Maombolezo 4
BHNTLK

Maombolezo 4

4
Yerusalemu baada ya kuangamia#4:1-22 Katika sura hii Mungu bado anachukuliwa kuwa ndiye aliyetaka Yerusalemu uangamizwe (4:11,16); lakini viongozi wa Yerusalemu (4:12-16) na maadui zake (4:21-22) walisababisha maangamizi hayo.
1Jinsi gani dhahabu yetu ilivyochujuka,
dhahabu safi kabisa ilivyobadilika!
Mawe ya thamani#4:1 Mawe ya thamani: Hapa yahusu aghalabu mawe ya hekalu na vitu vyake vya thamani kubwa. Ingawa hapa yahusu vitu ni dhahiri kwamba hivyo vinaombolezewa kwa vile vinawakilisha watu kama aya 2 inavyoonesha. yametawanywa
yamesambaa barabarani kote.
2Watoto wa Siyoni waliosifika sana,
waliothaminiwa kama dhahabu safi,
jinsi gani sasa wamekuwa kama vyombo vya udongo,
kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3Hata mbwamwitu huwa na hisia za mama
na kuwanyonyesha watoto wao;
lakini watu wangu wamekuwa wakatili,
hufanya kama mbuni#4:3 Mbuni: Ilifikiriwa hapo kale kwamba mbuni walikuwa wakatili na wazembe kwa vile waliyaacha mayai yao uwanjani yaanguliwe (Taz Yobu 39:13-16). nyikani.
4Midomo ya watoto wachanga imekauka kwa kiu,
watoto wanaomba chakula lakini hakuna anayewapa.
5Watu waliojilisha vyakula vinono
sasa wanakufa njaa barabarani.#4:5 Wanakufa njaa barabarani: Kutokana na uvamizi na kuzingirwa muda mrefu kwa mji wa Yerusalemu na majeshi ya Nebukadneza mnamo mwaka 587-586 K.K., njaa kubwa ilitokea humo. (Taz 2Fal 25:2-3).
Waliolelewa na kuvikwa kifalme
sasa wanafukua kwa mikono kwenye majaa.
6Watu wangu wamepata adhabu kubwa
kuliko watu wa mji wa Sodoma#4:6 Sodoma: Mji huu (pamoja na Gomora) uliteketezwa kwa sababu ya dhambi za wakazi wake (Mwa 19:24-25). Kwa kulinganisha, maangamizi ya Yerusalemu yalikuwa makubwa zaidi kwa vile haya yalichukua muda mrefu wa maumivu.
mji ambao uliteketezwa ghafla
bila kuwa na muda wa kunyosha mkono.
7Vijana wa Siyoni walikuwa safi kuliko theluji,
walikuwa weupe kuliko maziwa.
Miili yao ilikuwa myekundu kama matumbawe,
uzuri wa viwiliwili vyao kama johari ya rangi ya samawati.
8Sasa sura zao ni nyeusi kuliko makaa,
wanapita barabarani bila kujulikana;
ngozi yao imegandamana na mifupa yao
imekauka, imekuwa kama kuni.
9Afadhali waliouawa kwa upanga
kuliko waliokufa kwa njaa,
ambao walikufa polepole
kwa kukosa chakula.
10Kina mama ambao huwa na huruma kuu
waliwapika watoto wao wenyewe,#4:10 Mama …waliwapika watoto wao wenyewe: Taz 2:20; Kumb 28:56-57; Eze 5:10.
wakawafanya kuwa chakula chao
wakati watu wangu walipoangamizwa.
11Mwenyezi-Mungu alionesha uzito wa ghadhabu yake,
aliimimina hasira yake kali;
aliwasha moto huko mjini Siyoni
ambao uliteketeza misingi yake.
