririka.
Hakuna hata mmoja wa wapenzi wake wa kuufariji.
Rafiki zake wote wameuhadaa;
wote wamekuwa adui#1:2 Wapenzi wake …Rafiki zake … wamekuwa adui: Yaani mataifa ambayo Yuda ilijiunga nao na kufanya mikataba ya kisiasa (ambayo ililaaniwa na manabii, taz Isa 31:1-3; Yer 4:30; 27:1-7; 30:14; Eze 16:33), baadhi yao yalijiunga na Wababuloni kushambulia Yerusalemu (2 Fl 24:1-2). zake.
3Watu wa Yuda wamekwenda uhamishoni
pamoja na mateso na utumwa mkali.
Sasa wanakaa miongoni mwa watu wa mataifa,
wala hawapati mahali pa kupumzika.
Waliowafuatia wamewakamata wakiwa taabuni.
4Barabara za kwenda Siyoni zinasikitisha;
hakuna wapitao kwenda kwenye sikukuu.
Malango ya mji wa Siyoni ni tupu;#1:4 Malango ya mji wa Siyoni …tupu: Mara nyingi watu walikusanyika karibu na malango hayo kufanya biashara au kutatua matatizo (5:14; Rut 4:1-12).
makuhani wake wanapiga kite,
wasichana wake wana huzuni,
na mji wenyewe uko taabuni.
5Adui zake ndio wanaoutawala na wanafanikiwa,
kwani Mwenyezi-Mungu ameutesa
kwa sababu ya makosa mengi.
Watoto wake wametekwa na kupelekwa mbali.
6Fahari yote ya watu wa Siyoni imewatoweka;
wakuu wake wamekuwa kama kulungu wasio na malisho.
Bila nguvu waliwakimbia watesi wao.
7Ukiwa sasa magofu matupu,
Yerusalemu wakumbuka fahari yake.
Ulipoangukia mikononi mwa maadui zake,
hakuna aliyekuwako kuusaidia.
Washindi wake walichekelea kuanguka kwake.
8Yerusalemu ulitenda dhambi mbaya,
ukawa mchafu#1:8 Yerusalemu …mchafu: Yahusu hali ya unajisi ambayo ilihitaji kutakaswa kabla ya mhusika yeyote yule kuweza kumwabudu Mungu kihalali (Lawi 15). kwa dhambi zake.
Wote waliousifia wanaudharau,
maana wameuona uchi wake.
Wenyewe wapiga kite na kujificha kwa aibu.
9Uchafu wake ulionekana waziwazi,
lakini wenyewe haukujali mwisho wake.
Anguko lake lilikuwa kubwa mno;
hakuna awezaye kuufariji.
Wasema:
“Tazama ee Mwenyezi-Mungu mateso yangu,
maana adui yangu ameshinda.”
10Maadui wamenyosha mikono yao,
wanyakue vitu vyake vyote vya thamani.#1:10 Vitu …vya thamani: Vyombo vya thamani kubwa vya hekalu vilivyochukuliwa na Wababuloni (taz Yer 52:17-23).
Naam umeona watu wa mataifa wakiingia hekaluni,
watu ambao Mwenyezi-Mungu aliwakataza
kujumuika na jumuiya ya watu wake.
11Watu wa Yerusalemu wote wanahangaika kutafuta chakula;
hazina zao wanazitoa kupata chakula,
wajirudishie nguvu zao.
Nao mji unalia,
“Hebu niangalie, ee Mwenyezi-Mungu,
ona jinsi nilivyogeuka kuwa duni.
12“Enyi wapita njia, hivi hamjali kitu?
Tazameni! Hakuna aliyepatwa na uchungu kama mimi,
uchungu alioniletea Mwenyezi-Mungu,
siku ya hasira yake kali.#1:12 Siku ya hasira yake kali: Siku ya hasira kali ya Mungu kwa kawaida ilijulikana kama siku ya adhabu itakayokuja nyakati za mwisho wa dunia (pengine kwa maneno “Siku ya Bwana”). Lakini hapa yahusu siku hekalu la Yerusalemu lilipoteketezwa.
13“Aliteremsha moto kutoka juu,#1:13 Aliteremsha moto kutoka juu: Ni wazi kwamba mwandishi analalamika kwamba Mungu mwenyewe ndiye aliyeufanya mji wa Yerusalemu uharibiwe. Watu wakati huo walitambua maneno ya manabii kama vile Yeremia na Ezekieli kuwa ya kweli, kwamba hayo ni matokeo ya dhambi za watu na ni adhabu ya Mungu. Taz Yer 1:16; 30:14; Eze 7:2-4.
ukanichoma hata mifupani mwangu.
Alinitegea wavu akaninasa,
kisha akanirudisha nyuma,
akaniacha nimeduwaa na kuzirai mchana kutwa.
14“Aliyahesabu makosa yangu yote
akayakusanya mahali pamoja;
aliyafunga shingoni mwangu kama nira,#1:14 Makosa yangu …aliyafunga shingoni … kama nira: Dhambi za watu zinalinganishwa na nira nzito ambayo Mungu aliwawekea shingoni (Isa 9:4).
nikafyonzwa nguvu zangu kwa uzito wake.
Mwenyezi-Mungu aliniweka mikononi mwao
watu ambao siwezi kuwapinga.
15“Mwenyezi-Mungu aliwakataa askari walionilinda,
alitangaza wakati maalumu wa kuniadhibu
kuwaponda vijana wangu wa kiume.
Aliwaponda kama katika shinikizo
watu wangu wa Yuda.#1:15 Aliwaponda kama katika shinikizo watu wangu wa Yuda: Picha ya shinikizo hapa ni ile iliyotolewa kutoka kitendo cha kukamua zabibu kupata divai (taz k.m. Isa 63:3 na Yoe 3:13). Na maneno “watu wangu wa Yuda” katika Kiebrania neno kwa neno “binti bikira wa Yuda” maneno ambayo yanatumiwa kuonesha upendo wa pekee kwa watu wa Israeli na Yerusalemu.
16“Kwa sababu ya hayo ninalia,
machozi yanitiririka,
sina mtu yeyote wa kunifariji;
hakuna yeyote wa kunitia moyo.
Watoto wangu wameachwa wakiwa,
maana adui yangu amenishinda.
17“Nainyosha mikono yangu
lakini hakuna wa kunifariji.
Mwenyezi-Mungu ametoa amri dhidi yangu mimi Yakobo,#1:17 Mimi Yakobo: Yakobo alikuwa babu mjukuu wake Abrahamu ambaye ndiye babu wa kwanza wa Waisraeli na hapa jina hilo Yakobo linatumiwa kuwakilisha wazawa wake wote au makabila yote kumi na mbili ya Waisraeli.
jirani zangu wawe maadui zangu.
Naam, mimi Yerusalemu nimekuwa kinyaa kwao.
18“Lakini Mwenyezi-Mungu amefanya sawa
kwa maana nimeliasi neno lake.
Nisikilizeni enyi watu wote,
yatazameni mateso yangu.
Wasichana wangu na wavulana wangu,
wamechukuliwa mateka.
19“Niliwaita wapenzi#1:19 Wapenzi: Taz maelezo ya 1:2. Rejea pia Yer 14:15; 22:20; Omb 2:20. wangu,
lakini wao wakanihadaa.
Makuhani na wazee wangu
wamefia mjini
wakijitafutia chakula,
ili wajirudishie nguvu zao.
20“Ona, ee Mwenyezi-Mungu nilivyo taabuni.
Roho yangu imechafuka,
moyo wangu unasononeka
kwani nimekuasi vibaya.
Huko nje kumejaa mauaji,
ndani nako ni kama kifo tu.#1:20 Maneno haya mazito ya uchungu hapa, ingawa bado ni ya kulalamika, hii ni kama hatua au msingi wa kumrudia Mungu.
21“Sikiliza ninavyopiga kite;
hakuna wa kunifariji.
Maadui zangu wote wamesikia juu ya taabu yangu:
wanafurahi kwamba umeniletea maafa.
Uifanye ile siku uliyoahidi ifike,
uwafanye nao wateseke kama mimi.
22“Uwapatilize kwa ajili ya uovu wao wote.
Uwatende kama ulivyonitenda mimi
kwa sababu ya makosa yangu yote.
Nasononeka sana kwa maumivu
na moyo wangu unazimia.”