12Wafalme duniani hawakuamini
wala wakazi wowote wa ulimwenguni,
kwamba mvamizi au adui
angeweza kuingia malango ya Yerusalemu.#4:12 Hawakuamini …kwamba mvamizi … angeweza kuingia malango ya Yerusalemu: Katika karne ya 8 K.K. nabii Mika alitabiri maangamizo ya Yerusalemu (Mika 3:12) naye Yeremia baadaye alifanya hivyo hivyo, akatiwa ndani (Yer 19:15). Kisa ni kwamba kulikuwa na ahadi ya Mungu kwa Daudi kwamba utawala wake ungekuwa salama daima (2Sam 7:14-15); taz pia Zab 48:4-6; Isa 37:33-34.
13Hayo yalisababishwa na dhambi za manabii wake,
yalitukia kwa sababu ya uovu wa makuhani wake
ambao walimwaga damu ya waadilifu mjini kwake.
14Walitangatanga barabarani kama vipofu,
walikuwa wamekuwa najisi kwa damu,#4:13-14 Dhambi za manabii …makuhani … wamekuwa najisi kwa damu: Makuhani kama kawaida walimtambikia Mungu wanyama na damu hekaluni kumwomba baraka lakini sasa damu inayoonekana katika mavazi yao inachukuliwa kuwa najisi kama matokeo ya hatia zao. Damu hiyo imewafanya kuwa najisi.
hata asiwepo mtu yeyote wa kuwagusa.
15Watu waliwapigia kelele wakisema:
“Tokeni, nendeni zenu enyi mlio najisi!
Tokeni, tokeni, msiguse chochote.”
Hivyo wakawa wakimbizi na kutangatanga;
watu wa mataifa walitamka:
“Hawa hawatakaribishwa kukaa kwetu!”
16Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwatawanya,
wala hatawajali tena.
Makuhani hawatapata tena heshima,
wazee hawatapendelewa tena.
17Tulichoka kukaa macho kungojea msaada;
tulikesha na kungojea kwa hamu
taifa ambalo halikuweza kutuokoa.#4:17 Taifa ambalo halikuweza kutuokoa: Hapa yamkini inamaanisha Misri, taifa ambalo lilikuwa limeshirikiana na Yuda dhidi ya adui zao Babuloni. Taz Yer 37:6-10.
18Watu walifuatilia hatua zetu,
tukashindwa kupita katika barabara zetu.
Siku zetu zikawa zimetimia;
mwisho wetu ukawa umefika.
19Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai,
walitukimbiza milimani,
walituvizia huko nyikani.
20Walimnasa yule ambaye maisha yetu yalimtegemea,
yule mfalme aliyewekwa wakfu#4:20 Mfalme aliyewekwa wakfu: Yahusu mfalme Sedekia aliyekuwa mfalme wa mwisho wa utawala wa Yuda na ambaye alichukuliwa uhamishoni Babuloni mwaka 586 K.K. (2Fal 25:2-7). wa Mwenyezi-Mungu,
yule ambaye tulisema: “Chini ya ulinzi wake
tutaishi miongoni mwa mataifa.”
21Wakazi wa Edomu,#4:21-22 Edomu: Hii ilikuwa nchi kusini ya Bahari ya Chumvi. Katika Biblia kuna ujumbe mwingi dhidi ya Edomu: (taz Zab 137:7; Yer 49:7-22; Eze 25:12-14; Obadia 10:15). “Uzi”: Eneo au mahali panapoitwa kwa jina hili hapajulikani. mwaweza kushangilia kwa sasa,
mwaweza kwa sasa kufurahi enyi wakazi wa Uzi;
lakini kikombe hiki cha adhabu kitawajia pia,
nanyi pia mtakinywa na kulewa,
hata mtayavua mavazi yenu!
22Adhabu ya uovu wako ewe Siyoni imekamilika;
Mwenyezi-Mungu hatawaacha zaidi uhamishoni.
Lakini nyinyi Waedomu atawaadhibu kwa uovu wenu,
atazifichua dhambi zenu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza